Straika wa Azam FC, Donald Ngoma, raia wa Zimbabwe, jana Jumapili aliifungia timu yake hiyo na kuipa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.
Ngoma alifunga bao hilo dakika ya 40, lakini ilipofika dakika ya 90, alitolewa uwanjani kwa kuonyeshwa kadi nyekundu kwa utovu wa nidhamu na kuwafanya Azam kumaliza mchezo huo wakiwa pungufu.
Ngoma ambaye aliwahi kung'ara na Yanga, anasifika kuwa mmoja wa washambulizi wazuri lakini wenye tabia ya utukutu.
Hii ni kadi ya pili nyekundu Azam FC wanaipata kwenye mechi zao za msimu huu, ya kwanza waliipata walipoibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKT Tanzania ambapo ilikwenda kwa Enock Atta Agyei raia wa Ghana.
Kwa ushindi huo, Azam imeendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ikiwa imejikusanyia pointi 30 baada ya kucheza mechi 12, imeshinda tisa na sare tatu. Bado haijapoteza hata mechi moja na hii ni mechi ya kumi haijaruhusu bao. Imefunga mabao 15, imeruhusu mawili.
0 COMMENTS:
Post a Comment