March 28, 2018



Na Saleh Ally

Takribani wiki mbili sasa ndani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), hakuna jambo la maendeleo ambalo linazungumziwa badala yake mizengwe na kuchafuana.
Gumzo la nani hafai na nani anafaa ndiyo limechukua sura kubwa ya maisha mapya ya TFF ambayo ninaamini wako waliokuwa na matumaini makubwa kuhusiana na suala la maendeleo.

Kuna mambo mengi sana hayana majibu na huenda yametumika kuwabadilisha wengi walioamini chini ya Urais wa Wallace Karia, basi mambo yatakwenda vizuri kabisa.

Kwa sasa gumzo ni aliyekuwa Makamu Rais wa TFF, Michael Wambura ambaye amefungiwa maisha kujihusisha na masuala ya soka akipatikana na tuhuma kadhaa ikiwa ni pamoja na kupokea malipo ambayo yanaonekana hayakuwa sahihi, pia kushusha hadhi ya shirikisho.

Wambura amekuwa akipinga hilo na ametumia nguvu kubwa huku akieleza mambo mengi yakiwemo mengine ambayo yanaonekana si ya msingi kwa kuwa anayesema baada ya kuona ameondolewa wakati akiwa ndani ya TFF hakuwahi kusema jambo, kwamba mambo yanaharibika.

Sasa anasema kwa kuwa ametolewa na huenda kwa kuwa anaamini ameonewa na vinginevyo. Ndiyo maana kwangu naona kama anazungumza maneno ambayo alipaswa kuyasema mapema kama alipingana nayo, kwa kuwa alikaa kimya, kila kibaya anachokisema sasa, basi naye alishiriki akiwa kiongozi kwa kuwa kama aliyeharibu ni Karia, msaidizi wake ni yeye!


Msimamo wangu umekuwa hivi, kama Wambura ana hatia, achukuliwe hatua na iwe funzo kwa wengine kwa kuwa tumechoshwa na mambo yasiyoisha yanayokosa weledi ndani ya mpira.

Lakini kama hana hatia, basi apewe nafasi ya kuendelea na kazi yake. Naweka msisitizo, kuondoka kwake isiwe ni fitna naye asijenge njia ya kutaka kuwaonyesha watu kwamba baada ya yeye kuondolewa TFF kuna shida sana au ilikuwepo kubwa sana.

Maana hoja ya msingi, atueleze au agombee kurejea katika nafasi yake kwa kupita katika njia sahihi badala ya maneno mengi.

Lakini kama utatulia katika hiki kinachoendelea, inaonyesha wazi sasa ndani ya TFF ni vita ya madaraka, jambo ambalo limeturudisha nyuma kwa muda mrefu sana.

Huenda usingekuwa wakati mwafaka kusikia suala la vita ya madaraka kwa kipindi  hiki kwa kuwa TFF imefanikiwa kuwaleta viongozi wakuu wa soka duniani, ukianza na Rais wa FIFA, Gianni Infantino na Rais wa Caf, Ahmad Ahmad. Hii ni mara ya kwanza kabisa.

Heshima kubwa iliyopata Tanzania ilipaswa kuwa mfano na muendelezo sahihi. Lakini sasa gumzo ni vita ya madaraka na kusikia mambo mengi nje ya mpira kama yale mazengwe ya fulani si raia mara fulani si raia.
Inaonyesha wazi ndani ya TFF kuna chuki kubwa na makundi ambayo yakiendelea kuwa na nguvu zake, maana yake ndoto ya kuendeleza mpira wetu itabaki kuwa ya mchana na isiyo na hatua.

Tumechoka waungwana, tunataka maendeleo na dhamana mliyopewa ni kuendeleza mpira na si kushambuliana. Aliye mchafu aondoke, aliye na haki abaki na kusiwe na uonevu.

Hadi leo Fifa inashikilia zaidi ya Sh bilioni 3 za Tanzania katika suala la maendeleo ya mpira. Hii yote ilitokana na uongozi duni. Sasa tunaingia kwenye migogoro mingine ambayo kama kukifuatwa utaratibu sahihi hakuwezi kuwa na kinachoendelea.

TFF isimame imara ituonyeshe kama haijakosea, na kama kinachofanyika ni sahihi, kimefuata katiba basi nguvu irudishwe katika maendeleo kwa kuwa tunataka kusikia hatua zikipigwa kuujenga mpira wetu ambao kukua imekuwa ni hadithi.

Hi hivi, Wambura ajibu hoja za msingi atueleze zile tuhuma alizopatikana nazo na hatia ni sahihi au la na kwa nini.
Hali ilivyo, inaonyesha kila mmoja wenu anachoangalia ni madaraka anayoyataka na inaonekana ni kwa faida zenu na si kwa faida ya mpira wetu.

Vizuri hili linalozunguka, lifikie liishe katika njia sahihi. Halafu baada ya hapo tuanze kusikia mipango ya maendeleo ya mpira wa Tanzania.

TFF wakati ikiendelea na hili la Wambura, niwakumbushe tunachotaka ni maendeleo ya mpira na si kila kitu kionekane kimesimama kwa kuwa Wambura kasimamishwa.

Kwa Wambura, kikubwa apate haki yake, iwe kufungiwa kama ana hatia au kurudishwa kama hana hatia. Lakini naye asijaribu kuvuruga mambo kwa kuwa yeye hayupo.

Tunataka mpira uendelee, tunataka maendeleo ya mpira na si maneno yasiyo na mwisho. Tumechoshwa na haya na tumeyasikia kwa miaka mingi huku mpira ukiendelea kudorora.

2 COMMENTS:

  1. Jembe ebu acha kuonesha upande kama kweli unazungumzia ukweli na kama hutumiwi kama wengine tunaowasikia, ungesema kuwa kama Wambura kaonewa waliomuonea wanapaswa kuwajibishwa kwa sababu wamemchafulia jina na hayo ndio maadili. Ila si kusema kwamba aendelee na wadhifa wake pasi kuwaonya na kuwachukulia hatua wale waliohusika kumchafua. Haki itendeke kote kama ana hatia aadhibiwe na kama hana hatia waliomchafua wawajibishwea. Pili, hoja ya kwamba yale anayoyasema Wambura yangekuwa na mashiko kama angeyasema kabla hajafungiwa si hoja ya kisomi wala ya kimantiki. uhalali wa kosa kuwa kosa au si kosa hautambuliwi na muda. Hata kama, anayoyasema kama yana ukweli yatabaki kuwa kweli si kwa sababu yamesemwa lini. Kufungiwa kwakwe inabidi kuwe chachu ya kuibua na mnengine ambayo hatukuwai kuyasikia yale ya ovyo ili TFF nzima isafishwe. Kinachotakiwa ni kuyachunguza madai yake kama yana mashiko wahusika waadhibiwe na kufungiwa kwake kusiwe hoja ya kuhalalisha uharamu wa TFF, kisa hakuyasema mapema. Pia, kama unamhukumu kuwa kwa kuwa Karia amekosea basi na Wambura ni mkosaji kwani yeye alikuwa ni msaidizi wake, basi kanuni hiyohiyo itumike kumhukumu Karia kwani kama wasaidizi wake wanakosea na yeye amekosea pia maana ilibidi ashirikiane nao kuwakosoa.

    ReplyDelete
  2. Ndugu Jembe usijifanye huelewi kilichojiri kuwa kuna ngoma ya Malinzi na ngoma ya Karia.Sasa sie wadau wa soka Tanzania tucheze ngoma ya nani? Huyu kamwaga ugali na yule kanwaga mboga.Ni siri gani iliyojificha zaidi ya fumbo la Bilioni tatu zilizo lala kwenye coffer ya FIFA?
    Karia team haitaki kuendeshwa kwa remote control na pambaneni maana si vita ndogo hiyo

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic