Na Mwandishi Wetu
Mgombea pekee wa nafasi ya urais wa Simba, Swedy Mkwabi kama akifanikiwa kushinda nafasi hiyo, basi ataanza kwa kupitia mikataba upya ya wadhamini huku akiahidi kusimamia vizuri mfumo wa mabadiliko ya uendeleshaji ya klabu hiyo kwa kufuata katiba ya mwaka 2018 iliyopitishwa na wanachama.
Kauli hiyo aliitoa jana kwenye ufunguzi wa kampeni zake zilizofanyika Southern Sun Hotel, Posta jijini Dar es Salaam huku akisindikizwa na wenyeviti wa matawi wa wilaya ya Dar.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Mkwabi alisema ataipitia mikataba hiyo ya wadhamini kwa ajili kuangalia kama kuna sehemu ya kuboreshwa, basi iboreshwe, hiyo yote katika kuhakikisha klabu hiyo inakuwa na vyanzo vingi vya fedha.
“Ninafahamu klabu ina wadhamini, hivyo baada ya kuingia madarakani nitahakikisha ninaipitia upya mikataba hiyo pamoja na kukutana na wadhamini kwa ajili ya kujadili baadhi ya vitu.
“Hicho ni kitu cha kwanza nitakachoanza nacho, pia nitahakikisha kunakuwepo na ushirikiano wa karibu kati ya uongozi wa makao makuu na uongozi wa matawi, wilaya na mikoa ili kuleta ufanisi na umoja ndani ya klabu ya Simba.
“Katika kuhakikisha kwamba maslahi ya wanachama wa Simbakatika Simba Sports Club Limited yanalindwa vizuri kwa kushirikiana na muwekezaji mkuu wa klabu ya Simba.
“Pia, nitaondoa makundi ya wanachama ndani ya klabu ya Simba kwa kutengeneza umoja wenye nguvu ndani ya Simba kwa kuifuata na kuheshimu katiba ya klabu,”alisema Mkwabi mwenye Stashahada ya juu ya Biashara na Utawala Chuo ya CBE.
0 COMMENTS:
Post a Comment