April 9, 2018




NA SALEH ALLY
SUALA la utani kwa watani Yanga na Simba wala si geni, hawa wana haki ya kutaniana katika mambo mbalimbali hata nje ya mpira.

Kwa wale wafuatiliaji wa klabu za Yanga na Simba mnajua, kwamba hata katika misiba, mfano Simba wamefiwa, Yanga ndiyo wanasimamia msiba wote na Simba wanapumzika kama wafiwa. Lakini wakati wa shughuli yote ya msiba, Yanga wanafanya huku wakiporomosha mengi kuhusiana na utani.

Utani wa namna hiyo upo hata katika makabila mbalimbali ya Kitanzania. Kama haujui unaweza kukwazika kuona mtu akifanya mambo ya utani wakati watu wamefiwa.
Yanga na Simba ni ndugu, ni watu waliokuwa pamoja katika maisha ya kawaida na wameishi mtaa au nyumba moja, mkoa au wilaya moja, kitongoji kimoja na kadhalika.

Shida, kizazi cha sasa kinaonekana kimekuwa hakijifunzi hata kidogo kuhusiana na haya yanayoendelea kwamba yalipita wapi kabla ya kufikia hapa yalipo. Niseme wengi wamedandia na hawakutaka kujifunza hata kidogo na hili limekuwa jambo baya sana.

Ndiyo maana unaona, siku hizi mwenye matusi mengi anaweza kuonekana anajua mengi sana kuhusiana na mpira wa Tanzania au Yanga na Simba. Vijana wanaopenda mpira kipindi hiki kwa kuwa hawajajifunza mengi au kusoma, au kukubali kusimuliwa wanakuwa hawajui kabisa, hivyo kila linapoibuka suala, wanalihitimisha kwa matusi, nashangazwa sana na watu wa namna hii.

Chanzo cha kuandika Metodo ya leo ni wasemaji wa Yanga na Simba, yaani Dismas Ten na Haji Manara. Hawa wawili wamekuwa katika mlolongo mrefu wa kujibizana mitandaoni.

Gumzo lao limeshika kasi hasa baada ya Yanga kutengeneza tangazo la kuwahamasisha watu kwenda uwanjani kwa ajili ya kuiunga mkono Yanga ambao ni wawakilishi pekee wa Tanzania katika michuano ya kimataifa kwa sasa wakicheza dhidi ya Dicha ya Ethiopia.

Tangazo hilo lilikuwa na akina dada au kina mama wanne. Manara naye aliamua, ninaamini kutania au kutoa maoni yake akiona waliokuwa kwenye tangazo hilo hawakustahili hata kidogo.

Manara aliamua kutumia neno “Mitulinga”, hii ilionekana kumkera Dismas Ten, sijajua kwa kuwa aliandaa tangazo, au walivyoitwa waliokuwa katika tangazo. Naye akamkumbusha Manara kwamba watu hao waliwahi kumchangia akiwa mgonjwa akikaribia kwenda kutibiwa India. Baada ya hapo, Manara naye akajibu akieleza fedha alizotumia India na walizochangia watu wa Yanga akikumbushia Jerry Muro ndiye alihusika zaidi na si Dismas Ten.

Basi yamekuwa ni malumbano ambayo kweli katika mpira wa Tanzania hayana hata chembe ya tisa. Ni maneno ya kitoto sana ambayo yanapaswa kupuuzwa kabisa na huenda kama ilikuwa utani, nafikiri wasemaji hao hawakupaswa kufika mbali zaidi.

Wakumbuke wao wanaziwakilisha klabu kubwa za Yanga na Simba na wanapaswa kujipambanua kuwa tofauti. Yanga na Simba ni kubwa sana. Kuziwakilisha unalazimika kujitambua na kuacha mambo mengi sana. Lakini mwisho niwakumbushe wanachobishana kinawahusu dada na mama zetu.

Katika Kamusi ya Visawe, neno “mtulinga” ni mfupa wa bega, mitaani mtulinga ni mtu mnene. Si lugha rasmi, kuendeleza hilo neno ni kuwadhalilisha wale wenye maumbo ya namna hiyo.

Ninaamini utani ni sahihi, lakini kuna haja ya kuangalia wakati mwingine mnataniaje na utani unahusu nini. Wako wamehoji Simba wameitwa wa matopeni na kadhalika. Lakini si jambo linalohusisha watu wa aina fulani. Sasa si sahihi kuendelea kuwadhalilisha wengine kwa kufurahisha wengine.

Ziko njia sahihi za utani na njia za kupita na itakuwa vizuri Manara na Dismas Ten kuhusika kuwa watetezi wa heshima za mashabiki wa klabu hizi mbili. Badala ya wao, kuwa ndiyo wanaoongoza kwa maneno makali yanayowagusa wengine.

Tuwaheshimu dada na mama zetu hata kama tunaamini utani ni jambo la kawaida kwa Yanga na Simba. Maana tayari wako wa Yanga nao wameanza kusambaza picha za watu wanene wa Simba. Hii si sahihi na mtavuka mipaka ya haki za uanadamu. Acheni.


6 COMMENTS:

  1. Tatizo yuko msemaji mmoja hawezi kuisemea timu yake akaamini ameeleweka bila kuitaja timu nyingine kwa ubaya.
    Na anaongoza kwa kugombana na kila anayemsahihisha kwa uropokaji wake.
    Huku akijitetea nimetumwa na klabu.

    Mhh klabu gani? Nashauri apewe maandishi asome neno kwa neno.

    ReplyDelete
  2. Kama kuna vijana wasioijua historia ya utani kati ya Yanga na Simba labda huyo Dismas Ten si kwa Manara? Khaji Manara ni zao la historia halisi kati ya utani wa Yanga na Simba. Tunapouzungumzia ukoo wa Manara basi huwezi kuacha kuizungumzia Yanga. Sasa Manara kuja kuwa shabiki wa kujirusha gorofani wa Simba kwa kweli ni jambo la utani miongoni mwa watanzania wanaoijua historia halisi ya hizi timu mbili. Msemaji wa Yanga alilichukulia lile suala serious kwani karuka kutoka kwenye picha za watu na kwenda kumvamia Manara personal. Kwa kweli Dismass alifanya makosa. Manara utani wake ulilenga kwa klabu zaidi kuliko mtu binafsi lakini la kushangaza utaona Dismass amekwenda kumzungumzia Khaji Manara binafsi sio klabu yake.Dismass inabidi aache kazi ya usemaji wa klabu na kuwa msemaji wa wakina dada kwani inaonekana haelewi majukumu yake ya kazi. Nnaimani kama Manara alikosea katika kukoment kwenye ile picha na kupelekea kufikia kiwango cha uzalilishaji wakina mama zetu basi wenye kazi zao wa kukemea maudhi hayo wapo Tanzania wangemrudi Manara na sio Dismass Ten.

    ReplyDelete
  3. Dada yako akiitwa mtulinga kwa sababu tu ni mnene utaona saws!? Ikiwa Jerry alimuita Manara zeruzeru na akaonekana ametukana, leo kwanini Manara asiadhibiwe kwa kutukana!? Ni lazima kujua tofauti kati ya utani na matusi. Manara anadhani kutukana wengine ndio usemaji, jambo balo sio sahihi. Utani hata katika makabila upo lakini sio matusi ya kudhalilisha wenzio. Tatizo Manara amekuwa haadhibiwi kutokana na mapungufu aliyonayo ambayo yamemfanya watu wamchukulie ni kilema na akiguswa tu kelele zake zinawafanya watu wamuonee huruma.Dismass anachofanya ni kumkumbusha alikotoka, whether aliyekusanya pesa ni Muro au Dismass ila pesa zilichangwa na wanayanga ikiwemo akina dada hao anaowaita mitulinga. Ni wakati sasa,Manara aonywe na kama akiachwa kukawa na retaliation inaweza kuleta matatizo.

    ReplyDelete
  4. Wakati mwingine muwe mnaacha hisia, jaziba, kelele, maeneo mengi, mihemko mtumie akili. Naanza na maana ya utani (bahati nzuri mimi ni mtaalamu wa lugha - isimu na fasihi)Maana ya utani, kwa mujibu wa Kamusi Kuu ya Kiswahili ni: a.utaratibu wa kimila ambao unaruhussu jamii fulani kuelezena au kutendea mambo yoyote bili kukasirikiana, b.maneno ya mzaha, kisawe chake ni dhihaka. Kwa hiyo mtu mwenye akili timamu na anayeitumia akili yake kufikiri pasi kuweka hisia, hawezi kuliita jambo utani halafu akaliwekea mipaka ukizingatia mana halisi ya neno utani. Hilo ni neno rasmi na tena limeelezwa kwenye kamusi ya BAKITA (2015/2017) wataalamu wa lugha na wenye mamlaka ya kukilinda kiswahili. Hivo, hakuna kosa wala suala lolote alilofanya Manara ambalo ni baya kwenye muktadha wa utani ila hisia na mihemko, ukosefu wa ufikiri na kujua jambo limezungumzwa katika muktadha upi (isimu amali inapaswa itumike kuwaelewesha watu pamoja na fasihi). Pili, mtoa mada katoa maana ya neno 'mtulinga' kwa kurejea kamusi ya Visawe pasi kurejelea vyanzo vingine vyenye mamlaka kama hayo halafu katuotosha etineno 'mtulinga' mtaani hutumika kumaanisha mtu mnene na si lugha rasmi. Hivyo si vema kulitumia kumrejelea mtu mwingine. Swali nalomuuliza ni kwamba lugha huwaje rasmi? Watunga kamusi, pamoja na mambo mengine, huyaingiza maneno katika kamusi kutokana na jinsi yanavyotumiwa mitaani na jinsi yalivyoshika kazi kimatumizi na huya maana ileile. hivyo,hiyo si hoja ya msingi (bali katumia hisia). Zaidi ni kwamba neno mtulinga ni rasmi na linatumika kwa maana zote mbili alizotaja mtoa post. Kamusi Kuu ya Kiswahili inaeleza yafuatayo kuhusu neno 'Mtulinga'; mfupa wa begani mbele ya kifua cha mtu. Hutumika kama msemo kama (mtulinga wa mtu = mtu mwenye nguvu, kifua kipana) Kwa hiyo, kumuita mtu mene kuwa ni mtulinga au mtu mwenye nguvu, kifua kipana si tusi ni neno la Kiswahili lenye matumizi rasmi na sahihi yanayotambulika na mamlaka inayosimamia lugha. Hakuna kosa kwa Manara sema ujinga wa kutojua utani ndio unaowasumbua wengine, mbona wao wasemapo 'ninyi ni mikia' huwa hawajui kuwa wanawaambia watu kama wao? Ukishindwa kuelewa maana ya utani au kama huwezi kuhimiri utani ni bora useme wewe si mtani na mtu yoyote kuliko kumchagulia mtu utani. Hata ukienda mahakamani, mtu akisema mimi na huyu tu watani na nilisema kwa utani hakuna kesi. Wasiojua historia ya utani wa timu hizi ndio wanaotokwa na mapovu!!!!!

    ReplyDelete
  5. Tangu lini neno unene likawa tusi katika kamusi ya kiswahili?

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic