NA SALEH ALLY
WAKATI Abbas Tarimba alipoamua kukubali alichoombwa na wanachama wa Yanga kwa ajili ya kufanya mambo yatulie ndani ya Yanga, nilikuwa nina hofu kuu kama angeweza kudumu kwa muda mrefu.
Hofu yangu kwa Tarimba kama angebaki kwa muda mrefu ilitokana na mambo matatu makubwa ambayo hasa yalikuwa msingi wa mimi kuona kama vile haitawezekana.
Moja ilikuwa ni namna mambo yalivyo ndani ya Yanga katika kipindi hiki, tayari hata Tarimba hajakubali kuingia kusaidia, kulikuwa na makundi ambayo yalikuwa yakipishana kupitia suala la maswali.
Mara kadhaa, tuliona lawama ya kutoka huku kwenda huku na ile ya kule kuvushwa upande mwingine. Maana yake hakukuwa kumetulia kwa maana ya uhalisia wa ukweli na maumivu ya dhati.
Pili, nilijua Simba wasingefurahi, lazima wangeihusisha kazi ya Tarimba kama sehemu ya mdhamini na yeye kuamua kuingia Yanga kuokoa jahazi.
Tatu ni aina ya ufanyaji kazi wa Tarimba, aina ya mtu ambaye anazungumza mambo moja kwa moja. Hana kona wala mzunguko, anayetaka ukweli na akikosewa anasema kwa wakati bila ya kuficha au kusubiri.
Kwa wale wanaomkumbuka Tarimba, ndiye yule aliyepata upinzani mkubwa kutoka kwa Yanga Asili iliyokuwa inaongozwa na marehemu Yusuf Mzimba. Wakati huo yeye ndiye alikuwa ameanzisha hoja ya Yanga kuwa kampuni na suala hili lilionekana kama ni kuigawa Yanga na Yanga Asili, wakaanzisha upinzani mkubwa ambao kwa hakika haukuwa na faida kwa Yanga.
Inawezekana Yanga ingekuwa mbali zaidi ya klabu yoyote nchini kama Tarimba angeeleweka wakati huo. Alichokiona miaka zaidi ya 18 iliyopita, sasa ndiyo gumzo.
Hivyo, ilikuwa lahisi sana kwake safari hii kuachia ngazi katika kamati yake kama angeona mambo hayaendi sababu ya yale makundi, hicho ndiyo kimetokea na wakati akitangaza alielezea kukerwa na hali hiyo.
Lile la pili, kwa kiasi fulani niliona malalamiko ingawa hayakuwa kiofisi. Mwisho halikuwa suala ambalo lilimtatiza sana na badala yake anaonekana amepania kuisaidia Yanga kuhakikisha inapata ahueni, huenda hata Simba hawakulipa nafasi yoyote.
LAkini hili la tatu la kuwa ni mtu anayependa kusema moja kwa moja, limekuwa gumu ndani ya Yanga kipindi hiki kwa kuwa wengi walikuwa wakifanya mambo kwa mpindo na kusababisha mgawanyiko na ikiwezekana makusudi. Kweli, Tarimba ameona ni kama mtu asiyesikilizwa na ushirikiano ni mdogo na hili ndilo lilikuwa hofu kuu kwangu.
Unapomuingiza mtu kama yeye, maana yake suala la uhakika wa matumizi ya fedha katika utaratibu sahihi ni mambo yatakayopewa kipaumbele. Kuhoji, kutaka kujua faida na hasara ya jambo na uhakika wa mambo pia.
Mwisho, Tarimba ameamua kuondoka kama ambavyo nilifikiri. Lakini Yanga lazima wakubali kwamba, pamoja na uamuzi wake wa kukaa kando, wasikubali kumpoteza.
Nazungumzia kumpoteza kwa maana ya kuamua kumuachia aondoke kabisa. Kwamba akae kando kabisa, halitakuwa jambo sahihi.
Kama wanajua kuna sehemu hawakuelewana naye vizuri, basi ni suala la kuzungumza naye lakini lazima wajue kuwa wanamhitaji katika kipindi kingine na hasa watakapokuwa wanakwenda katika mpito wa mabadiliko ya mfumo.
Wasikubali aamue kukaa kando kutokana na maudhi aliyoyapata alipoamua kuipigania Yanga. Achana na hivyo, lazima wawe karibu naye kama mmoja wa wenyeviti walioiongoza Yanga.
Lakini suala la Tarimba kuwa muasisi wa mabadiliko hayo, bado msaasa wake unahitajika sasa na baadaye. Kama kuna tofauti, hasa na uongozi, zimalizwe na kumpa nafasi Tarimba ya kushauri kama mkongwe, kukataza na ikiwezekana kuhumiza kwenda kwenye mabadiliko.
Tarimba ni sawa na hazina ambazo Yanga wamebahatika kuwa nazo. Safari hii wameshindwa kuelewana, lakini hakikisheni Yanga hamumpotezi kwa kuwa kwenu Tarimba ni sawa na maji, usipoyaoga, utayanywa na usipoyanywa, utayatumia hata kupikia.
ACHANA NA MAMBO YA YANGA KILAZA WEWE
ReplyDeleteTulia dawa iingie
DeleteHUYU TATIZO KWELI UANDISHI GANI HUUU? UPUUZI GANI HUU UNAOANDIKWA?
ReplyDelete