NA SALEH ALLY
KRC Genk sasa ni moja ya timu maarufu sana hasa nchini Tanzania na hii ni kutokana na Mbwana Samatta.
Samatta anakipiga Genk ya Ubelgiji ambayo alijiunga nayo akitokea TP Mazembe ambako alipata mafanikio makubwa.
Wakati Samatta akifanya vizuri, Genk inaonekana ni njia sahihi ya wachezaji kupata timu katika ligi nyingine kubwa kama Italia, Ufaransa, Hispania, Ujerumani na England.
Wachezaji wengi wamepita Genk na kwenda katika ligi hizo na hiyo inakuwa ni taa ya mambo mazuri kwa Samatta.
Mfano wao ni Leon Bailey ambaye anacheza katika Bundesliga akiwa na Bayer Leverkusern na huyu alicheza pamoja na Samatta katika msimu mmoja. Yeye akiwa ameichezea Genk 2015-17.
Kiungo wa Leicester City, Wilfred Ndidi alicheza na Samatta pia, yeye akianzia 2015 hadi 2017 alipotua England.
Kipa wa zamani wa Chelsea, Thibaut Courtois ambaye sasa amejiunga na Real Madrid alipita Genk na sasa ni nyota mkubwa duniani.
Achana na hao, nyota wa zamani wa Chelsea na ghali zaidi sasa Manchester City Kevin De Bruyne, naye alipita Genk na kuitumikia kwa muda mrefu akianzia 2005 hadi 2012.
Hii ni njia nzuri kwa Samatta ambaye ameanza kuonyesha cheche akipiga hat trick yake ya kwanza katika Play Off za Europa League dhidi ya Brondby.
Kikubwa ni kwa Samatta kuendeleza anachokifanya sasa na zaidi, huenda akakaa Genk kwa muda mfupi sana.
Namba anayocheza Samatta ni tatizo kubwa duniani, washambulizi hatari wanatakiwa kila sehemu na kama ataenda na mwendo huo ana nafasi ya kucheza ligi nyingine kubwa.
Si vibaya kusema hatuna hofu na Samatta kwa kuwa amekuwa ni mtu anayejitambua, anajiongoza na si mtu wa utani kazini.
Ambacho Watanzania wanaweza kumpa ni maombi asiumie na yeye kuendelea kufanya vema. Ikiwa hivyo, bila shaka, siku si nyingi sana, tutasikia habari njema.
Kila la kheri.
Amin
ReplyDelete