AZAM FC KUSEPA UGANDA NA JESHI KAMILI
Uongozi wa Klabu ya Azam, umeweka wazi kuwa msafara wa timu hiyo sambamba na benchi lake la ufundi utaondoka nchini Julai 30 kwa ajili ya kuelekea nchini Uganda watakapoenda kuweka kambi ya muda mfupi ya kujiandaa na msimu ujao wa ligi huku wakiondoka na wachezaji wote katika msafara huo.
Azam FC chini ya kocha wake Hans van Der Pluijm itakuwa timu ya pili kwa msimu huu kutimkia nje ya nchi baada ya hivi karibuni Simba kukimbilia Uturuki. Wanalambalamba hao wataenda Uganda kwa ajili ya kambi hiyo ambapo pia watakuwa na michezo ya kirafiki.
Kwa mujibu wa Championi Jumatano, Ofisa Habari wa Azam, Jaffar Idd amesema kuwa wataenda nchini humo Julai 30 wakiwa na kikosi kama ambavyo benchi la ufundi limependekeza kwa ajili ya kwenda kuwaona wachezaji wao vizuri na kutengeneza mipango ya msimu ujao.
“Tunatarajia kuondoka Julai 30 kwenda Uganda kama ambavyo tulipanga awali ambapo tukiwa huko tutakuwa na michezo ya kirafiki na wenyeji wetu wakiwemo Vipers ambao wamethibitisha kucheza na sisi kwa ajili ya kujipima nguvu.
“Tutaenda tukiwa na kikosi chetu kamili kama wataachwa wachezaji basi watakuwa wachache na kwa sababu maalumu lakini tofauti na hivyo hatutaweza kumuacha mchezaji yeyote yule kwa sababu kocha wamependekeza twende na wachezaji wote,” alisema Idd.








0 COMMENTS:
Post a Comment