April 23, 2018





Na Saleh Ally
YANGA imepangwa Kundi D katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa ni moja ya timu za Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati zilizofanikiwa kufika katika hatua hiyo.

Hatua waliyofikia Yanga licha ya kuwa na matatizo lukuki yanayowaandama, ni jambo la kujivunia kwa mashabiki wao lakini Watanzania wote wanaopenda mpira na michezo kwa jumla.

Nilizungumzia kuhusiana na faida za Tanzania kama Yanga itafanikiwa kufuzu hadi hatua ya makundi. Ziko nyingi lakini ni kwa ajili ya mafanikio, changamoto lakini hata kiuchumi.

Yanga wamefanikiwa kufuzu na nilichoeleza mwanzo kitaanza kuonekana hatua hiyo ya makundi itakapoanza.

Lakini kabla ya kuanza kwa hatua hiyo, kinachoshangaza sana ni baada ya kupangwa kwa makundi manne ya michuano hiyo.

Awali, hatua ya makundi ilikuwa ni timu nane na makundi mawili lakini Shirikisho la Soka Afrika (Caf), likaamua kubadilisha na kufanya makundi manne yakiwa na timu nne kila moja, maana yake timu 16.

Yanga ni moja ya timu 16 bora kabisa ambazo zimefikia hatua hiyo ya michuano ya Kombe la Shirikisho. Kumbuka hata kabla ya hapo, iliwahi kufanya hivyo.

Kwa kuwa ndani ya miaka mitano, Yanga inafanikiwa kuingia mara mbili katika hatua hiyo, hivyo itambue kwamba haitakuwa na upinzani mdogo kwa kuwa wapinzani wataichukulia kama timu kubwa na ngumu.

Soka la Afrika limebadilika na sasa lile suala la timu za Kaskazini kutawala katika michuano ya Ligi ya Mabingwa na ile ya Kombe la Shirikisho inakwenda huku inapungua na mfano mzuri ni hatua ya makundi ya safari hii.

Utaona kuna timu nyingi kutoka Afrika Mashariki na Kati kama zinazotokea Tanzania, Sudan, Rwanda na Kenya. Wakati msimu uliopita zilikuwa timu za Sudan na Uganda pekee.

Angalau DR Congo walikuwa na TP Mazembe lakini safari hii wana AS Vita ambayo pia ni timu kubwa. Sudan wameirudisha tena Al Hilal lakini Afrika Mashariki imekuwa na ongezeko la juu.

Yanga isingevuka, bado ingevuka timu ya ukanda huu lakini imekuwa ni vizuri zaidi kwa Afrika Mashariki kwa kuwa Yanga ni sahihi kiasili kwa ukanda huo.

Lakini ukisikia maneno ya wachambuzi wengi au wengi wanaopenda mpira yanaelekea kuipotosha Yanga ianze kuamini kwamba imepangwa kundi mchekea, hii ni sumu.

Yanga imepangwa na timu karibu zote za ukanda wake kasoro USM Alger ya Algeria, nyingine ni Rayon ya Rwanda na Gor Mahia ya Kenya.

Timu mbili za Gor Mahia na Rayon unaweza kusema ni saizi ya Yanga kabisa kwa maana ya mazoezi na ubora ambao unafahamika na nafasi nzuri kwa Yanga kwa kuwa itakuwa inajua inacheza na timu za aina gani.

Yanga itakuwa inaona ina wakati mgumu kwa USM Alger ambayo ni moja ya timu kubwa na ngumu katika suala la michuano ya kimataifa ya Afrika.

Huenda hili limewafanya wengi waanze kuamini Yanga ipo katika kundi laini na inapaswa kupita kwa ulaini kabisa. Binafsi naona hii itakuwa ni sumu kali kabisa kwa Yanga.

Kuanza kuona Rayon na Gor Mahia ni walaini ni kosa kubwa na kujichongea mapema. Itakuwa vizuri sumu hii isiingie katika vichwa vya wachezaji wa Yanga na vizuri wakiamini wako katika mapambano na wakati mgumu kabisa.

Timu hizo atakazokutana nazo, zitakuwa na tahadhari kubwa kwa kuwa nao wanaona ni nafasi ya kusonga mbele zaidi na kupangwa na Yanga pia ni nafasi nzuri kwao. 

Yanga inapaswa kuwachukulia Gor Mahia ni kama Al Ahly na Rayon sawa na TP Mazembe na maandalizi yao yaendane na ukubwa huo.

Kama Gor Mahia na Rayon watafanya maandalizi ya uhakika zaidi kwa kuwa wanaochukulia Yanga kama timu kubwa na hatari kwao, basi hii ni hatari kwa Yanga.

Lazima kuwe na tahadhari na heshima kwa kila timu iliyofikia hatua hiyo bila ya kujali au kuangalia suala la nchi iliyotokea.

USM Alger, kawaida itajiandaa sana kuliko ingekuwa inacheza na timu za nchi zinazojulikana ni maarufu katika michuano hiyo ya Caf.

Hii ni kwa kuwa kama itashindwa kufuzu katika hatua ya baada ya makundi, inajua haitakuwa sahihi na itaonekana imefeli maradufu. 

Lakini kwa Yanga na uzoefu wake, ikiwa na Rayon na Gor Mahia. Kama itashindwa kufuzu pia kutakuwa na maswali mengi. 

Hivyo hili si suala la kulichukulia chinichini au kawaida. Badala yake Yanga lazima iamini kila timu iliyofikia hatua hiyo ni imara na ngumu na itakuwa imepania kusonga zaidi.

Yanga wakumbuke katika michuano hiyo kuna suala la fedha kutokana na nafasi itakayoshika katika kundi, lakini kuna fedha zaidi kama itafuzu katika hatua ya mtoano.

Kama inaona fedha ni jambo muhimu, basi Yanga ijue hata Gor Mahia na Rayon wanazihitaji sana hizo fedha na halitakuwa jambo rahisi na lazima wapambane hasa kufikia hapo.

Kuna kila sababu ya Yanga kujua hatua iliyopiga ni kubwa lakini ugumu umeongezeka na ijue inacheza mpira wa biashara kwa kuwa pamoja na kushinda kwa ajili ya rekodi, kuna suala la mafanikio pia kifedha.

MAKUNDI:
KUNDI A
Asec Mimosa (Ivory Coast)
Raja Casablanca (Morocco)
AS Vita (DR Congo)
Aduana Star (Ghana)

KUNDI B
Rennaisance (Morocco)
El Masry (Misri)
El Hilal (Sudan)
Uniao Desportiva (Msumbiji) 

KUNDI C
Enyimba (Nigeria)
Williamsville (Ivory Coast)
Club Athletic (Congo)
 Djoliba AC de Bamako (Mali)

KUNDI D
Yanga (Tanzania)
USM Alger (Algeria)
Rayon (Rwanda)
Gor Mahia (Kenya)



2 COMMENTS:

  1. Muandishi usiwatishe yanga ili wasije boronga. Wao wanajiamini sana hasa baada ya kupata pesa

    ReplyDelete
  2. Yanga inakikosi kipana mwaka huu wana tuletea kombe jangwani yanga woyee

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic