April 4, 2018

KIKOSI CHA MTIBWA SUGAR MSIMU ULIOPITA


Klabu ya Mtibwa Sugar imeamua kufunguka na kuzungumzia kuhusiana na adhabu yao waliyotandikwa na Shirikisho la Soka la Afrika (Caf).

Kumekuwa na hofu miongoni mwa wadau kwamba Mtibwa Sugar, bado wanatumikia adhabu hiyo.

Mwaka 2003, Mtibwa Sugar ilifungiwa na CAF kutoshiriki michuano yoyote inayosimamiwa na shirikisho hilo kutokana na kushindwa kwenda kucheza dhidi ya Santos FC ya Afrika Kusini katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika kutokana na kile kilichodaiwa kuwa uongozi wa klabu hiyo ulikosa fedha za nauli za kuisafirisha timu hiyo kwenda nchini humo.

Hiyo ilikuwa ni baada ya mchezo wa kwanza uliozikutanisha timu hizo hapa nchini na Mtibwa Sugar kukubali kipigo cha mabao 3-0.

Ofisa Habari wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru alisema kuwa adhabu yao hiyo ilishaisha siku nyingi na amewataka wale wote wanaowapotosha mashabiki wao kuacha mara moja kufanya hivyo.

“Adhabu hiyo ilishaisha siku nyingi, kwani tulifungiwa miaka mitatu kutoshiriki michuano ya CAF, kutokana na kosa hilo la kutoenda Afrika Kusini kucheza na Santos, kwa hiyo wanasema bado tumefungiwa tunaomba waache mara moja kuwadanganya mashabiki wetu.

“Tangu kipindi hicho mpaka sasa ni karibia miaka 15 kwa hiyo ni wazi kuwa adhabu yetu ilishaisha na sasa tunajiandaa kuhakikisha mwaka huu tunakuwa mabingwa wa Kombe la FA ili tuweze kuiwakilisha Tanzania katika michuano Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya nne,” alisema Kifaru.

Mara ya kwanza kwa Mtibwa Sugar kushiriki michuano hiyo ilikuwa mwaka, 2001, kisha ikashiriki 2002 na mara ya mwisho ilikuwa ni 2003, katika miaka hiyo yote ilikuwa ikishia hatua ya pili ya michuano hiyo.




2 COMMENTS:

  1. mwambi kifaru adhabu itahesabaika pindi timu husika itapopata nafasi ya kushiriki mashindano ya CAF.. toka hiyo 2003 wamepata nafasi mara ngapi kushiriki mashindano ya CAF?

    ReplyDelete
  2. Ila kama hawajashiriki tujiulize adhabu inafutwa au inabaki palepale?

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic