May 16, 2018


Na George Mganga

Klabu ya Simba imeeleza machache kuhusiana na Mkutano Mkuu wa dharura utakaofanyika Jumapili ya Mei 20 2018 katika Ukumbi wa Mkutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere uliopo Ocean Road Posta, Jumapili ya wiki hii.

Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Haji Manara, ameeleza kuwa Simba inaenda kufanya mabadiliko ya Katiba yatakayoifanya Simba iendeshwe katika mfumo kwa kisasa zaidi.

Manara ameeleza kuwa Simba ina zaidi ya miaka 82 mpaka sasa lakini imekuwa ikiendeshwa kwa kutegemea ada za wanachama ambazo hazijitoshelezi kuleta manufaa ndani ya klabu.

Ameongeza kuwa licha ya ada za wanachama, Simba imekuwa ikitegemea zaidi mashabiki Uwanjani ili kupata mapato yatakayoweza kuendesha timu kwa ujumla haswa na ulipaji wa fedha za wachezaji au mishahara.

Katika mkutano Mkuu utakaofanyika Jumapili ya wiki hii, Simba inaenda kuzungumzia rasmi muundo wa kisasa wa klabu ili kujiendesha kibiashara zaidi tofauti na kuendelea kutegemea wanachama.

Simba itawapa nafasi wanachama kumiliki hisa zao huku ikiwatengenezea Kampuni yao itakayojulikana kwa jina la Simba Sports Club Company Holding Limited ambayo itakuwa chini ya Baraza la Wadhamini wa klabu.

Vilevile klabu hiyo itaweza kubadilika jina kutoka Simba Sports Club mpaka Simba Sports Club Company Limited kwa lengo la kujiendesha zaidi kibiashara.

Manara amewaomba wanachama kujitokeza kwa wingi katika mkutano huo Jumapili ya wiki hii ili kuweza kuweka historia kubwa ya soka la Tanzania, Afrika Mashariki kwa Ujumla na Kati haswa kwenye soka.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV