April 2, 2018




NA SALEH ALLY
KUMEKUWA na kasumba hii ya wachezaji wa klabu mbalimbali kutoonyesha kuwa wanajali sana kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars.

Hii inatokana na yale mazoea kwa hapa nyumbani au kwa kuwa tunasikia tu au kimwonekano kwamba klabu hasa Yanga na Simba ni kubwa na maarufu kuliko timu ya taifa.

Hili pia limejaa kwenye vichwa vya mashabiki wengi wa soka. Hivyo kuwafanya baadhi ya wachezaji kuamini kwamba wanaweza kufanya vizuri zaidi au kujituma zaidi wakiwa na klabu na si timu ya taifa.

Hakika hili ni jambo ba ya sana na linapaswa kukemewa kwa kiasi kikubwa kwa kasi ya juu. Lazima kubadilika kimawazo kwa mengi tu.

Kwanza suala la uzalendo kwa nchi, sisi ni Watanzania na unapopata nafasi yoyote ya kuliwakilisha taifa lako, si jambo dogo hata kidogo.

Pili heshima, kuliwakilisha taifa lako ni heshima kwa kuwa unaingia kwenye rekodi ya mashujaa ya taifa kwani unakuwa umelipigania taifa lako na bendera yako.

Tatu ni soko, mchezaji anajiuza kwa kuwa unapozungumzia mauzo ya wachezaji kutoka klabu za Tanzania kwenda zile za nje, wenzetu huangalia zaidi kwenye kikosi cha timu ya taifa, mchezaji husika amefanya kipi kikubwa au ameichezea timu ya taifa mechi ngapi.

Wacheaji wa Ulaya wamekuwa wakililia au kupigana kupata nafasi za kuzichezea timu zao za taifa. Angalia wachezaji kama Wilfred Zaha wamekimbia England na kurejea Ivory Coast ili wapate nafasi ya kucheza kwenye timu ya taifa. Alex Iwobi pia, aliona bora Nigeria atapata nafasi kuliko England.
Hivyo kucheza katika timu ya taifa, ni jambo kubwa la heshima na linatangaza na kuongeza soko la mchezaji husika na tumeona mfano mdogo hivi karibuni.

Tanzania ilicheza mechi ya kirafiki na timu ngumu ya DR Congo ikiwa ni sehemu ya kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) ya mechi za kirafiki.

Tanzania au Taifa Stars ilishinda kwa mabao 2-0 na kuwashangaza wengi baada ya kuwa imetoka kupokea kipigo cha mabao 4-1 kutoka kwa wenyeji wake Algeria katika mechi nyingine ya kirafiki hapo kabla.

Baada ya mechi hiyo, baadhi ya watu wa TP Mazembe walianza kuulizia kuhusiana na kiungo wa Simba, Shiza Kichuya kwa kuwa alionyesha kiwango cha juu katika mchezo huo.

Uhakika watu kutoka TP Mazembe wamekuwa wakitaka kujua kama inawezekana kumpata Kichuya ambaye siku hiyo alilingana na Mbwana Samatta aliyewahi kuwa shujaa wa TP Mazembe na hatasahaulika katika rekodi za timu hiyo.

Kichuya alitoa pasi kwa Samatta ambaye alifunga bao la kwanza na Samatta akatoa pasi kwa Kichuya, akafunga bao safi la pili akiwa katika sehemu ambayo haikutarajiwa angeweza kufunga.

Kama siku Kichuya atafanikiwa kwenda Mazembe, maana yake Mazembe watakuwa waliomuona katika kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ambayo huenda wengi mliiona haina faida au msaada au ya kawaida sana.

Wanaona katika kiwango cha timu za taifa, akikutana na DR Congo yenye rundo la wachezaji kutoka Ulaya akiwemo mshambuliaji wa Everton, Yannick Bolasie ambaye inawezekana pia alifurahia bao la Kichuya, haliwezi kuwa jambo dogo hata kidogo.

Kitu kingine kizuri, siku hizi huduma za timu ya taifa zimebadilika na kuwa rafiki kwa wachezaji kwa kuwa kuna wadhamini na TFF wanafuata utaratibu sahihi wa kuhakikisha wachezaji wanacheza katika mazingira rafiki.

Ninaamini ni raha kulitumikia taifa lako huku ukiamini kuna faida ya kufanikiwa zaidi kimaisha. Basi tujifunze.





3 COMMENTS:

  1. Hoja yako ya 3 si sahihi sana. Isitoshe, wanhemuona wapi Kichuya wakati TP Mazembe hawajacheza na timu anayoichezea Kichuya kama si Timu ya taifa? Msuva, Samatta, na hata wachezaji wngi wa Ulaya walionunuliwa na vilabu vyao walinunuliwa kwa sababu walionekana timu ya Taifa??? Professional Player huwezi kuridhika naye kuwa ana kiwango cha hali ya juu kwa kuangalia mechi moja au mbili za timu ya taifa ni lazima uwe umemfuatilia hata kabla au baada ya mechi ya kwanza kumuona. Hivyo, Mazembe watakuwa walimfuatilia Kichuya kabla ya kuwa timu ya Taifa.

    Jambo la uzalendo huwa lina sababu. Jiulize kwanini wakati wa Maximo wachezaji wa Taifa Stars walionekana wanacheza kwa kujituma, wana uzalendo kuliko kwa sasa? Kwa sababu walikuwa wanapewa heshima wanayostahili, malipo yalikuwa mazuri, heshima ya kile wanachokifanya kinataminiwa tofauti na sasa. Uzalendo usiokunufaisha hauwezi kukufanya ukajihisi thamni kulitetea taifa lako. Mfano, mzazi hupendwa na kuheshimika sana na watoto wake kadri anavyowaonesha upendo na kuwajali kama wanawe. Mfano, mwingie ni Nigeria, ambapo chama cha soka cha nchi hiyo kiliwahi kuwadhulumu wachezaji posho zao, kilichotokea ni baadhi ya wachezaji kususia kuchezea timu ya taifa na wale waliocheza hawakucheza kwa moyo mkunyufu na watu walisema moja ya sababu ya timu hiyo kutokufanya vizuri ni migogoro ndani ya chama. Tunaona wachezaji wengi wa sok la kulipwa hawataki kujituma na kujumuza au kujisumbua sana katika timu za taifa ili warudi katika vilabu vyao wakiwa hawana majeraha ili wazitumikie timu zao. Ni kwanini? Kwa sababu wanapajali pale panapowaletea masilahi mazuri, kuliko uzalendo unaokuumiza. Inabidi wachezaji wetu wawapo timu yataifa, wajaliwe, waheshimiwe ili tulawaumu kwa kutojituma

    ReplyDelete
  2. Kapombe aliumia Mwanza.Kuna aliyemjali?Hata kumjulia hali?Alitibiwa na kulipwa na Simba.Hatupingi timu ya taifa lakini msiwasifie wakiwa fit tu.Wakiumia kwenye timu ya taifa wathaminiwe pia.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Ujumbe umemfikia....kuna wachezaji wengi waliumia wakitumikia Taifa lkn TFF wanakuwa hawana habari...una lingine ndugu Saleh?

      Delete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic