Huku wakiwa wanahitaji kufanikiwa kuibuka na ushindi katika mchezo wao dhidi ya Wolayta Dicha ya Ethiopia, benchi la ufundi la Yanga limewaweka kitimoto wachezaji wao kuhakikisha wanafanikiwa kupata ushindi katika mchezo huo kwa kusahau yaliyopita.
Yanga itaikaribisha Wolayta Dicha kesho Jumamosi katika Uwanja wa Taifa jijini Dar kucheza mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kutolewa katika mechi ya Ligi ya Mabingwa.
Meneja wa Yanga, Hafidhi Saleh, alisema kuwa benchi la ufundi limezungumza na wachezaji hao kuhakikisha wanautazama mchezo huo kwa jicho la tatu na kusahau yaliyopita ili kufanikiwa kushinda.
“Benchi la ufundi limekaa na wachezaji kuzungumza nao kuelekea mechi yetu hiyo kwa kujipanga na kufanya vyema kwa kusahau yaliyopita kuhakikisha mtazamo wao wote unakuwa katika mchezo huo ili tufanye vyema.
“Tunaendelea vyema na maandalizi yetu kuelekea mechi hiyo wachezaji wetu wote wapo vizuri kuelekea mchezo huo majeruhi wote wanaendelea vyema na mazoezi,” alisema Hafidhi.
Pamoja na kwamba haifanyi vizuri katika ligi ya nyumbani kwao, Dicha si timu ya mzaha kwa kuwa imefika hatua hiyo kwa kuing'oa Zamalek, moja ya timu vigogo barani Afrika.
0 COMMENTS:
Post a Comment