Kiungo mchezeshaji wa Simba, Haruna Niyonzima raia wa Rwanda ameweka bayana kwamba kwa msimu ujao anajipanga kuona anafanya kitu cha tofauti na lazima abebe moja ya tuzo za mdhamini wao Mohammed Dewji ‘MO’.
Niyonzima ambaye alitua Simba mwanzoni mwa msimu uliomalizika hivi karibuni hakuwa na msimu mzuri kutokana na kuandamwa na majeraha ya muda mrefu. Kutokana na kutokuwa na mchango mkubwa Niyonzima alijikuta akiwa nje ya wachezaji ambao waliwania tuzo mbalimbali ndani ya timu hiyo ambazo zilitolewa Jumatatu iliyopita na MO.
Katika tuzo hizo John Bocco ndiye aliyeibuka kidedea kati ya wote walioshiriki. Akizungumza na
Championi Ijumaa, Niyonzima ambaye ni baba wa watoto pacha Atka na Atfa, amesema kwamba tuzo hizo zimempa mzuka wa kufanya vizuri kwa msimu ujao kuona kwamba naye anakuwa mmoja wa watakaotwaa baada ya kukosa kwa msimu huu.
“Ni jambo zuri kuona kwamba kuna tuzo kama hizi ndani ya timu kwani zinaamsha hamasa kwa wachezaji kupambana kuhakikisha mwishoni mwa msimu wanakuwa moja ya watu wanaogombania tuzo, ni jambo zuri sana kuwepo kwake.
“Kwangu sikuwa na msimu mzuri kwa safari hii lakini kwa mara nyingine nitapambana vizuri na kujitoa kwa timu kuona kwamba nakuwa sehemu ya wachezaji ambao majina yao yatakuwepo kwenye kuwania tuzo hizo msimu ujao,” alisema Niyonzima mchezaji wa zamani wa Yanga na APR ya Rwanda.
CHANZO: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment