FEI TOTO AANZA NA MKWARA WA KWANZA YANGA SC
BAADA ya kusaini mkataba wa miaka mitatu wa kuichezea Yanga, kiungo mpya wa timu hiyo, Feisal Salum ‘Fei Toto’ ameibuka na kutamka kuwa amekuja kucheza na siyo kukaa benchi, hivyo hana hofu yoyote juu ya hilo.
Kauli hiyo, aliitoa hivi karibuni baada ya kiungo huyo kutambulishwa na timu hiyo akitokea JKU inayoshiriki Ligi Kuu ya Zanzibar.
Kiungo huyo anatarajiwa kukutana na upinzani wa namba kutoka kwa viungo nane ambao ni Papy Tshishimbi, Deus Kaseke, Jafary Mohammed, Mohamed Issa ‘Banka’, Raphael Daud, Pius Buswita, Said Makapu na Thabani Kamusoko.
Akizungumza na Championi Jumatano, Fei Toto alisema kuwa amekuja Yanga akiwa anatarajia kukutana na ushindani wa viungo wengi wenye uwezo mkubwa, hivyo hilo halimpi tabu.
“Ninaamini uwezo wangu wa ndani ya uwanja na uzuri mpira unachezwa uwanjani, hivyo sina hofu juu ya hilo.
“Kikubwa ninawaahidi Wanayanga kuipambania timu yangu kwa kutimiza majukumu yangu yote nitakayopewa na kocha wangu na kikubwa ni katika kuipa mafanikio Yanga na hilo linawezekana.
“Kikubwa ninaomba ushirikiano kutoka kwa wachezaji wenzangu wote wale wapya na wa zamani niliowakuta Yanga,” alisema Fei Toto.
0 COMMENTS:
Post a Comment