Simba imeamsha makali yake jana baada ya kuichapa African Lyon ya Dar es Salaam mabao 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara uliofanyika Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
Kwa ushindi huo, Simba SC inafikisha pointi 14 baada ya kucheza mechi saba, ikijivuta hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu, nyuma ya Azam FC pointi 15 za mechi saba, Singida United pointi 16 mechi tisa na Mtibwa Sugar pointi 17 mechi tisa.
Ushindi wa jana wa Simba umetokana na mabao ya kiungo mzalendo, Shiza Ramachani Kichuya kipindi cha kwanza na mshambuliaji wake Mganda, Emmanuel Okwi kipindi cha pili, wakati bao la Lyon limefungwa na Awadh Juma dakika ya 62.
Kichuya ambaye ameporomoka kiasi cha kuachwa timu ya taifa, leo aliamsha makali yake kwa kufunga bao la kwanza mapema tu dakika ya 9 akimalizia krosi ya beki wa kulia, Shomari Kapombe.
0 COMMENTS:
Post a Comment