July 18, 2018






Na Mwandishi Wetu, Songea
BAADA ya mnyukano wa siku tatu mfululizo katika mashindano ya Ngoma za Asili Tamasha la Majimaji Selebuka mjini Songea, Ruvuma hatimaye kundi la Keifo Ling’oma kutoka Kyela Mbeya limeibuka bingwa.

Kundi hilo toka awali lilionyesha kuteka mashabiki wengi waliokuwa wakijitokeza kwenye Uwanja wa Majimaji mjini hapa kutokana na umahiri wao wa kulishambulia jukwaa huku wachezaji wake baadhi licha ya kuwa na maumbo makubwa lakini walikuwa wepesi kupita kiasi kufuata mirindimo ya ngoma.


Akitangaza washindi, Jaji Mkuu wa mashindano hayo, Nathan Mtega, aliwatangaza Keifo mabingwa baada ya kupata pointi 94.3 wakifuatiwa na kikundi cha Sonamcu ‘Lizombe’ cha mkoani Ruvuma pointi 88.3 huku nafasi ya tatu ikienda kwa Mshikamano Group Kioda Mangua pia Ruvuma pointi 84.

Bingwa katika mashindano hayo alijitwalia kitita cha Sh. 500,000 na Kombe, wa pili Sh. 300,000 na Kombe huku wa tatu akijipoza na Sh. 250,000.
Vikundi saba vilifanikiwa kuingia fainali ambavyoni Keifo, Sonamcu, Mshikamano, Songera, Ruvuma Champion, Kinjekitile na Mshikamano Likuyufusi ambakoukiacha washindi watatu bora vilivyobakia vilipata kifuta jasho cha Sh. 100,000 kila kimoja.

Mashindano hayo yalishirikisha jumla ya vikundi 15 kutoka ndani na nje ya Mkoa wa Ruvuma.

Vikundihivyo vilichuana vikali kwenye hatua ya mchujo na vikundi saba kufanikiwa kupenya hatua ya fainali.

Hata hivyo haikuwa kazi nyepesi kupatikana kwa washindi kutokana na kila kikundi kujiimarisha ipasavyo hasa katika kipengele cha ujumbe wa kazi zao, achilia mbali kutawala jukwaa.

Mtifuano zaidi ulikuwa ni kupima uzito wa ujumbe kutokana na kazi nyingi kuvutia huku asilimia kubwa ya nyimbo zikielekeza pongezi kwa Serikali ya awamu ya tano ya Rais John Magufuli kula sahani moja na ‘watenda maovu nchini’, ulipaji kodi na kujikinga na maambukizi ya virusi vya Ukimwi.

Tamasha hilo la wiki nzima linaloandaliwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Songea Mississippi (SOMI), kwa ukaribu na Mwandi Tanzania, hufanyika kila mwaka kwenye Uwanja wa Majimaji kwa kushirikisha michezo ya riadha, soka, mbio za baiskeli, ngoma za asili, mdahalo kwa shule za sekondari, fursa za kibiashara kwa wajasiriamali kupitia elimu na maonyesho ya kibiashara pamoja na utalii wa ndani  ya mkoa wa Ruvuma.

Kwa mwaka huu, tamasha hilo lilikata utepe Julai 14 kwa mchezo wa riadha- mbio za Mita 800 kwa watoto, Kilomita 5, Kilomita 21 ‘Nusu Marathon’ na Kilomita 42 ‘Marathon’.

Tamasha la mwaka huu linatarajiwa kufikia tamati Julai 22 kwa mtanange wa mechi ya Veterani ya Watani wa Jadi, Simba na Yanga kwenye dimba la Majimaji.
 


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic