November 17, 2018


Bodi ya Udhamini ya Simba Sports Club Limited iliyo chini ya mfadhili wao bilionea, Mohammed Dewji ‘MO’ ipo kwenye hatua za mwisho za kumtangaza Selemani Matola kuwa mbadala wa Mrundi, Masoud Djuma.

Hiyo, ikiwa ni siku chache tangu bodi hiyo ilipokutana na uongozi mpya ulioingia madarakani wiki moja iliyopita baada ya kufanya uchaguzi wa wajumbe na mwenyekiti wao mpya ambaye ni Swedy Mkwabi.

Simba ipo njiani kumleta mbadala huyo wa Djuma baada ya kutokea kutoelewana kati yake na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mbelgiji, Patrick Aussems kabla ya kusitishiwa mkataba wake na kurudi Rwanda.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumamosi, zoezi la kumpata msaidizi wa Djuma lipo chini ya Ofisa Mtendaji Mkuu (C.E.O) mpya wa klabu hiyo, Crescentius Magori na kocha Aussems ambao tayari wamekutana kujadiliana masuala ya usajili pamoja na kocha msaidizi.

Mtoa taarifa huyo alisema, kwa upande wa bodi hiyo mpya, wenyewe tayari wamelipitisha jina la Matola na kilichobaki ni kwa kocha huyo kukabidhiwa jina hilo kabla ya kutoa maamuzi yake.

“Kocha alitoa mapendekezo ya kuomba msaidizi wake atakayeweza kufanya naye kazi na yeye mwenyewe aliomba apatiwe mzawa.

“Kama bodi iliweka majina kadhaa na kuyajadili, kwa pamoja tulipitisha jina la Matola baada ya wajumbe wote kuvutiwa na uwezo wake wa kufundisha.

“Hivyo, kilichobakia ni kukutana na kocha kusikia maoni yake kabla ya kumtangaza Matola kuwa ni kocha msaidizi wa Simba,” alisema mtoa taarifa huyo.

Kwa upande wa Matola alipotafutwa kuzungumzia hilo alisema kuwa: “Mimi siyo msemaji wa hili, nafikiri hilo wanaloweza kulizungumzia ni Simba pekee, sijapata rasmi taarifa za kunihitaji.

“Lakini mkataba wangu unaniruhusu kuondoka Lipuli FC kama wakinihitaji, kikubwa wafuate kanuni na utaratibu kama unavyofahamu mimi bado ni kocha wa Lipuli mwenye mkataba.”

Kwa upande wa Simba, Mkwabi alisema: “Hilo suala halipo mikononi mwangu, lipo kwa Magori ambaye yeye hivi karibuni alitarajiwa kukutana na kocha kujadiliana masuala mbalimbali likiwemo hilo la kocha msaidizi na usajili.”

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic