April 28, 2018






NA SALEH ALLY
MECHI ya kesho itakuwa na mambo mengi sana na kama ilivyo kawaida, itaacha gumzo la muda mrefu watu wakijaribu kuzungumzia kilichotokea.

Simba na Yanga wanakutana katika mechi yao ya pili ya Ligi Kuu Bara kufunga msimu dhidi yao. Kila mmoja anataka kushinda kwa ajili ya mbio za ubingwa lakini heshima pia.

Asili ya mechi za watani zina tofauti kubwa na mechi nyingine hasa kuhusiana na gumzo. Mwanzoni huwa na gumzo na majigambo ya kila aina, kila upande ukiamini utafanya vizuri na kuwatoa shoo wenzao.

Baada ya mchezo huo, majigambo huwa hayaishi siku moja. Inaweza kuwa ni kuhusiana na aliyeshinda kutamba sana au kama ni sare kila mmoja humueleza mwenzake alikosea wapi na kadhalika.

Kawaida mechi hiyo haiwezi kwisha bila gumzo la muda mrefu, liwe na sifa nyingi au lawama. Liwe na majigambo au kusikitisha.

Mechi hiyo mara nyingi sana imekuwa ikiwaibua wachezaji ambao huonekana kwamba hawana faida sana au walikuwa wamesahaulika.

Wakati mwingine huwapoteza wachezaji ambao wanakuwa wanategemewa na kuonekana wanafaa, lakini siku ya mechi hiyo aidha kwa makosa au mchezo kuwakataa, hubaki gumzo lakini upande wa kuonekana walikwamisha jambo siku hiyo.




Wachezaji wengi waliokuwa wakiaminiwa, walianza kuonekana hawafai katika mechi hiyo ya watani au walionekana hawana mvuto au hawaaminiki sana, walirejea.

Wachezaji wa kila upande yaani Yanga na Simba wanalijua hilo. Ndiyo maana pamoja na hofu, wengi hujitahidi kucheza kwa juhudi kubwa ili kufanya vizuri katika mechi hiyo.

Kwa upande wa Yanga na Simba pia kuna wachezaji ambao walikuwa wanacheza lakini sasa hawana nafasi, wako ambao wameanza kucheza lakini hawajaaminika sana na wale waliokuwa wameanza kucheza lakini sasa hawana nafasi ya uhakika, wanaweza wakaamka kesho.

Wachezaji hao wana nafasi ya kuamka na kutengeneza upya hali ya kujiamini kama tu watafanya vizuri katika mchezo huo na nafasi ya kufanya hivyo.

Mchezo huo ni wa kawaida kabisa kama mechi nyingine hasa kwa wanaocheza, lakini “mtengenezo” wa hofu kutokana na historia na rekodi, unaufanya kuwa na hofu kubwa kwa wachezaji, makocha, viongozi na hata mashabiki wenyewe.

Katika mchezo wa kesho kuna wachezaji ambao watakuwa na nafasi ya kutengeneza imani kubwa kwa mashabiki kama watapata nafasi.

Kupata nafasi pekee pia inaweza isitoshe lakini kama watatulia na kuona mchezo huo ni nafasi kwao ya kuaminika kwa mara ya kwanza, au kurudisha imani kama awali walikuwa wakiaminika na baadaye kupoteza imani hiyo kwa benchi la ufundi na hata mashabiki wao.

Mavugo:
Amekuwa sawa na roli la mkaa, “tripu shamba, tripu gereji.” Kidogo mechi dhidi ya Lipuli FC, akaiokoa Simba kupoteza pointi zote tatu kwa kufunga bao la kusawazisha.

Kama atapewa nafasi ya kucheza, akatulia na kuacha uoga wake na kutokuwa mtulivu, basi ana nafasi kubwa sana ya kuwapa wakati mgumu Yanga na kuamsha upya ‘nyota’ ya jina lake.

Mavugo ana uwezo lakini si mchezaji anayependa kujituma au kulazimisha mambo yanapokuwa magumu.

Mhilu:
Yusuf Mhilu ni kinda na tayari ameanza kuaminika, lazima atakuwa anataka kuonekana katika mechi hiyo ili kuongeza imani kwake.

Kwa mfumo wa Simba kutaka kupanda na kushambulia kutumia mabeki, Mhilu ana kasi na anaweza kuwa chanzo cha kuanzisha mabao au kufunga mwenyewe.

Silaha nyingine nzuri ya Mhilu ni uwezo wake wa kupiga mipira ya mwisho ya krosi na mabeki wa Simba wajipange.

Mzamiru:
Kama amesahaulika hivi, lakini nafasi ya kuikoa Simba kwa kung’ara na kutoa pasi za mabao au kufunga mwenyewe, inawezekana kabisa.

Hata hivyo, kwa kumuangalia Mzamiru anaonekana ni kama ameshakata tamaa.

Akitulia, akaamini na kujipa moyo, basi kama atapata nafasi, mechi ya kesho iwe ya kurejea tena.

Mwashiuya:
Geofrey Mwashiuya alianza msimu vizuri sana, lakini katikati amekwenda anapotea. Hata hivyo, kasi yake, krosi zake ‘dongo’ Yanga inazihitaji na zinaweza kuwa maumivu kwa Simba.

Kama Yanga itataka kucheza kwa kasi hasa mwanzoni, basi imtumie na atawasaidia na itakuwa nafasi yake ya kurejea na kurudisha imani lakini kama tu ataamua kutulia na kuamini mechi hiyo ni saizi yake.

Ndemla:
Bado Kocha Pierre Lechantre hamuamini sana kuanza, lakini Said Ndemla anastahili kucheza mechi hiyo hata kwa dakika 30 na Simba watayaona matunda.

Akiwa timamu katika mwendo wake, Ndemla ni mchezaji anayebabaisha sana kwa mlinzi au yeyote anayemkaba. Maana hajulikani anatoa pasi ndefu au fupi au anapiga shuti.

Bahati nzuri ana nguvu ya kupiga lakini ana uwezo wa kulenga. Hivyo hata kama kipa akiokoa, bado atakuwa ametengeneza hatari.

Ajibu:
Kama Ibrahim Ajibu Migomba amepotea hivi, tayari yameanza maneno dhidi yake kwamba hivi na vile. Kwa maana ya uwezo wa kazi ana uwezo mkubwa sana.

Mechi ya kesho inaweza kuwa yake akipata nafasi naye akaamua “kumaliza kazi”. Angalia akipewa mipira ya faulo, angalia akiwa nje ya 18 anavyokuwa haeleweki ni pasi au anapiga moja kwa moja.

Kazimoto:
Mwinyi Kazimoto ni ng’ombe ambaye hajazeeka maini, ana uwezo wa kumiliki mpira vizuri, kupiga pasi za uhakika, pasi za mwisho na mashuti chanya.

Kama atapewa nafasi, kwake mechi hii ni nyanya na ana uwezo wa kufanya vizuri na mambo yakaenda vizuri. Akipewa nafasi, ana nafasi kubwa ya kung’ara.

Kessy:
Hassan Kessy kafanya vizuri katika mechi nyingi zilizopita, amekuwa chanzo cha mabao na mahiri katika ulinzi. Anaweza kung’ara ingawa atatakiwa kubadili aina ya uchezaji maana atakuwa na Emmanuel Okwi.

Akiwa Mtibwa Sugar, kisa cha Simba kumsajili ni baada ya kumdhibiti Okwi pale Jamhuri Morogoro. Okwi amebadilika na Kessy amepevuka zaidi, hivyo ana nafasi ya kutamba.

Wako, wengine wanaoweza kung’ara pia kama James Kotei, Paul Bukaba, Mohammed Zimbwe kwa upande wa Simba, Yanga kuna Juma Mahadhi bado ana nafasi kama ilivyo kwa Makka Edward au Ramadhani Kabwili.

Kikubwa atakayepata nafasi lazima ajue umuhimu wa siku yenyewe. Atakayeteleza, basi atakuwa kajiondoa katika reli na kuingia katika gumzo hasi.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic