Mechi ya kibabe! Si Simba wala Yanga kila upande umetamba kushinda mechi yao ya leo Jumapili ya Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakisema; “Hawa wetu kabisa”.
Timu hizo zote zinawania ubingwa wa ligi kuu ambapo makocha wake wametamba kushinda mechi hiyo ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kubeba taji hilo.
Mechi hiyo inatarajiwa kujaa upinzani mkubwa kutokana na ushindani uliopo zinapokutana timu hizo huku mechi iliyopita ya ligi hiyo, Oktoba mwaka jana zikitoka sare ya bao 1-1.
Katika mechi hiyo, Yanga wataingia uwanjani ikiwa na kocha mpya, Zahera Mwinyi raia wa Ufaransa mwenye asili ya DR Congo pia Simba itakuwa na Kocha Pierre Lechantre raia wa kuzaliwa wa Ufaransa.
Zahera alisema ameshiriki kwa asilimia ndogo katika maandalizi yake huku kazi kubwa ikifanywa na makocha aliowakuta Mzambia, Noel Mwandila na Shadrack Nsajigwa, lakini wamepanga kushinda.
Zahera alisema, kwa siku chache alizokaa na timu hiyo kuifundisha ameridhishwa na kiwango cha kila mchezaji hali inayompa matumaini makubwa ya kupata ushindi dhidi ya Simba.
“Kwa kikosi hiki nilichokikuta na kufanya nacho kazi kwa siku hizi mbili kambini (Morogoro), nimefurahishwa nacho nimekuta wachezaji wote wakiwa na fitinesi na pumzi za kutosha kitu ambacho ni muhimu ili mchezaji acheze mpira.
“Mimi kwa siku hizi chache nilizofanya mazoezi na timu nimeongezea baadhi ya vitu vichache ikiwemo mbinu za jinsi ya kulinda lango letu timu ikiwa haina mpira na kushambulia pale timu inapokuwa na mpira.
“Kingine nimeongeza hamasa kwa wachezaji wangu tukiwa kambini, kwani nilifanya kikao nao na kikubwa nimewajenga kisaikolojia ili waione mechi ya Simba ni ya kawaida kama zilivyokuwa nyingine, hivyo naamini tutashinda mechi hii,” alisema Zahera.
Kwa upande wa Kocha wa Simba, Lechantre ambaye alihamishia kambi ya timu yake jijini Dar es Salaam juzi Alhamisi, alisema tayari amekamilisha maandalizi ya kikosi chake na kipo fiti kwa ajili ya pambano hilo na kikubwa anahitaji ushindi ili aiongoze Yanga kwa pointi nyingi.
“Kila siku nawakumbusha wachezaji wangu vitu muhimu na kikubwa ni kutodharau timu tunayokutana nayo katika ligi ili tushinde.
“Nataka timu yangu ishinde kila mechi iliyo mbele yetu ikiwemo hii dhidi ya Yanga.
“Yanga ninaifahamu vizuri kwani niliwaona kwenye mechi kadhaa kupitia runinga, pia niliwaona uwanjani wakicheza dhidi ya Singida United, wana baadhi ya wachezaji hatari.
“Ambaye sijamuona ni kiungo wao mwenye rasta anayevaa jezi namba 13 (Thabani Kamusoko), nimeambiwa ni hatari, lakini hii si sababu ya kupoteza mechi hii,” alisema Lechantre.
Jana Ijumaa jioni Simba ilifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Boko Veterani uliopo Boko nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam huku Yanga ikirejea Dar es Salaam, jana jioni kutoka kambini Morogoro.
Kutoka Championi
0 COMMENTS:
Post a Comment