AMUNIKE AMPA MAKALI STRAIKA MTIBWA
Mshambuliaji tegemeo wa Mtibwa Sugar, Kelvin Sabato ‘Kiduku’ amesema kuwa muda mchache aliokaa pamoja na Kocha Mkuu wa timu ya taifa, Taifa Stars amepata mbinu nyingi sana.
Kiduku aliitwa hivi karibuni kwenye kikosi cha Stars kilichokuwa kinajiandaa na mchezo wa kuwania kufuzu Afcon dhidi ya Uganda chini ya kocha Emmanuel Amunike.
Mshambuliaji huyo aliitwa kwenye kikosi cha Stars baada ya mchezo wa Ligi Kuu Bara waliocheza na Yanga kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ambao walifungwa mabao 2-1.
Kwa mujibu wa gazeti la Championi, Kiduku alisema kwa muda mchache aliokaa pamoja na Amunike amejifunza vitu vingi ikiwemo jinsi ya kupambana na mabeki wa timu pinzani.
Kiduku alisema, pia amejifunza jinsi ya kufunga mabao kwa mashuti na kumchambua kipa akiwa amebaki yeye na kipa, hivyo anaamini akirejea katika ligi atakuwa tishio.
“Lipo wazi hakuna mtu asiyefahamu uwezo mkubwa wa kufundisha wa Amunike tofauti na historia yake ya kucheza soka kwenye klabu kubwa Ulaya.
“Ni kocha anayeweza kumtengeneza kiufundi mchezaji kwa maana ya kumpa mbinu za kufunga mabao mshambuliaji, hivyo binafsi nimejifunza vitu vingi kwa kipindi kifupi cha wiki moja na nusu niliokaa pamoja naye,” alisema Kiduku ambaye aliifunga Simba bao la kuongoza kwenye Ngao ya Jamii.








0 COMMENTS:
Post a Comment