MSIMU wa pili wa tamthilia ya vichekesho maarufu vya Mwantumu ambayo huonyeshwa na Chaneli ya Maisha Magic Bongo kupitia King’amuzi cha DStv, umezinduliwa rasmi leo Jumatatu na kesho Jumanne itaanza kuonyeshwa katika chaneli hiyo namba 160.
Vichekesho hivyo ambavyo vinaongozwa na mchekeshaji maarufu nchini, Lucas Mhavile ‘Joti’, kwa msimu huu wa pili amevaa uhusika wa watu watatu ambao ni Mzee Mrisho, Kaboba na Mwantumu Sahare.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Masoko wa Multichoice Tanzania, Alpha Mria, amesema tangu kuanza kwa msimu wa kwanza wa vichekesho hivyo Oktoba mwaka jana, vimekuwa na msisimko mkubwa na vimepokelewa vizuri na watazamaji wote.
“DStv kupitia chaneli yake pendwa ya Maisha Magic Bongo, siku zote imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha tunatoa msisitizo kwenye maudhui ya ndani na vichekesho hivi vya Mwantumu ni mfano halisi. Hii ni yetu na imetengenezwa hapa Tanzania na wazalishaji, waandaaji na waigizaji wote ni wa hapa nchini,” alisema Mria.
Mria aliongeza kuwa, katika msimu wa kwanza, vichekesho hivyo vilikuwa vikionyeshwa mara moja kwa wiki, lakini sasa vitakuwa vikionyeshwa mara mbili kwa wiki yaani Jumanne na Jumatano kuanzia saa 1:30 usiku.
Naye Joti amezungumzia msimu huo wa pili wa Mwantumu kwa kusema: “Mwantumu imenitoa kule ambapo watu walikuwa wananijua nilipo na kunileta huku.
“Wameniongezea kitu ambacho sikutegemea kwa sababu niliruhusu wanitumie na wao wakaona kitu cha ziada wakanitumia vilivyo, kwenye uhusika wa safari hii imeongezeka ya mzee, nimefurahi sana kwa sababu ni kitu kipya na inaniongezea uwezo mkubwa sana.”
Baadhi ya waigizaji maarufu ambao watakuwepo katika msimu huu wa pili ni Mzee Fungafunga ‘Mzee Mwalubadu’, Mama Abdul ‘Mwantumu Mcharuko’ na Alex Wasponga ‘Kayombo’.









0 COMMENTS:
Post a Comment