May 11, 2018







Na Saleh Ally
REJEA katika baadhi ya aya zilizo katika vitabu vya dini, utagundua kwamba sisi wanadamu tumeumbwa na usahaulifu. Kutaka kupata ubora, vizuri kujikumbusha mara kwa mara hasa kwa masuala muhimu na yale yanayoweza kukuepusha na mambo ambayo si sahihi.


Simba haijabeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa zaidi ya misimu minne, kipindi ambacho mashabiki na wanachama wake walikuwa katika wakati mgumu. Msimu wa kwanza hadi wa tatu, walikuwa wakiamini huenda mambo yangekuwa mazuri lakini haikuwa hivyo na miaka ilienda inaongezeka.



Sasa wana matumaini makubwa, huenda ndani ya siku tatu, nne, tano au wiki watatangazwa kuwa mabingwa. Tena wanaona wana nafasi baada ya msimu uliopita kuwa wamemaliza pointi sawa na mabingwa watetezi wa sasa, Yanga lakini tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa, ikawaangusha.


Wakati Simba wakiwa wanasubiri ubingwa, Yanga wanaonekana wakiwa wamekata tamaa utagundua, Wanasimba wamejifunza mengi ambayo hawakuwa wamejifunza kabla ya miaka mitano iliyopita na moja wapo ni kuheshimu juhudi na moyo wa kujitolea wa watu ambao wanapambana kwa mazuri ya klabu yao.


Angalia, kipindi cha mabadiliko kilipowadia, wamekuwa mstari wa mbele kutaka kujua undani wa suala lenyewe, wakakubali kujifunza. Wameendelea kuhoji kwa nia ya kujifunza lakini wanachotaka ni kuona suala linafanyika kwa usahihi na mabadiliko yanakuwa msaada.


Wakati Yanga ikifanya vizuri, wanachama na mashabiki walionekana kujisahau kabisa kama vile timu yao ilikuwa ikifanya vizuri tu na ndiyo kawaida yake. Baada ya kuona mambo yanakwenda vizuri, wakaanza ujeuri na hata kufikia kuwakashifu waliokuwa wakijitolea, kwamba waondoke, wanafaidika na klabu yao.


Mfano mzuri ni mfanyabiashara Yusuf Mehbub Manji, ninaamini si sura ngeni, kila mpenda soka atakuwa anaikumbuka. Manji aliyeanza kuwa msuluhishi, mfadhili na baadaye akaamua kugombea Uenyekiti akisema anataka kurudisha umoja wa Wanayanga baada ya timu hiyo kufungwa mabao 5-0 na watani wao Simba.


Baada ya Manji kuingia madarakani, Simba haikuwahi kuchukua ubingwa tena na si vibaya kusema kuna dalili ya kuchukua baada ya kuwa hayupo ukiwa msimu wa kwanza tu.

Lakini baadhi ya wanachama, wakiwemo wazee kama mzee Ibrahim Akilimani, huenda kwa sasa ndiye mzee maarufu zaidi kuliko wote wa Yanga, walianza kumsakama na ilionekana wazi msigano wao haukuwa wa kuisaidia klabu.


Taarifa zilielezwa kwamba mzee Akilimali alikuwa akiongoza moja ya kamati za ufundi iliyokuwa ikipokea fedha zilizokuwa katika bajeti. Baadaye “Mhindi” kama ambavyo wao humuita akaizuia hiyo, hapo ndipo kikawa chanzo cha mgogoro. Baadaye mzee Akilimali alilikanusha hilo na kusema anapigania maslahi ya klabu yake.


Akasisitiza wako wadhamini waliokuwa tayari kujitokeza, tena akaeleza uwepo wa Sh milioni 600 ambazo zingeisaidia Yanga na kuwatoa hofu wanachama. Tena msisitizo wake ukawa kama yale maneno ya mashabiki na wanachama wengi, kuwa “wanajifaidisha na klabu, yenyewe haipati kitu.”

Hatukuwahi kuzisikia hizo fedha za mzee Akilimali, leo Yanga mishahara inakosa hadi ya miezi mitatu, hakuna aliyeonyesha zilipo Sh milioni 600, hakuna msaada na mzee Akilimali hazungumzii tena mamilioni!


Kama haitoshi, baadhi ya viongozi hasa wale waliochaguliwa katika kamati ya utendaji mpya ya Yanga baada ya uchaguzi. Walianza kulalama, kwamba mwenyekiti wao aliwanyima uhuru, wakazua mgogoro wa chinichini na mwisho wakasisitiza kuna watu wengi waliokuwa tayari kuwekeza lakini Manji aliwazibia.


Sasa Manji hayupo, hatuoni wanaowekeza zaidi ya wadau wachache akiwemo mwanachama mmoja aliyejitolea kuleta kocha na kumlipa baada ya kuondoka kwa George Lwandamina ambaye uvumilivu uliisha.


Viongozi hao wa kamati ya utendaji hadi sasa wapo klabuni hapo, wako kimya, hatuwaoni hao wawekezaji, hawasemi kama kuna fedha zitawekezwa, hawazungumzi mipango thabiti inayoweza kuikoa Yanga katika wakati huu mbaya ambao inaonekana inashindwa kuutetea ubingwa wao wakiwa madarakani na pia inashindwa kuwa imara kushiriki katika michuano ya kimataifa kutokana na kubanwa na ukata.

Wakati wa Manji, viongozi hao walikuwa na maneno rundo, walitaka kuwahakikishia Wanayanga Manji si lolote na wao wanaweza kuweka mambo yakawa mazuri kuliko ilivyo.


Siku zinavyokwenda ugumu unaongezeka, Yanga inazidi kuumiza mioyo ya wanachama na mashabiki wake kwa kasi ya kimondo, vipi yale maneno yalikuwa ni maneno kutekeleza chuki ya mioyo yenu na furaha ya nafsi zenu?



Mna wawekezaji, nyie ni wabunifu, sasa mateso haya ya Yanga yanayoishia kwenye mioyo ya Wanayanga yataisha lini. Kufikia mishahara ya miezi mitatu, maana yake lilikuwa tatizo linalokua taratibu na halikupata ufumbuzi hadi lilipogeuka bomu na kulipuka!

Mnafanya nini, inueni vichwa vyenu muonyeshe mliyoyatoa midomoni wakati huo mambo yakiwa laini kwa kazi nzuri ya Manji, yanaweza kugeuka matendo na mwisho kukawa kuna wokovu.

Unakumbuka wakati wa ile Kampuni ya Yanga Yetu, Manji alitaka kuokodisha timu kwa miaka 10, mzee Akilimali alisema Yanga haikodishwi kwa kuwa si masufuria. Utaona namna jambo makini lilivyokuwa likiingizwa kwenye mipasho badala mjadala unaoweza kuzaa jibu sahihi la kupata mabadiliko.


Miaka hii Yanga inateseka ni ndani ya ile 10 kama Manji angekuwa amekodishwa na angekuwa akilipa mishahara, fedha za usajili, posho, kuiendesha timu kwa maana ya usafiri wa ndani na nje na kadhalika. Hakuwa ametaka kuinunua, mkataba ulionyesha baada ya miaka 10 ingerudi kwa wanachama ambao wakati imekodishwa wangeendelea kuwa wamiliki.


Hata kabla ya kusoma mkataba, au kuhoji kwa hoja za msingi, watu waliishia kutukana na kulifanya jambo hilo ni la mzaha au kufurahisha nafsi zao kama mabao yanavyofungwa uwanjani. Kinachotokea leo, kinaweza kuwa sehemu ya kumbukumbu ya pale mlipojikwaa na kujifunza kuwa makini katika masuala ya msingi.


Hili ni funzo kubwa, hata kwa wewe shabiki au mwanachama uliamini Manji alifaidika tu. Na kama alikuwa na ubaya wake, basi hukuhangaikia uzuri wake na linakuwa jambo sana kujua uzuri, ubora au umuhimu wa mtu anapokuwa hayuko nawe. Maana unakuwa umeishachelewa.


Manji alikatishwa sana tamaa na Wanayanga wenyewe huku klabu nyingine zikitamani angekuwa wa kwao ili wapate huduma aliyokuwa akiitoa Yanga. Wale waliosema tu, leo wameonekana walikuwa ni maneno mengi na hawakuwa na maana hata kidogo.

Jifunzeni kuweka kando maslahi yenu binafsi na ushabiki usio na maana kunapokuwa na mambo makini kwa ajili ya klabu zenu. Wapunguzieni mateso wanachama na mashabiki wenu kwa kuwa viongozi wenye malengo badala ya wale wapenda sifa na mnaoona kuonekana tu mnazungumza ndiyo umakini au kutengeneza umaarufu.

Leo hii ni hukumu yenu na mnapaswa kutubu kwa kubadilisha ugumu uliopo sasa ndani ya Yanga.






4 COMMENTS:

  1. Uko sawa kabisa, ukiondoa Mzee Akilimali, MTU mwingine ambaye alikuwa na maneno ya kumkebehi Manji

    Na kuwaaminisha Yanga kuwa Manji si lolote ni kikwazo pale Yanga ni MKEMI

    Sasa uwanja uko wazi mipango,mikakati na ubunifu unaoenezwa kuwa Yanga wenyewe ni brand kubwa haihitaji MTU.

    Ndo wakati wake KUTHIBITISHA sio kujificha nyuma ya KABATI BOVU.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Hahahhahahhhahah umenifurahisha nyuma ya kapata bovu

      Delete
  2. Umesema kweli tupu. Tena hongera sana. Manji ameondoka na yeye kama binadamu lazima ungefika wakati aondoke tu. Manji alipigwa vita na watu walio ndani ya yanga na wale waliokuwa nje ya yanga. Tena wale waliokuwa nje ya yanga tena wasio wana yanga walifanikiwa kuwashawishi wale walio ndani ya yanga hata kwenda mahakamani kupinga ukodishwaji wa yanga na walipewa msaada ili kuvuruga mpango mzima wa mabadiliko ya maendeleo ndani ya yanga.

    ReplyDelete
  3. Mwaka mmoja tu .Povuu lote hilo?Umedhihirisha upenzi .Simba ilipotangaza itachukua ubingwa bila kufungwa ulikuwa wa kwanza kupinga. Simba ilipitia huko hatukuona makala ndefu. Sababu sio kundoka kwa Manji tu bali udhaifu mkubwa wa kiungozi.Manji alikuwa kila kitu na wewe ulisifia mfumo huo Leo povu za nini?Ulitegemea Manji abakie milele?

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic