MOURINHO NA KIBARUA KIZITO KESHO
Manchester United itakuwa inasaka ushindi wa kuwasahaulisha mashabiki wake na kipigo cha Brighton & Hove Albion wakati watakapoikaribisha Tottenham Hotspur kwenye Uwanja wa Old Trafford kesho Jumatatu.
Miamba hiyo wiki iliyopita ililala mabao 3-2 kwa Brighton ugenini kwenye mechi ya Ligi Kuu England.
Manchester United wana mechi ngumu kwa kuwa Tottenham Hotspur imeshinda mechi zao mbili za kwanza za ligi baada ya kuiliza Fulham mabao 3-1 na mchezo wa pili ikaichapa Newcastle 2-1.
Hata hivyo, watakuwa na matumaini ya kufanya vizuri baada ya kurudi mazoezini kwa Nemanja Matic, Antonio Valencia na Alexis Sanchez, ambao walikuwa majeruhi. Kocha wa Manchester United, Jose Mourinho bado hajaamua kama atawarudisha mastaa hao kikosini.
Tottenham kwa upande wao watamkosa Son Heung-min, ambaye ameungana na kikosi cha Korea Kusini kwenye Michezo ya Asia inayofanyika nchini Indonesia. Man United, hata hivyo, itaingia ikiwa na rekodi ya kutisha dhidi ya Tottenham linapokuja suala la kucheza Old Trafford, ambapo imeshinda mechi za ligi 21 kati ya 26 dhidi ya Spurs.
Pia Manchester United imeshinda mechi saba zilizopita ikiwa ni rekodi iliyoanzia Machi 2015. Spurs ndio timu ya mwisho ya London kushinda mechi ya Ligi Kuu England kwenye Uwanja wa Old Trafford na ilikuwa siku ya Mwaka Mpya wa 2014. Naye Kocha wa Tottenham Hotspurs, Mauricio Pochettino ameshinda mechi 199 kama kocha na mechi 123 ni katika kipindi akiwa kocha wa Spurs.
0 COMMENTS:
Post a Comment