September 3, 2018





NA SALEH ALLY
HIVI karibuni, Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alitembelea katika Ofisi za Global Group zilizopo Sinza Mori jijini Dar es Salaam.

Ndani ya ofisi hizo, imo Global Publishers Ltd inayochapisha magazeti mbalimbali yakiwemo ya michezo ya Spoti Xtra na Championi.

Hakika Dk Mwakyembe anastahili pongezi kutokana na uamuzi wake wa kufika na kujionea Global Publishers inavyofanya kazi. Alifika wakati ratiba yake ikiwa imembana sana.

Lakini baada ya kupata nafasi ya kutembelea katika ofisi zetu, alijionea mengi ambayo hakuwa ameyategemea kama ilivyo kwa watu wengi ambao huwa hawayatarajii kabla ya kufika.

Kati ya alivyozungumza baada ya kutembelea Global Group ni namna kazi zinavyofanyika kwa mpangilio, tunavyoweza kuwakuza vijana kutoka vyuoni na kadhalika.

Hivyo nirudie kumpongeza kwa kuwa alikuwa amebanwa sana lakini alitenga muda wake. Na wakati akiulizwa maswali kadhaa alizungumzia masuala mbalimbali yakiwemo kama Serikali ya Tanzania inaweza kutoa fedha michezoni.

Hakika kama ambavyo Dk Mwakyembe alikubali, michezo ni ajira, michezo ni afya na michezo ni burudani. Hivyo si jambo dogo linaloweza kufanyiwa mzaha.

Kwa miaka mingi sana michezo imekuwa ikionekana ni burudani, si lazima na mambo ya kawaida. Lakini katika nchi zetu wako wanaoishi kama wafalme kwa sababu ya michezo.

England ni kati ya nchi zinazoingiza kodi nyingi sana kupitia michezo. Jambo ambalo si vibaya kusema kwamba michezo haipaswi kudharauliwa tena.

Dk Mwakyembe amekuwa akijitahidi kuwasimamia wanamichezo, kuwa karibu nao na kujaribu kuweka mambo katika misingi sahihi. Lakini hata misingi ikiwa sahihi, basi fedha ni muhimu pia.

Fedha inaweza kutumika katika mambo mengi kama vile kusomesha wataalamu wa michezo husika katika nchi mbalimbali zilizopiga hatua.

Wataalamu wanaweza kuwa makocha, madaktari, watu wa mipango ya kifedha na kadhalika. Maana kama klabu itakuwa na wataalamu wa kiwango cha juu, lazima watakuwa msaada.

Serikali inapaswa kuisimamia michezo hata kama kuna vyama na mashirikisho. Ndani yake kumekuwa na mwendo wa kukimbia na kusimama ambao wakati mwingine si mzuri kwa afya ya michezo nchini.

Serikali inaweza isitoe fedha, lakini ikawasaidia wataalamu wa michezo baada ya kuwasiliana na wahusika sahihi kama mashirikisho au vyama fulani.

Watakaopelekwa baada ya mwaka au miaka miwili, watakaporejea waingizwe serikalini kukiwa na programu maalum kuusaidia mchezo fulani.

Kama kila mwaka watasomeshwa au kufundishwa mambo ya msingi ya jambo fulani, basi baada ya muda mchango wa elimu kwa wataalamu utaanza kuonekana kwa kuwa watakuwa wengi wamejifunza.

Hao ndiyo watakwenda wakiwainua wengine wasio na ufahamu wa mambo kadhaa. Baada ya miaka kadhaa, hii itakuwa msaada kwa jamii ya wanaopenda kushiriki mchezo fulani.

Wakati mwingine viongozi wa juu wa serikali wamekuwa hawashauriwi vizuri na wengi wao wamekuwa hawajui kuhusiana na jambo fulani kama michezo ina afya kwa taifa.

Serikali kama itaisimamia baadhi ya michezo, kuweka kambi ya timu za taifa au kuzijali zinaposafiri na ikiwezekana kuhoji mambo yanapoharibika, itasaidia sana. Pia kulisimamia suala la wachezaji vijana kwa karibu kabisa. Mambo yatabadilika sana.

Tuna vipaji vingi katika michezo na wenye nia ya kuviendeleza ni wachache sana. Wengi wa viongozi huingia wakilenga kujinufaisha wao.

Serikali ya awamu ya tano ikiamua kuwamaliza watu hao na kuhakikisha mambo yanakwenda sahihi ni mara moja na matunda yataanza kuonekana. Serikali inaweza ikiamua na ikifikia hapo itawakomboa wengi sana.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic