Benchi la Ufundi la Yanga linaloongozwa na Mzambia, George Lwandamina, limewashitukia wapinzani wao, Wolayta Dicha ya Ethiopia ambapo sasa limeamua kuumaliza mchezo nyumbani kuepuka hujuma wakienda ugenini.
Kesho Jumamosi, Yanga na Wolayta Dicha kutoka Ethiopia, zitapambana kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar ukiwa ni mchezo wa kwanza wa hatua ya mtoano ya Kombe la Shirikisho Afrika kutafuta nafasi ya kufuzu hatua ya makundi ya michuano hiyo.
Yanga ambayo awali ilikuwa ikishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kutupwa kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, ilikuwa ikishindwa kuutumia vizuri uwanja wa nyumbani jambo ambalo kwa sasa hawataki kulirudia ndiyo maana wameamua kuweka mikakati kabambe ya kuumaliza mchezo huo hapa jijini Dar.
Mkakati wa kwanza ni wa kuweka kambi mkoani Morogoro baada ya Lwandamina kuhitaji iwe hivyo kutokana na kugundua kwamba kuiweka timu jijini Dar kujiandaa na mchezo huo si sawa.
Ofisa Habari wa Yanga, Dismas Ten, amesema kambi ya Morogoro ni yenye utulivu ndiyo maana benchi la ufundi limependa kuiweka timu huko.
“Tunatambua kwamba mchezo wetu wa marudiano hautachezwa Addis Ababa bali utachezwa katika Mji wa Hawassa ambapo ni kilomita zaidi ya 100 kutoka katika Jiji la Addis Ababa.
“Kutokana na hali hiyo, tunahitaji kutengeneza mazingira mazuri kwa kushinda mchezo wa hapa nyumbani ili tukienda kwao tuwe na uhakika wa kusonga mbele na siyo kwenda kuanza kutafuta ushindi, kikosi chetu kipo katika hali nzuri kabisa.
“Donald Ngoma na Thabani Kamusoko ni sehemu ya wachezaji wanaofanya mazoezi na wako fiti, kwa hiyo ni jukumu la mwalimu kuona kama atawatumia au la,” alisema Ten.
CHANZO: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment