· Wanariadha wakongwe wapongeza, Tanzania sasa kurejea kuwa kinara
MultiChoice Tanzania ikishirikiana na klabu ya riadha ya Rift Valley ya Karatu imefungua kambi maalum ya raidha wilayani Mbulu ambapo wanariadha 16 watakuwa wakipatiwa mafunzo kwa mwaka mzima. Uzinduzi huo ulifanyika mwishoni mwa wiki na kuhudhuriwa na mwanariadha mwenye sifa ya kipekee duniani John Stephen Akhwari, katibu mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania Wilhelm Gidabuday na Naibu Rais wa Shirikisho hilo Dk. Hamad Ndee.
Kambi hiyo ina wanariadha wengi wenye umri mdogo akiwemo Francis Damiano Damas ambaye ni balozi maalum wa DStv na mshindi wa medali ya shaba katika mashindano ya vijana ya Jumuia ya Madola yaliyofanyika visiwa vya Bahamas mwaka jana
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi huo, Mkuu wa Mawasiliano MultiChoice Tanzania Johnson Mshana, amesema kuwa dhamira yao ni kuhakikisha kuwa riadha inakuwa na mchango mkubwa katika kuliletea taifa sifa, kutoa ajira kwa vijana wengi na kuchangia kikamilifu katika kukuza uchumi wa nchi.
“Tunataka Tanzania ijulikane ulimwenguni kote kama chimbuko la mabingwa. Tumedhamiria kikamilifu kukuza mchezo huu na kufanya kama chanzo kikubwa cha ajira kwa vijana wetu, lakini pia riadha ni mchezo, burudani na ni sekta nyeti kiuchumi kama ikiendelezwa”
“Tunataka kuusikia wimbo wetu wa taifa katika mashindano makubwa ya riadha ya kimataifa, tunataka kuiona bendera yetu ikipepea juu katika kila mashindano makubwa ya riadha ya kimataifa , tunataka mamia ya vijana wetu wenye uwezo mkubwa katika riadha washiriki kwenye mashindano makubwa , waweze kujipatia kipato na kuwa chanzo cha maelfu ya ajira na hatimaye kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya kiuchumi ya nchi yetu” amesema Mshana.
Kambi hii ilianza rasmi tarehe 1 Septemba 2018 na itasimamiwa na klabu ya Riadha ya Rift Valley kwa ufadhili wa kampuni ya MultiChoice Tanzania, kwa mujibu wa makubaliano kati ya pande hizo mbili. Kwa kuanzia kambi hiyo ina jumla ya wanariadha 16 ambapo awamu ya kwanza ya mafunzo itakuwa kwa miezi mitatu (Septemba – Novemba 2018) na awamu ya pili (Januari- Machi 2019).
Kwa upande wake mgeni maalum katika ufunguzi huo na mwanariadha nguli aliyewahi kuweka rekodi ya aina yake mashindano Olyimpic ya mwaka 1968 nchini Mexico, Mzee Stephen John Akhwari amesema kuwa huu ni uwekezaji mzuri uliofanywa na kampuni ya MultiChoice na ni mfano wa kuigwa na wadau wengine. “Ni kweli kabisa kuwa kwa muda mrefu kumekosekana uwekezaji katika riadha, mchezo ambao unaweza kuwa nguzo kubwa ya maendeleo ya jamii yetu nan chi yetu kwa ujumla. Huu ni uwekezaji wa maana sana na wenye tija kubwa” alisema Mzee Akhwari
Amewaasa vijana wanaopata fursa ya mafunzo kambini hapo kuitumia vizuri. “Ni jukumu lenu nyinyi kama vijana mliopata fursa hii kuhakikisha kuwa mnaweka bidii kubwa na hatimaye muwe wanariadha wakubwa ulimwenguni na kuilieletea sifa nchi yetu kupitia mashindano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa mtakayobahatika kushiriki.” Kwakuwa kambi ipo hapa karibu na nyumbani kwangu, nawaahidi kuwa karibu nanyi muda wote na nitashiriki kwa kwa hali na mali katika kuwalea na kuwatia moyo” alisema Mzee Akhwari.
Naye Katibu mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania Wilhelm Gidabuday, amesema wamefarijika sana kuona kuwa MultiChoice inaendelea kudhamini riadha kwani wameanza jitihada hizo muda mrefu na matunda yake yameshaanza kuonekana.
Amesema Shirikisho la Riadha la Tanzania litahakikisha kuwa ufadhili huo unakuwa na manufaa na unazaa matunda yaliyotarajiwa ya kuleta medali nyingi zaidi katika mashindano ya kimataifa. “Ufadhili wa aina hii ni muhimu sana kwa maendeleo ya mchezo wa riadha . Tunaahidi ushirikiano wetu wa dhati ili kufanikisha malengo na tutahakikisha kuwa tunatoa ushikiano unaostahili kwa wafadhili wetu” alisema Gida.
Mwaka ulipita, kampuni ya MultiChoice Tanzania ilidhamini kambi ya riadha ya timu ya taifa na pia ilimdhamini mwanariadha Alphonce Felix Simbu, ambaye kwa sasa ni miongoni mwa wanariadha tegemeo kwa nchi hii.
Hivi sasa MultiChoice Tanzania inamdhamini mwanariadha kinda Francis Damiano Damas ambaye ni mshindi wa medali ya shaba katika mashindano ya vijana ya Jumuia ya Madola yaliyofanyika visiwa vya Bahamas mwaka jana.
0 COMMENTS:
Post a Comment