BEKI SIMBA AFUNGUKA MAZITO KUHUSIANA NA STARS
Ni mara chache kwa nchi kama Tanzania kuona mchezaji akidumu kucheza katika kiwango cha juu kwa miaka zaidi ya 12 na kufanikiwa pia kuitwa timu ya taifa mfufulizo kwa miaka yote hiyo na kucheza soka la ushindani.
Beki na kiungo wa Simba, Erasto Edward Nyoni ni mchezaji ambaye anashikilia rekodi ya kuwa ndiye mchezaji pekee aliyedumu zaidi katika kikosi cha timu ya taifa, tangu alipoitwa kwa mara ya kwanza mwaka 2006.
Akiwa na umri wa miaka 30 kwa sasa Nyoni bado anaonekana kuwa na nguvu licha ya umri kusogea, huku akiwa ameitumikia Stars katika michezo kadhaa ya kimataifa akikumbukwa zaidi kwa bao lake safi alilofunga mwaka 2006 dhidi ya Burkina Faso, Juni 16, mwaka 2007 katika mchezo wa kuwania kufuzu Kombe la Mataifa Afrika (Afcon). Burkina Faso wakilala nyumbani kwa bao 1-0.
Ukiachana na rekodi na mambo mengi aliyofanya akiwa na jezi ya Taifa Stars, hivi karibuni rekodi yake iliingia doa mara baada ya kuondolewa kwenye kikosi cha timu ya taifa, kilichoivaa Uganda mwishoni mwa wiki iliyopita katika mchezo wa kusaka tiketi ya kucheza Afcon. Mchezo uliomalizika kwa suluhu.
Nyoni na wenzake waliondolewa na kocha mpya wa Stars, Emmanuel Amunike kwa madai ya utovu wa nidhamu baada ya kuchelewa kuripoti kambini katika muda sahihi uliopangwa, hali ambayo ilizua mijadala kwa mashabiki na wapenzi wa soka nchini. Championi Ijumaa limemtafuta Nyoni na kuzungumza naye, ambapo amefunguka mambo kadhaa kuhusiana na sakata hilo na mipango yake juu ya timu ya taifa.
ULIJISIKIAJE BAADA YA KUTEMWA TIMU YA TAIFA?
“Kiukweli nilijisikia vibaya na niliumia sana wala sikutegemea kwa sababu halikuwa lengo langu, ndiyo maana nilienda kambini baada ya kuambiwa
tuende ila kwa bahati mbaya mwalimu alisema kuwa maamuzi yameshapita na wachezaji wengine wameshachukua nafasi zetu. “Niliumizwa sana na kile kitendo ilikuwa ni pigo kwangu kwa kukosa kuwepo timu ya taifa kwa mara ya kwanza.
YALE MAAMUZI YALIKUATHIRI VIPI?
“Yaliniathiri kwa kiasi kikubwa
sana kwa sababu yameharibu ‘CV’ yangu, unajua mimi sijawahi kuchelewa kambini hata mara moja toka nimeanza kucheza, nimekuwa mtu ambaye nafuata taratibu na nidhamu. “Iwe timu ya taifa au klabu yoyote ambayo nimecheza sijawahi kuchelewa mara zote nimekuwa nikiwahi kambini, pia imeathiri kwa upande wa rekodi yangu ya kucheza timu ya taifa kwa muda mrefu, hivyo suala la kukosekana bila matarajio yangu imeniuma sana kiukweli.
ILIKUAJE MKACHELEWA KUINGIA KAMBINI?
“Ishu ilikuwa ni mawasiliano, unajua mimi namilikiwa na klabu siwezi kuondoka mpaka nipate ruhusa ya viongozi wangu kwamba natakiwa niende sehamu fulani.
sita kwa bahati mbaya tulipoingia kambini, tukaambiwa tumeondolewa kikosini kwa hiyo nahisi mawasiliano yalikuwa siyo mazuri baina ya uongozi.
SOMO GANI UMELIPATA KUTOKANA NA HILO?
“Somo ambalo nimelipata mimi na wachezaji wengine ni kubwa na linatufundisha kuwa inapotokea suala la timu ya taifa au ratiba yoyote inatakiwa tuitikie haraka na kufuata maagizo tutakayopewa. “Kuitwa timu ya taifa ni sifa kubwa sana kwa kuwa kuna wachezaji wengi ambao wanaitafuta hiyo, hivyo tunapaswa kuitikia wito haraka pindi tunapohitajika timu ya taifa kwa ajili ya kuiwakilisha nchi. “Kwani maisha ya mpira yanahitaji sana nidhamu ndiyo maana nakwambia kuwa mimi binafsi niliumia sana kwa sababu watu wameniweka kwenye kundi la wachezaji ambao hawana nidhamu, wakati mimi ni mtu ambaye nafuata misingi ya nidhamu.
ULIFIKIRIA KUSTAAFU KUCHEZA STARS BAADA YA KUTEMWA?
“Hayo ni maamuzi tu binafsi lakini ukiona mpaka leo nipo nacheza timu ya taifa au nacheza mpira basi ujue nimevumilia mambo mengi sana huko nyuma. “Nashukuru Mungu alinipa subira japo niliumia baada ya kutokea lile suala ndiyo kitu ambacho nashukuru, nafahamu hayo ni mambo tu ya mpira yanatokea na ninaamini yatapita kama nilivyokwambia mpaka unaniona leo nimefika hapa ujue nimevumilia mengi kwenye mpira.
UNAHITAJI KUCHEZA TIMU YA TAIFA KWA MUDA GANI?
“Siwezi kusema nataka nicheze mpaka muda gani au baada ya miaka mingapi ila kikubwa ni kwamba mipango yangu nicheze timu ya taifa mpaka pale nitakapoona nguvu zimeniishia na siwezi tena kucheza, ndipo nitakapoacha na kufanya shughuli nyingine.
ULIIONAJE STARS KWA MARA YA KWANZA IKICHEZA CHINI YA AMUNIKE?
“Timu ni mzuri sana ilicheza vizuri na nilipenda sana mbinu aliyoitumia mwalimu dhidi ya Uganda, kwa sababu kila mechi hupangwa na plani yake na uzuri hata wachezaji wenzangu walifuata zile plani. “Pia wachezaji walicheza kwa kujituma sana ni kitu ambacho kilitusaidia kupata suluhu ugenini, kwa jumla timu ni mzuri kama tutaongeza juhudi tutafika mbali.
MRISHO NGASSA KAREJEA YANGA, UNAHISI ANAWEZA AKAPATA NAFASI STARS? “Ndiyo anaweza akarejea kama yeye mwenyewe ataamua, kwani bado ana uwezo wa kucheza mpira lakini pia ni mzoefu, ashacheza sana timu ya taifa, nafikiri akiongeza juhudi mwalimu anaweza akamuona na kumuita.
ALIKIBA KAGEUKIA SOKA KWA UPANDE WAKO UNAHISI ATAFANYA VIZURI? “Kiba ni mchezaji mzuri na ana matumizi mazuri ya mguu wake wa kushoto na nimecheza naye sana pale Muhimbili, kuna timu fulani ya Haruna Moshi ‘Boban’ hivyo namfahamu vizuri ataisaidia Coastal,” anamaliza Nyoni ambaye amewahi kutwaa ubingwa wa ligi kuu akiwa Azam FC na Simba SC.
Na Issa Mponda, Championi
0 COMMENTS:
Post a Comment