LUGOLA: KWA NINI WANAOKUFA WAKIFANYA MAPENZI HAMCHOMI VITANDA? – VIDEO
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amesema, si watu wote wanaopoteza maisha katika vituo vya polisi wanakuwa wameteswa.
Waziri Lugola pia amehoji, kwani nini mtu akipoteza maisha akiwa kituo cha polisi wananchi wanavamia kituo lakini hawachomi nyumba na kitanda mwananchi anapoaga dunia wakati anafanya mapenzi.
Ameyasema hayo bungeni wakati anajibu maswali ya nyongeza ya wabunge kwenye kikao cha nane cha Mkutano wa 12 wa Bunge unaoendelea jijini Dodoma.
Lugola amesema, mwananchi anaweza kupoteza maisha wakati wowote na mahalali popote na ndiyo maana kwenye Biblia imeandikwa kifo ni mtego, humnasa mtu wakati wowote na mahali popote.
“Kwa hiyo mwananchi anaweza akafa akiwa polisi, anaweza akafa akiwa anafanya mapenzi, anaweza akafa akiwa kwenye gari anasafiri, anaweza akafia hata humu ndani ya Bunge humu. Kwa hiyo isije ikachukuliwa kwamba anayekufia kwenye kituo cha polisi ni kwamba ameteswa” amesema.
Hata hivyo Waziri Lugola amekiri kuwepo kwa matukio ya wananchi kufia mikononi mwa Polisi.
“Na pale ambapo matukio hayo yanajitokeza tumekuwa tukifanya uchunguzi. Na pale inapobainika kwamba Polisi wamehusika tumekuwa tukichukua hatua.
Na ndiyo maana Mheshimiwa Spika tunazuia wananchi wasichukue sheria mikononi za kuanza kuvamia vituo kwa sababu mtu amefia mikononi mwa polisi…
“Na ndiyo maana nimekuwa nikihoji, huyu anayekufa akifanya mapenzi mbona hawaendi kuchoma kitanda na nyumba kwamba amefia mikoni mwa kitanda” amesema Lugola.
Wakati anajibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mlimba, Suzan Kiwanga, Waziri Lugola amesema, Jeshi la Polisi halina nia ya kuwatesa wananchi wanapokamatwa na kuwekwa mahabusu.
Mbunge huyo alitaka kufahamu kauli ya Waziri Lugola kuhusu mahabusu kukosa chakula.
“Mahabusu wote wanapata chakula na wapo watu ambao wanapewa tenda hizi za kuleta vyakula kwa mahabusu”amesema na kuongeza kuwa, kuna wananchi wanaoruhusiwa kupeleka vyakula kwa mahabusu.
0 COMMENTS:
Post a Comment