MUNICH, Ujerumani
HATIMAYE ni sahihi kusema kuwa Bayern Munich itakuwa timu ya kwanza kutwaa ubingwa barani Ulaya kwa msimu huu baada ya juzi kupata ushindi mnono.
Bayern ambayo inawinda ubingwa wa Bundesliga wa mara sita mfululizo, ilifanikiwa kuichapa Humburger mabao 6-0 kwenye mchezo uliokuwa wa upande mmoja.
Robert Lewandowski, alifanikiwa kufunga mabao matatu kwenye mchezo huo na kujiweka kwenye nafasi nzuri sana ya kutwaa ubingwa huo.
Mashabiki wanaotazama ligi hiyo kupitia King’amuzi cha Startimes waliwaona Bayern wakionyesha kiwango cha juu sana dhidi ya timu hiyo ambayo haina matumaini yoyote msimu huu.
Humburg huu ulikuwa mchezo wao wa 13 wanacheza bila kushinda na kuendelea kujiweka kwenye wakati mgumu wa kubaki kwenye ligi hiyo.
"Tumecheza vizuri leo nafikiri kiwango tulichokionyesha kilikuwa sahihi kwetu huu ndiyo uwezo wetu wa kila siku kama tutakuwa tunataka ushindi.
“Lazima tukubali kuwa tuna uwezo wa juu na mashabiki wetu wanataka kutuona tukiuonyesha uwanjani," alisema kocha wa Bayern, Jupp Heynckes, ambaye wiki hii timu yake itacheza na Besiktas kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya ikiwa na nafasi kubwa ya kufuzu baada ya ushindi mnono katika mechi ya kwanza.
Zikiwa zimebaki mechi nane kwenye Bundesliga, Bayern wapo mbele kwa pointi 20, dhidi ya Schalke ambao wanashika nafasi ya pili baada ya juzi kushinda kwa bao 1-0 dhidi ya Mainz.
"Haijalishi kama tupo mbele kwa pointi 10, 15 au 20 bali tunachotakiwa ni kuhakikisha kuwa tunaendelea na kasi hii kwenye Ligi Kuu ya Ujerumani, hadi mwisho wa msimu huu,” alisema staa wa timu hiyo Arjen Robben.
Bayern wamekuwa na rekodi nzuri nyumbani kila wanapocheza na Hamburg na iliwachukua dakika nane tu kuongoza kwa bao lililofungwa na Franck Ribery.
Dakika nne baadaye Lewandowski aliifungia timu yake bao la pili baada ya kupata pasi ya Joshua Kimmich.
Dakika ya 19, Mpolandi huyo aliifungia timu yake bao la tatu, Robben akafunga la nne, huku Ribery akipiga la tano dakika ya 80 na Lewandowski akamaliza kazi kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 85.
Wakati hali ikiwa hivyo, vijana wa Bayer Leverkusen wenyewe walikwea hadi nafasi ya tatu baada ya kuichapa 2-0, Borussia Moenchengladbach.








0 COMMENTS:
Post a Comment