September 28, 2018





NA SALEH ALLY
JUMAPILI inakuwa ni siku ya kwanza ya Ligi Kuu Bara ambayo imesubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini hasa katika Ligi Kuu Bara ya msimu huu.


Hii inakuwa ni mechi ya kwanza kabisa ya Ligi Kuu Bara kuwakutanisha watani wa jadi Simba watakaokuwa nyumbani dhidi ya Yanga ambao sasa wanaonekana kufanya tofauti.


Yanga wanakwenda na mwendo mzuri kabisa. Inaonekana wameanza tofauti na ilivyokuwa matarajio ya wengi na wakati fulani nilieleza kuhusiana na kuwadharau wakati viwango vya Ligi Kuu Bara huwa havina tofauti kubwa sana.


Mashabiki wa Yanga na Simba wamekuwa ni wa aina tofauti na wengi ambao nimebahatika kuwashuhudia nikiwa uwanjani wakishangilia timu zao.


Nimepata bahati kubwa ya kushuhudia mechi nyingi zikiwemo zinazohusisha timu maarufu duniani kama Manchester United, Arsenal, Chelsea, FC Barcelona, Atletico Madrid, Real Madrid, Kaizer Chiefs, Orlando Pirates na nyingine nyingi.


Mashabiki wengi wa timu hizo hufika uwanjani kwa ajili ya kuziunga mkono timu zao ili kuhakikisha zinashinda mechi husika. Lakini kwa Tanzania, inawezekana hilo lipo lakini ikawa kwa asilimia ndogo sana.

Mashabiki wa Tanzania, huenda uwanjani kuangalia mpira lakini pia huenda uwanjani wakiwa na mambo mengi sana tofauti na mashabiki wa nchi mbalimbali ambao nimekuwa nikiamini wanaijua vizuri raha ya mpira kwa kuwa hawaitangulizi karaha hata kabla ya mpira kuanza.



Kwa kuwa mpira ni keshokutwa, nimeona si vibaya kukumbusha kwa kuwa nimebahatika pia kushuhudia uwanjani au kwenye runinga zaidi ya mechi 50 za watani wa jadi na nimejitahidi kuziangalia kwa tathmini ya kiufundi zaidi.


Kuna mambo ambayo yanapaswa kwa shabiki anayeingia uwanjani na kuna mengi wanapaswa kuyaacha ili kutengeneza furaha sahihi kwa kuwa pale uwanjani si sehemu ya mateso na lengo si kwenda kutengeneza karaha.

Tukubaliane kila mechi moja ya Simba na Yanga ni sehemu ya rekodi na mara zote imekuwa ikiacha funzo hasa kwa waliotaka kufurahi na kujifunza.


Kuna mambo mtu anaweza kufanya akiwa uwanjani. Uhuru wa kushangilia, kutania kistaarabu, pia kutanguliza suala la heshima mbele kwa wengine.

Pamoja na hayo, kuna mengi yanapaswa kufanyika hasa katika suala la kubadilika na kutengeneza njia sahihi inayothibitisha ushabiki wako wa soka.

Moja, hakuna haja hata kidogo mashabiki kupigana hasa kwa wale ambao wanakuwa wamevaa rangi tofauti. Sababu ipi hasa ya kumuumiza mwenzako na nani amesema ushabiki ni kuumizana.

Kama kuna mtu amevuka upande ambao si wake, aelezwe aondoke na kama kuna ubishi watu wa usalama wapo uwanjani, wafanye hivyo.

Pili, kushangilia kwa namna yoyote ile, si lazima kuwe na matusi kwa kuwa inawezekana kushangilia bila ya kutoa lugha chafu.

Lugha chafu zimewakimbiza watu wengi wastaarabu kwenda uwanjani, watoto na hata watu wazima.

Tatu, ni jambo la msingi sana kuheshimu wanawake. Inatakiwa kuwaheshimu dada na mama zetu hasa wanaojitokeza uwanjani badala ya kuzungumza nao kwa lugha ya kejeli, mwisho inawafanya wengi waone uwanjani ni kama sehemu hatari kwao.


Mwisho, kama mwamuzi amekosea, au mchezaji amekosea. Kuna haja gani ya kurusha chupa uwanjani au kuwarushia chupa watu wengine?

Kwa nini mashabiki wengi wanataka kuonekana ni hatari au wana hasira sana mbele ya wengine? Kwani ukishabikia kwa raha zako bila ya kubeba ujiko mbele ya wengine utapata hasara ipi?

Mnaofanya hivyo, inawezekana ilikuwa ulimbukeni, sasa ni wakati wa kubadilika. Furahia kwa raha zako na si kutaka kuonekana na mwisho unakuwa bugudha kwa wengine.

Mwisho niwakumbushe, timu yoyote inaweza kufungwa na pia sare ni sehemu ya mchezo, tafadhali msiende na matokeo mfukoni. 


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic