Kocha mwenye nafasi kubwa ya kuiongoza Simba kwenye michuano ya Kagame baadae mwezi huu, Masoud Djuma, ameamua kukifumua kikosi kile ambacho kilikuwa kikitumiwa na aliyekuwa bosi wake, Mfaransa, Pierre Lechantre.
Uamuzi wa Mrundi huyo umekuja siku chache baada ya Lechantre kuachana na timu hiyo huku kikosi hicho kikiwa kinajiandaa na michuano ya Kagame inayoanza Juni 29, mwaka huu jijini Dar.
Kikosi cha Simba ambacho wikiendi iliyopita kilishika nafasi ya pili kwenye michuano ya SportsPesa Super Cup baada ya kufungwa mabao 2-0 na Gor Mahia katika fainali, hivi sasa kimepewa mapumziko ya wiki moja kabla ya kuanza maandalizi ya kushiriki Kagame.
Akizungumza na Championi Jumatano, Djuma ambaye ni mnazi mkubwa wa Simba alisema: “Baada ya mapumziko haya ya wiki moja, vijana watarudi kwa ajili ya maandalizi ya Kagame, tunataka tufanye vizuri kwenye Kagame zaidi ya kule Kenya tulipotoka.”
“Lakini katika kufanya vizuri huko, ni lazima tubadilishe kikosi, wale wachezaji tuliowatumia sana kwa msimu mzima ni lazima tuwapumzishe kwa ajili ya kuwaandaa kwa msimu ujao, na naamini tutafanya vizuri kwa hawa wengine watakaopata nafasi.
“Msimu ujao wa ligi tunataka tufanye vizuri zaidi ya msimu huu, hivyo ni lazima niwapumzishe vijana wangu wale ambao ni tegemeo kikosini.”
Muwekezaji wa Simba, Mohammed Dewji ‘MO’ amepania kusajili kikosi kipana na kitakachokuwa tishio kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika inayoanza Desemba mwaka huu.
CHANZO: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment