NA SALEH ALLY
WOTE tunakubaliana kwamba Yanga na Simba ni timu za Watanzania na wanaopaswa kuziunga mkono zaidi ni Watanzania wenyewe.
Wale ambao wana itikadi zinazowalazimisha kushangilia au kuzomea, ni raha zao tunaweza kuwaachia lakini haizuii kuwaeleza ukweli kwamba wanachofanya si sahihi.
Mimi nabaki palepale, kwamba unaweza kuwa na ushabiki wakati upinzani ukiwa nyumbani, yaani ligi ya nyumbani lakini inapofikia suala la kuwakilisha taifa letu, watu waungane.
Ambao hawataki wana haki kwa kuwa ni hiyari lakini kama wanadamu wanapaswa kujifunza na kuacha kuwa fuata mkumbo wakiangalia mambo yaliyopitwa na wakati kama mapya au kutaka kufanya ili waonekane.
Unaona hauwezi kuiunga mkono Yanga wakati inacheza michuano ya kimataifa, basi unaweza kukaa kimya na kuwaacha wachache wanaoweza kubadilika kwa kuwa wanaelewa maana ya uzalendo wakafanya hivyo. Yaani baki na yako moyoni.
Yanga inakwenda kucheza mechi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Township Rollers ya Botswana. Inakwenda katika mchezo mgumu kabisa kwa kuwa tayari imepoteza nyumbani kwa kufungwa kwa mabao 2-1.
Simba nao wanakwenda Misri, huko watakutana na Al Masry ambayo katika mechi ya kwanza jijini Dar es Salaam, Simba walilazimika kusawazisha na kupata sare ya mabao 2-2.
Hakuna mechi rahisi hata kidogo kati ya hizi mbili na hatupaswi kudanganyana hata kidogo kwamba Yanga au Simba zinakwenda kupita kirahisi tu kutokana na namna mambo yalivyo na mpira unadunda.
Yanga na Simba wanaweza kusaidiwa na mambo mawili makubwa ambayo wakiyafanyia kazi basi wanaweza kupita katika mechi hizo kabisa kuliko wanavyozitarajia.
Kwanza ni kuwaeleza kweli mechi hizo ni ngumu na hakuna lelemama na kama wanataka kupita wanapaswa kunuia kweli na kuzifanyia kazi kwa juhudi na maarifa na kila mmoja akiwa amejitoa hasa kwamba ni ngumu na anapaswa kupambana kwa kiwango chake cha juu kuliko siku zote.
Pili ni nafasi ambayo wameipata, kuwa ukali wa Rollers na Al Masry wameshaujua kwa kuuonja. Sasa si kwa takwimu, kusikia tu au kuhadithiwa kuhusiana na timu hizo, badala yake wamecheza nazo na wanajua kila kitu na mambo yalivyo.
Maana yake, wanajua mengi kiufundi kuhusiana na uwezo wa timu hizo wakianza kuchambua mchezaji mmojammoja aliyekuwa nje hadi walioingia.
Wanajua wanaweza kufanya nini kupitia makosa ambayo wameyafanya na nini cha kufanya na hasa kuhusiana na wafanye nini kuzuia au kumalizia.
Uwezo walionao Al Masry au Rollers ni mkubwa lakini si mkubwa ambao unashindikana Simba au Yanga kushinda ugenini. Kama wakijiamini na kufanya kazi yao kwa usahihi na hesabu za uhakika nafasi ya kupita ugenini pado wanayo.
Kitakwimu, inaonekana nafasi ya Yanga au Simba kupita ugenini ni ndogo na wanaweza kuitanua na kuwa nafasi kubwa kutokana na wenyewe watakavyofanya maandalizi yao na baada ya hapo maandalizi hutakiwa kufanyiwa utekelezaji.
Maana yangu kuwa Yanga na Simba, hawapaswi kujiandaa kwa maneno tu. Unajua, mipango huanza na maneno, maelekezo na kadhalika lakini baada ya hapo unafuatia utekelezaji.
Utekelezaji ndiyo sehemu sahihi hasa ambayo inatakiwa mambo yaende katika ubora wa asilimia 90 na zaidi na hapo ndiyo ile mipango iliyopangwa kwenye karatasi, kwenye vikao au majaribio uwanjani inaweza kufanya kazi.
Simba au Yanga, hawatakiwi kuwa waoga hata kidogo hasa linapofikia suala la kupambana kwa kuwa Rollers au Masry hawana uwezo wa kuwashikia panga. Badala yake ni mapambano ya ujuzi yanayohitaji umakini mkubwa lakini moyo wa kuamini inawezekana kupitia utendaji bora.
Kila la kheri kwenu.








0 COMMENTS:
Post a Comment