April 30, 2018



NA SALEH ALLY
HATIMAYE Simba na Yanga wamevuka katika ile siku ambayo walikuwa wanaisubiri kwa hamu kila mmoja akiwa na majigambo yake, lakini mwisho ukweli wa kila kitu umekuwa wazi.


Mechi imeisha kwa Simba kushinda kwa bao 1-0 dhidi ya watani wake Yanga, bao lililofungwa na Erasto Nyoni katika kipindi cha kwanza cha mchezo huo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, jana.


Kwa mashabiki wa Simba lazima watakuwa ni watu wenye furaha kubwa kutokana na kujipatia pointi tatu ambazo zimewasogeza katika ubingwa wa Ligi Kuu Bara ambao wamekuwa wakiulilia kwa zaidi ya miaka minne sasa bila ya mafanikio.


Yanga watajilaumu kwa kuwa angalau wangepata hata sare kwa kuwa wanajua, timu yao pamoja na kuandamwa na matatizo rundo lakini wamekuwa wakiendelea kupambana na sasa ndiyo wawakilishi pekee wa Tanzania katika michuano ya kimataifa.


Yanga hawakuwa na matumaini makubwa kama Simba, lakini walitamani kushinda, walitaka kufanya vizuri na walijua wangeweza kujaribu. Mwisho wameshindwa kupata kile ambacho walitaka na Simba walistahili kushinda kutokana na walivyocheza.


Pamoja na Simba kufanikiwa kupata pointi tatu kwa ushindi huo wa bao 1-0, bado nitakuwa tofauti na wengi wanaoamini mchezo huo ulikuwa mzuri na ulikuwa unavutia kuangalia.


Ulikuwa ni mchezo ulioanza taratibu sana, kila upande ulionekana kuwa na hofu na upande mwingine. Angalau ingekuwa dakika tano hadi saba za mwanzo. Lakini kwa dakika 20 zote, hakuna timu iliyosogea kukaba katika ‘zone’ ya mwenzake.


Hii iliifanya mechi hiyo kuwa na taswira na mpira wa kutaka kubahatishana, ulikuwa mpira wa kuviziana na kwa kiasi kikubwa ulipoteza ile hali ya kuwa ni mchezo wa watani ambao unazikutanisha timu mbili kubwa zinazobeba historia ya soka ya Tanzania.


Ukiangalia kila kikosi kilikuwa na wageni, utaona kutoka Ghana, Uganda, DR Congo, Cameroon na kadhalika, lakini timu zilicheza mpira utafikiri mechi ya kirafiki, mipango ya makocha ilikuwa utafikiri kombe la mbuzi na zaidi ni kupata pointi tatu hata kwa mpira ilimradi. Haukuwa mchezo wa kufurahisha.


Maandalizi yalikuwa makubwa, ya muda mrefu, yenye kelele nyingi na hata wachezaji kupewa ulinzi mkubwa. Mwisho unaona hakika mashabiki waliofika uwanjani au waliokaa katika runinga hawakustahili kulipwa tulichokiona jana.


Simba inaweza kucheza vizuri zaidi ikicheza dhidi ya Singida United au Njombe Mji, Yanga inaweza kutulia na kucheza kwa uhakika ikikutana na Ndanda FC au Kagera Sugar au Stand United?


Kama ulikuwa ni mfumo wa makocha, vipi hata wachezaji wanaoonekana ni wakongwe na wenye uwezo walishindwa kuonyesha soka la uhakika zaidi kuishia kutemeana mate, kutukanana na kufanya vurugu badala ya mchezo mzuri wa soka mashabiki waliotaka kuuona.


Kila mmoja anaweza kusema anavyoamini, lakini uhalisia Simba na Yanga hawakuwatendea haki mashabiki wa soka nchini kwa kuonyesha kiwango ambacho mimi naona hakifanani na mechi yenyewe kama ambavyo inajulikana.


Kawaida viingilio huwa vinakuwa vikubwa, basi soka liwe la juu. Maandalizi ya kutosha na mazito, basi mchezo ungekuwa na soka zito na la uhakika.


Mashabiki huandaliwa kwa muda mwingi kwa kuwa watani wanakutana. Tunakubaliana pamoja na vyote lazima kuwe na soka safi la viwango sahihi.


Sitaki kuwakatisha tamaa wachezaji, sitaki kuwakatisha tamaa viongozi na makocha lakini nataka kuwakumbusha wachezaji kwamba lazima waonyeshe zaidi ya kile walichoonyesha jana kwa kuwa wanaokuwa pale uwanjani ni watu wanaotaka kuona kile cha ziada tofauti na siku nyingine.



Thamani ya kila kitu hujengwa na uhalisia, kama itaendelea hivi, baada ya mchezo mwingine na mwingine, mwisho itafikia mtakosa mashabiki uwanjani na kuwarudisha itakuwa shida.

6 COMMENTS:

  1. Eeeeh bwna mchezo ulichezwa kweli kulinganisha na mechi yenyewe huwa kuna dakika 15 hadi ishirini za kusomana mchezo maana timu moja ikifika tu na kumfunga mwenzie huu siyo mchezo mkubwa kwangu mimi shabiki mpira ulistahili kuwa hivyo kabisa kulingana na mechi yenyewe mfano. tazama mechi kati ya Man united Vs Man city au Barcelona Vs real madrid utakuta mchezo huwa ni hivyo hivyo sasa mechi iko vizuri sasa japo kuwa mechi ya clasico huwa lazima na vituko kama hivyo vya kutemeana mate hii utokea kwa upande unaozidiwa kimchezo wachezaji huanza kufanya hivyo wakiamini watawapunguza wenzao kasi ya mchezo. Jana mpira umechezwa sana na simba na wange weza hata kupata zaidi ya goli tano.yanga kufika ndani ya 18 ya simba walifika mara 4 tu ndaini ya dakika 90 kuna wachezaji wa simba walibeba timu kwa namna moja au nyingine hawa ni JONAS MKUDE engeener wa mchezo, KAPOMBE aliyemficha SHISHIMBI, ERASTO NYONI aliyemtunza CHIRWA pamoja na MLIPILI. Kwa upande wa yanga VICENTE DANTE alimficha BOCCO.

    ReplyDelete
  2. Na mimi nakuwa tofauti sana na wewe Saleh kwa kuwa sio kila unachokiandika watu wakiamini kuwa ndicho sawa. Mechi ya Simba na yanga siku zote huwa ni FAINALI na maechi ya fainali siku zote huwa ni mechi ya matokeo na sio mechi ya kuonesha manjonjo.

    ReplyDelete
  3. Pengine angeshinda Yanga japo kwa bao la mkono kama lile la Amis Tambwe ndio ingependeza zaidi na mpira ungekuwa umechezwa?

    ReplyDelete
  4. Huo ni ukweli ila ukweli mwingine ni kwamba hii mechi ilikuwa ni ya pointi tatu kuliko burudani.

    ReplyDelete
  5. Kusema ivyo imekosea kiongozi. Mchrzo migumu na mikubwa lazima timu zisomane kwanza ukikurupuka umeumia. Na hapo kumbuka tu upinzani wa jadi. Cha kulaumu ni kwanini simba hakulazimisha kushinda goli nyingi kwa yanga iliyokuwa inapiga mipira mirefu isiyo na malengo. Yanga kwa ujumla hawakuwa na lengo la kushindana mana mipango ya kushambulia haikuwepo. Somba ndo alokuwa anashambulia na kupiga krosi nyingi za kutafuta goli.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic