July 15, 2018



Na Saleh Ally
NINAAMINI utakuwa umelisikia gumzo kuhusiana na Ufaransa, Waafrika wengi wameamua kuiunga mkono kama timu yao iliyoingia fainali ya Kombe la Dunia.


Kawaida Afrika huwakilishwa na timu na idadi ya timu tano ambazo mara nyingi zaidi huishia hatua ya makundi kwa kuwa uwezo ni duni.


Nafasi ya juu zaidi ya Bara la Afrika kufikia katika Kombe la Dunia ni robo fainali na timu mbili tu zimewahi kufika hatua hiyo, nazo ni Cameroon na Senegal kutoka Afrika Magharibi.


Mashabiki wengi wa Afrika, hasa wale wanaokuwa si kutoka katika nchi tano zilizofuzu kuwa wanagawana timu mbalimbali.


Mara nyingi hivi, mgawo wa timu unaanzia Afrika. Wale ambao timu zao hazijafuzu kuonyesha sapoti yao kwa timu za Afrika.


Lakini kwa kuwa timu za Afrika hazina uhai mrefu katika Kombe la Dunia, baada ya hatua za awali, basi watu huanza kugawana timu za Ulaya na Amerika Kusini.


Raha ya soka ni ushabiki, kama hauna timu unayoiunga mkono basi hakuna raha. Ili kufanya mambo yanoge lazima uchague timu.



Ndipo kila mmoja anaanza kuchagua timu kutokana na upendeleo wa jambo fulani. Inawezekana mchezaji anayechezea katika timu ya ligi ya nchi inayomvutia kama La Liga, Seria A, Premier League na kadhalika.


Bado inawezekana chaguo likatengenezwa na rangi za jezi, inayovaa njano au nyekundu na kadhalika. Pia mvuto unaweza kuwa na mchezaji wa klabu anayoishabikia katika ligi za Ulaya.


Inawezekana pia rangi ya mwili au asili. Kwamba timu fulani ina Waafrika wengi, basi akachagua ndiyo timu yake ya mashindano.


Hili la mwisho la ndilo linalowafanya wengi kuiunga mkono Ufaransa katika mechi ya fainali ya Kombe la Dunia itakayopigwa kesho Jumapili kuhitimisha michuano hiyo iliyoanza mwezi uliopita.


Ufaransa inaungwa mkono kwa kuwa ina wachezaji 15 ndani ya kikosi chake kinachoshiriki Kombe la Dunia wakiwa walizaliwa au wana asili ya Afrika.


Kwa sasa Ufaransa inaonekana ni kama timu ya Waafrika inayotokea Ulaya. Wengi wanafurahishwa na hilo ingawa haina wachezaji wengi wanaocheza Ligi Kuu England kwa kile kigezo cha kusapoti wachezaji wanaotokea katika klabu inayokuvutia.


Wachezaji hao wameifikisha Ufaransa katika fainali ya Kombe la Dunia. Ufaransa ndiyo timu yenye mchanganyiko kwa asilimia kubwa zaidi kwa maana ya kuwa na wachezaji wengi zaidi wenye asili ya Afrika.


Pamoja na sapoti hiyo ya Afrika, kumekuwa na maswali ambayo yako kama utayapa nafasi yanaweza kukupa funzo kwamba kuna jambo ambalo pamoja tunaweza kujifunza.


Kwamba wachezaji 15 wenye asili ya Afrika wakiwemo waliozaliwa katika bara hili, wameipeleka Ufaransa katika fainali ya Kombe la Dunia.


Timu za Afrika zinashindwa kusonga mbele. Utaona mara nyingi Ufaransa imekuwa ikitamba kupitia wachezaji wenye asili ya Afrika.

Mara nyingi Afrika Kaskazini kama akina Zinedine Zidane na wenzake, lakini hata Afrika Magharibi. Safari hii inaonekana hadi Afrika ya Kati na ile ya Kusini upande wa Angola. Inayokosekana ni Afrika Mashariki tu.

Wachezaji hawa wanaweza vipi kufanya wakiwa wanaiwakilisha bendera ya nchi kutoka Bara la Ulaya lakini wale wa asili kabisa wanaotokea Afrika wanashindwa?

Sehemu ya mijadala ni kuangalia Waafrika tunavyokwama. Unajiuliza kama Samuel Umtiti ambaye alizaliwa Cameroon, kama angekuwa katika timu hiyo angeisaidia kuingia fainali ya Kombe la Dunia?

Wakati fulani Corentin Tolisso alitaka kuichezea timu ya Taifa ya Togo kabla ya kupata nafasi Ufaransa. Kama ilivyo kwa Adili Rami aliyewahi kushawishiwa aichezee Morocco maana wazazi wake wote wana asili ya nchi hiyo.

Nidhamu yao inatoka wapi hadi wakafanikisha hili? Lazima tukubali, kuna mengi tunakosa Afrika na hasa kuwa na mwendelezo wa rushwa kupindukia, kufanya mambo kwa kufuata maslahi yetu binafsi, kumekuwa kunaziangusha timu za Afrika.

Kwa kifupi msingi ni mbovu na unaweza kuligeuza hili suala kwa upande wa pili. Kwamba wachezaji wa Afrika ambao wanategemewa au wale ambao hufanya vizuri, nao hutokea barani Ulaya.

Maana wanaofanya vizuri Ulaya, basi wanaweza kufanya vizuri na timu za taifa, angalau. Wale wanaotokea Afrika, nafasi yao ni finyu sana.

Tukubali, wachezaji wa Afrika pia hawana nidhamu, si wenye malengo sahihi, hawataki kujifunza zaidi, wanaridhika mapema na kujisahau haraka.

Viongozi wanaowangoza wachezaji hao, hawana misingi bora ya uendelezaji na ukweli wanafanya kila kitu katika mpira kwa ajili ya maslahi yao binafsi na ndiyo jambo linalotuangusha kwa kiasi kikubwa.

Ufaransa pia inaweza kuwa somo, angalia wachezaji walivyo na mapenzi na wanaweza kulipigania taifa ‘lao’ kwa juhudi za juu.

Wale wa Afrika mara nyingi umewasikia katika ya michuano wakilia au kulalama kuhusiana na posho zao, jambo ambalo si rahisi kulisikia kwa timu za wenzetu.

Suala la posho linawajumuisha watoaji kwa kuwa si waadilifu wanatengeneza migogoro, lakini wachezaji pia si wavumilivu, wanasababisha sokomoko.

Upendo ni sehemu ya mafanikio ya utendaji bora. Upendo unasukuma kutaka kufikia mafanikio na ikiwezekana kupigana bila ya kuchoka.

Mafunzo ya Wazungu ni bora kuliko yetu, wachezaji hao wangeishi Afrika wangepokea mafunzo ya Afrika na kuwa hawana lolote kama walivyo wetu. Hivyo, tunaweza pia kujifunza kwamba Wazungu, kuna jambo wanafanya na vema kuiga kwa ajili ya mabadiliko.

Tujifunze na kuamini, tujifunze na kubadilika na ikiwezekana badala ya kuishangilia Ufaransa pekee, basi tujiulize maswali mengi na kutafuta majibu kuwa kwa nini iko hapo na wachezaji wanaoshindwa kama wangekuwa Afrika!

 ASILI ZAO AFRIKA:
Samuel Umtiti-(Kazaliwa Cameroon)
Adili Rami (Ana wazazi Wamorocco)
Thomas Lemar (Asili ya Nigeria)
Benjamin Mendy (Asili ya Senegal)
Nabil Fekir (Wazazi Waalgeria)
Djbril Sidibe (Asili ya Senegal)
Steve Mandanda (Alizaliwa DR Congo)
Blaise Matuidi (Baba Muangola, Mama Mkongo)
Steven Nzonzi (Asili ya DR Congo)
Ng’olo Kante (Asili ya Mali)
Ousmane Dembele (Asili ya Mauritania)
Corentin Tolisso (Asili ya Togo)
Presinel Kimpembe (Baba Mkongo)
Paul Pogba (Asili ya Guinea)
Kylian Mbappe (Baba Mcameroon, Mama Mualgeria)


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic