MINZIRO (KUSHOTO) |
NA SALEH ALLY
TUMEZUNGUMZA mengi sana kuhusiana na suala la kutoa nafasi kwa makocha wazawa katika kufundisha timu kubwa na ikiwezekana hata timu zetu za taifa.
Sote tunajua kwamba kuna makocha wazalendo wamekuwa wakifanya kazi yao kwa juhudi kubwa na mafanikio tumekuwa tukiyaona.
Makocha hao wazalendo wamefanikiwa kuzisaidia timu zao kubeba makombe au kufanya vizuri wakiwa sehemu ya kujenga mfano bora wa soka nchini.
Tunajua makocha mbalimbali kama Selemani Matola, Fred Felix Minziro, Abdallah King Kibadeni, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, David Mwamwaja na wengine wengi.
Lakini wapo kama kocha wa Prisons ya Mbeya, Abdallah Mohammed ‘Bares’, Ali Bushiri aliyewahi kuwa kocha msaidizi wa Taifa Stars na wengine wengi ambao wamekuwa wakijitahidi.
Ubora wa makocha wa Kitanzania umekuwa na msaada katika kukua katika ligi au soka lakini lazima tukubali thamani wanayopewa ni ndogo sana.
Tumekuwa tukitumia muda mwingi kuzungumzia upungufu wao unaowafanya kufeli na kwamba wanatakiwa kurekebisha mambo katika nyanja mbalimbali ili waweze kupiga hatua.
Mara kadhaa, tumewakumbusha kwamba waache kuwa waoga na huu ni wakati mwafaka wa kutaka kwenda au kutamani kuingia katika nchi za watu ili nao wakutane na changamoto tofauti zitakazowafanya wazidi kukua.
Kawaida, unapokuwa mbali na nyumbani mwili na akili kwa ujumla unataka kupambana. Kuendelea kubaki nyumbani tu wakati mwingine ni sawa na kudeka!
Suala la kwenda nje kwa wingi, hilo halina mjadala maana tunaona namna makocha wa nchi kama Kenya, Uganda na sasa hadi Burundi wanaingia kwa wingi Tanzania wakati sisi hapa kwetu wanakuwa waoga kwenda kupambana na changamoto ya nje ya nchi.
MATOLA. |
Changamoto zaidi ni msaada wa kukua. Hivyo ni lazima kupambana na kufanya mambo yaende kwa maana ya kupiga hatua.
Ninaamini hayo ambayo tumekuwa tukiwaeleza kwa nia njema kabisa ya kutaka wajue, wameyasikia na kuyafanyia kazi na tutaendelea kuwahimiza na kuyakumbuka tena. Pamoja na hivyo, basi vizuri wakati wao wakiwa katika zoezi la kujirekebisha, basi wahusika kwa maana ya viongozi wa klabu lazima wafanye linalowezekana katika suala la maslahi kwa makocha wazawa. Waungwana, hawa ni wanadamu na wangependa kupata zaidi kimaisha ili wapige hatua.
Kupiga hatua vizuri kwa maana kwamba wanalipwa vizuri na hii itaongeza morali kwao kuendelea kuithamini kazi yao badala ya kuendelea kuamini kwamba wanastahili kuifanya kwa weledi zaidi na kupiga hatua.
Kuwalipa vizuri ni kuwakuza na kuwapa nafasi ya kuamini zaidi ya awali kwamba kazi yao ni muhimu sana na inaweza kuwaendeshea maisha kwa kuwapatia kila wanachohitaji.
Lakini kuwaongezea au kuwapa maslahi mazuri ni kuwafanya wajenge hisia za kuifanya kazi yao kwa ufasaha zaidi kwa kuwa ndiyo inayowajali.
Ndoto za mwanadamu kutimiza jambo fulani, fedha inakuwa matokeo. Lakini fedha ikiwa ni sehemu ya mafanikio inasaidia kukuza nuru ya hisia za upambanaji kutafuta mafanikio sahihi.
Kocha anayetokea Rwanda, Burundi au Uganda anaweza kupewa maslahi ya juu mara tatu ya yule wa nyumbani
Tanzania. Huenda neno mgeni linawababaisha viongozi wengi wa klabu?
Kama ni hivyo basi hawako sahihi na wanapaswa wao kuwa wa kwanza kuonyesha thamani kwa makocha wazawa ili nao wabadilike. Tukubali wako wazawa wengi wamepata mafanikio kuzidi wageni na wako wageni wengi wamevurunda hata kuliko wazawa.
Kikubwa wazawa waendelee kujifunza kupitia wageni lakini viongozi wa klabu wawajali wazawa kuwapa changamoto ya kukua zaidi.
0 COMMENTS:
Post a Comment