March 26, 2018





Na Saleh Ally, aliyekuwa Cairo
CAIRO ni mji mkuu wa Misri, ukifanikiwa kufika ni jiji hasa na ndiyo mji wenye watu wengi kwa maana ya wazi kuliko miji mingine yote ya Bara la Afrika.

Cairo iko katika 10 Bora ya miji yenye wakazi wengi zaidi duniani ikiwa inashika nafasi ya tisa baada ya Osaka, Japan iliyo nafasi ya nane na Dhaka, Bangladesh ndiyo inafunga hiyo 10 bora.

Wakazi takriban milioni 20, wanaishi katika jiji hilo ambalo linaongoza kwa barabara za juu kuliko mji mwingine wowote wa Bara la Afrika.


Takwimu za makazi zilizotolewa mwishoni mwa mwaka jana zinaonyesha Tokyo, Japan ndiyo inaingoza kwa kuwa na wakazi wengi duniani, wako milioni 38, wakifuatiwa na Delhi India wenye milioni 28, Shanghai, China milioni 25, Beijing, China milioni 23 na Mumbai, India milioni 22 na ushee.

Kama si mtu unayependa kuwa katika kundi la watu au sehemu yenye watu wengi, unaweza kuona kero kuwa Cairo, lakini ni mji wenye vivutio vingi sana.

Unapokuwa katika Jiji la Cairo unaweza kushangazwa na jambo moja, kama ni mpenda mpira utavutiwa nalo na kama si mpenda soka, basi unaweza kujiuliza maswali mengi sana.


Kuna picha za mshambuliaji nyota wa Liverpool, Mohamed Salah, maarufu kama Mo Salah ambaye anaonekana karibu kila sehemu ya jiji hilo.

Salah ndiye shujaa wa Misri na sasa, kila kampuni kubwa ya biashara inaamini mambo kwenda vizuri lazima ifanye biashara na Salah.

Kiungo huyo mshambuliaji wa Liverpool kwa sasa ndiye kinara wa kupachika mabao katika Ligi Kuu England akiwa na mabao 28 akifuatiwa na mpinzani wake, Harry Kane wa Tottenham mwenye 24.

Umaarufu wa Salah ndani ya nchi yake ya Misri umepanda kwa kiasi kikubwa ukizungushiwa wigo wa heshima ya juu baada ya kuifungia timu ya taifa bao katika dakika za lalasalama dhidi ya Congo na kuiwezesha kurejea katika Kombe la Dunia baada ya miaka 28.

Nyota waliopendwa na kuaminika kupita kiasi kama akina Abou Trika waliishindwa kazi hiyo. Salah, maarufu kama Messi wa Misri, ameweza na amezidi kujenga heshima kubwa kwa nchi yake ya Misri.

Hii imefanya makampuni yote kuona kufanya naye kazi ni kutengeneza imani kubwa kwa wateja wao na inakuwa hivyo si kwa sababu ya mafanikio pekee badala yake pia tabia yake.

Tabia ya Salah ni utulivu, mtu asiye na makuu na watu wa Misri wanafurahishwa zaidi kwamba si mtu anayebweteka na mafanikio aliyoyapata na hana mbwembwe za kuchora tatu, kusuka nywele au mambo ambayo yangekuwa ni kuonyesha amelewa sifa.


Katika mitaa ya Jiji la Cairo na hata ule Mji wa Port Saidi ulio Kaskazini Mashariki mwa Nchi ya Misri, bado kuna mabango mengi ya Salah.

Karibu kila barabara inayopitisha watu wengi, unaweza kukutana na mabango zaidi ya 10 ya Salah na mabango hayo ya matangazo ya barabarani yanakuwa ya makampuni mbalimbali ambayo yameingia mkataba na nyota huyo.

Imeelezwa Salah sasa ana uwezo wa kuingiza zaidi ya dola milioni 10 kupitia matangazo mbalimbali ambayo ameyapata kwao Misri.


Utajiri wake sasa si kutoka Ulaya, badala yake ile hali ya thamani ya juu aliyopewa nchini kwao, inamfanya kuzidi kuingiza fedha nyingi zaidi na inaelezwa kuwa, Salah haonyeshi kwamba ana mabadiliko makubwa katika kipato kutokana na aina yake ya maisha kuendelea kubaki ilivyo.

Kampuni ambayo inamuingizia fedha nyingi ni ile ya simu ya Vodafone na ndiyo yenye mabango mengi makubwa ya Salah katika sehemu nyingi za miji ya Misri na hasa Cairo.


Ingawa wamekuwa wakificha kiwango cha fedha alizopewa ikielezwa, Salah ameweka msisitizo kutotaka kuonekana ni mwenye fedha nyingi. Pia runinga maarufu ya michezo ya On Sports, nayo imeingia naye mkataba ingawa mkataba huu unaanzia kutoka kwa timu ya taifa ya Misri kupitia shirikisho lao na inamjumuisha Salah na wachezaji wengine wa timu ya taifa.

Kampuni ya vinywaji baridi ya Pepsi, nayo haijajivunga hata kidogo. Imempa Salah mkataba wa mwaka mzima na tayari mabango yameenea karibu kila eneo la mitaa maarufu Salah ‘akijimwaga’ na soda za Pepsi.

Kampuni ya usafirishaji ya Uber kwa Misri, nayo inamwaga mamilioni kwa mwaka kwa Salah baada ya kuingia naye mkataba wa kuwa balozi wake.

Kama hiyo haitoshi, benki kubwa ya Alex ya Misri imekubali kuingia mkataba na Klabu ya Liverpool na mabango yake yanatumika yakiwa na picha za wachezaji wa Liverpool wakiongozwa na Salah.

Pamoja na kujua Liverpool ina mkataba na benki nyingine, lakini benki hiyo ya Misri haikuona shida na mambo yalivyokuwa sawa, wameingia mkataba lakini Salah ana mkataba wake pembeni.

Kwa sasa mashabiki wa Arsenal nchini Misri kwa asilimia 14.5% wamehamia Liverpool, Manchester 9.3%, Chelsea 3.3% na Manchester City 1.2% na hawa wote wanaelezwa kujiunga na Liverpool kutokana na umahiri wa Salah na heshima kubwa anayoipa nchi yao ughaibuni na duniani kote.

Wako ambao wamehamia wakiamini kufanya hivyo ni kumuunga mkono Salah ambaye ndiye shujaa wa nchi yao kwa kipindi hiki na unapaswa kukumbuka kwamba Misri, ni wendawazimu hasa wa mchezo wa soka.

1 COMMENTS:

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic