March 28, 2018


Na George Mganga

Kocha wa Taifa Stars, Salum Mayanga, anahusishwa kuondoshwa kuitumikia timu hiyo akiwa ameiongoza kucheza jumla ya michezo 16 tangu aanze kuifundisha.

Mayanga alitangazwa kukichukua kikosi cha Taifa Stars kutokea kwenye mikono ya Charles Boniface Mkwasa ambaye ni Katibu Mkuu wa klabu ya Yanga kwa sasa.

Ukiangalia rekodi za Mayanga, zinaonesha ameiongoza timu hiyo katika mechi 16 huku akiwa amepoteza michezo miwili pekee.

Mayanga vilevile ameenda sare michezo 7 tangu aanze kukinoa kikosi hicho cha Stars na akiwa ameshinda mechi 7.

Kwa rekodi hizi bado inaonesha Mayanga anapaswa kupewa nafasi ya kuendelea kukinoa kikosi cha Stars licha ya kushindwa kuipa mataji timu hiyo.

Wapo baadhi ya wadau wamekuwa wakieleza kutofurahishwa naye haswa katika uteuzi wa kikosi pamoja na timu inavyocheza kwenye mashindano wakidai kuwa kiwango hakiridhishi.

Yawezekana kutofanya vizuri pia katika mashindano mbalimbali ndiyo sababu ya Mayanga kulaumiwa na kuanza kuhusishwa aondoke.

Siku kadhaa zilizopita Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Wilfred Kidao, alinukuliwa akisema wameanza mchakato wa kumpata Kocha atakayechukua nafasi ya Mayanga.

Kwa kauli kama ile ukijumlisha na hizi za baadhi ya wadau wa soka zinaonesha kabisa kuwa Mayanga hapewi motisha ya kutosha kwenye nafasi yake kuendelea kuinoa Stars. Inadhihirisha ipo mashakani.

Nadhani ifikie wakati tujaribu kuwa na uvumilivu na si kutegemea kupata mafanikio makubwa ndani ya siku moja. Unaambiwa ng'ombe hawezi kunenepa siku ya mnada kama alikuwa hajapata marisho ya kutosha tokea utotoni.

Juzi hapa kaka yangu Haji Manara, alieleza kuwa inabidi taifa liitishe mjadala wa kujadili tatizo la timu yetu ya Taifa kushindwa kufanya vizuri ilihali ilishaleta 'Sampuli' ya kila Kocha kuinoa Stars.

Tatizo kubwa linaloikabili Stars kwa jicho la ndani ukija kutazama vizuri utagundua hata Makocha hawahusiki, vipi kuhusu ubora wa ligi yetu?

Tuna akademi za kutosha kuanzisha msingi wa soka kuanzia ngazi ya chini kabla ya kufika huku juu? Ni baadhi ya maswali ambayo tunapaswa kujiuliza.

Mipango inayofanywa kwenye Ligi Daraja la Kwanza, shutuma za baadhi ya viongozi kuzipandisha baadhi ya timu mpaka Ligi Kuu unadhani zitaweza kuleta matokeo chanya kwenye kikosi chetu?

Tuna wachezaji wachache sana ambao wanacheza soka la nje, na hatuwezi kuwategemea peke yao kuweza kuinua soka letu.

Ifikie wakati kuwe na mipango mikakati endelevu ya kuimarisha soka la vijana kuanzia mashuleni, haswa shule za msingi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma ambapo hamasa kubwa ilikuwa katika mashindano ya UMITASHUMTA iliyokuwa ikiibua vipaji vya wachezaji.

Tusimhukumu Mayanga wakati tulishakuwa na Makocha wengi walioifundisha Stars hata wasio wazawa. Tuangalie ligi zetu za ndani kwanza kama zinaendeshwa kiuhalali bila mipango mipango, figisu na rushwa ambayo inaua mpira wa nchi hii.

3 COMMENTS:

  1. fact: kwa wakati huu timu ya taifa inatakiwa kuwa na kocha mzawa kwa sababu "interaction"yake na wachezaji kabla/na wakati wa mchezo huchangia mafanikio ya timu hususan timu yetu bado vijana wengi wanacheza hapa hapa tz.kwenye soka la vijana tuendelee na hao hao wazungu itafika wakati national team itahitaji kocha wa kigeni kufundisha lakini kwa sasa nafikiri si kwa mayanga tu lakini kwa wakati huu timu yetu ya taifa inahitaj kocha mtanzania.'we have seen how national players with confidence talking to manager every time the referee stopped the game Y'sterday against congo.It was amazing seeing players talking friendly that way.we win we win all/we lose we all lose'Tanzania kwanza
    p,methew
    udsm

    ReplyDelete
  2. Silazima apewe maana malengo hayajatimia mfano CHAN hatukucheza nayeye amechangia sana tena sana

    Mpaka Leo timu unaona inautofauti kwa mechi 2 ambazo Hemed yupo tatizo lake kukalili wachezaji na substitute zake tatizo na ukiangalia kwa mbali Usimba na Uyanga unamponza

    ReplyDelete
  3. Bado Tanzania hatuna kocha anaeweza kuisimamia timu yetu ya Taifa hata kwa miaka mia moja kwenda kupata ushindi mbele ya Timu za Taifa kama Misri, Nigeria, Tunisia,Algeria, Ghana nakadhalika. Watanzania wengi tuna upeo mdogo sana wa kufikiria vitu vikubwa zaidi. Mwengine anasema Timu ya Taifa lazima apewe mzawa? Kwa rekodi gani ya kiuchezaji na mataji kama kocha aliyonayo huyo mzawa? Katika Timu zinazowakilisha Africa katika kombe la Dunia ni Timu moja au mbili zenye makocha wazawa. Ikiwa Misri hawajapata mzawa wa kumuamini kumpa timu yao Taifa sisi Tanzania huyo kocha mzawa wa kwenda kushindana na makocha wazawa wa Misri tutampata wapi? Viongozi wengi soka nchini ni wenye kulichukulia suala la mpira kirahisi rahisi tu kiasi cha kuwadumaza watanzania kifikra. Ningetamani sana angepatikana Magufuli wa kwenye soka katika uongozi wa mpira Tanzania. Mtu ambae anauwezo wa kuthubutu kufanya mambo makubwa hata yanaonekana na wengi hayawezekani. Timu yetu ya Taifa Tanzania tunao uwezo kabisa wa kula sahani moja na mataifa mengine yenye nguvu kisoka barani Afrika kama tutakuwa na viongozi wenye kuthubutu na wanaowajibika. Ukiangalia sasa tunawachezaji ambao tunaweza kusema vizazi vya zahabu lakini dhahabu bila Sonara mahiri wa kuisanifu kamwe haiwezi kuwa na thamani yake halisi. Tanzania tunahitaji Kocha mwenye uwezo zaidi mwenye upeo wa kimataifa wa kutuondoa hapa tulipo.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic