November 5, 2018






NA SALEH ALLY
BADO Tanzania inahitaji idadi kubwa ya wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi yetu, Tanzania.

Wachezaji wengi wa kulipwa nje ya nyumbani watakuwa chachu ya mabadiliko mengi sana na raha tumeanza kuyaona mengi.

Wanaocheza nje wamekuwa ni chachu ya mabadiliko ya soka katika nchi nyingi na mfano mzuri Kenya na Uganda.

Uganda wamepiga hatua kubwa hata katika ubora wa viwango chini ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa). Leo ndiyo nchi bora zaidi Afrika Mashariki na Kati lakini wenye ligi dhaifu.

Ubora wao unatokana na mafanikio ya kikosi cha timu ya taifa ambacho kwa kweli kwa ukanda wetu, wana kikosi kizuri zaidi na kinategemea wachezaji wanaocheza nje ya Uganda, akiwemo Emmanuel Okwi na Juuko Murshid ambao wanacheza Ligi Kuu Tanzania Bara.

Pamoja na hivyo, hapa kwetu tumeanza kuona faida ya Mbwana Samatta aliye Ubelgiji lakini hata kubadilika kwa maisha ya wachezaji kama Thomas Ulimwengu, Saimon Msuva, Himid Mao, Abdi Banda na wengine kwa mengi kama aina ya uzungumzaji, namna ya kuishi na hata kipato.

Kama bado wangekuwa hapa nyumbani, yote haya wasingekuwa nayo hata kidogo. Ajabu, baadhi wamekuwa wakiumizwa sana na mashabiki wa soka walio nyumbani, wakisema wanawakatisha tamaa.

Wachezaji watatu nilizungumza nao kwa nyakati tofauti, walinieleza namna walivyokuwa wakijitahidi kuwapuuzia mashabiki wasio waelewa lakini wakanieleza wanavyojisikia vibaya kuona wanaungwa mkono huko nje waliko na kupuuziwa nyumbani.

Kwa mwanadamu yeyote, lazima hilo litamuuma kwa kuwa kila mmoja hutamani au kutegemea kuona unaungwa mkono nyumbani.

Kibaya zaidi huku imekuwa tofauti kwa kuwa Watanzania wasiojua uhalisia wa mambo wengi hawapendi kujifunza na kitu kibaya zaidi tumepewa kama laana, kuamini kulaumu tu ndiyo jambo pekee ambalo ni sahihi. Kwani hata wanaolaumu, wao hawana walilofanya au kujaribu.

Wakati mwingine unaweza kupongeza na kukosoa kwa mlango sahihi wa ujenzi kwa kuwa kama mchezaji wa timu fulani amekosea na unaiunga mkono, amini alitaka kufanya vema mambo yakamshinda.

Tanzania ndiyo imeanza kuwa na wachezaji wanaotoka, kuamini wao kwa kuwa wanacheza nje ya nchi basi watakuwa kama malaika ni kuthibitisha ulimbukeni wetu. Wao wanabaki kuwa watu kama kawaida lakini bado tuamini wanaumia na wanastahili kupewa moyo na kuungwa mkono.

Waliokosea wakijaribu, wapewe moyo. Waambiwe kosa lao na kushauriwa kupambana zaidi. Haujawahi hata kumpongeza, haujawahi hata kumshauri au hakukosea hata mara moja, alipokosea mara ya kwanza, basi lawama utafikiri ndiyo mwisho wa kuishi, kweli mashabiki wa namna hii wanakera sana.

Wachezaji walioonekana kuumizwa na mashabiki nikawashauri wakati mwingine wanaweza kuacha kuwasikiliza kabisa kwa kuwa maneno yao yanawaumiza na hasa kama wanaona hawana sababu za msingi.

Pia nikawashauri wanaweza kuwasikiliza wale wanaowapa maneno ya msingi, hata kama wanalaumu lakini wana hoja jenzi. Basi wachukue hata kama inaumiza, basi waifanyie kazi.

Kuna mashabiki wengi sana wa soka ambao ni waelewa na wanaujua mpira wanaoushabikia. Wanaweza kuwa msaada kutokana na kuwa na maoni chanya na si maoni “mikito” yanayowakatisha tamaa wachezaji wanaoamini Tanzania ni nyumbani na mashabiki kutoka nchini mwao ni mashabiki “ndugu”.

Kwa kifupi, kuwapuuza wasiojua na wanaolaumu pekee ni kuonyesha ni “profesheno”. Maana unatumia muda mwingi kuwekeza katika kazi yako kwa ajili ya maisha yako na taifa lako.

Wako wengine hukosoa wakiumizwa na maendeleo ya wachezaji fulani au ushabiki wa kijinga. Hivyo kuyasikiliza yote wanayosema, ni kujiumiza kichwa bila sababu ya msingi.

Nanyi, jifunzeni kuamini wachezaji ni binadamu kama nyie na si malaika. Kosoeni mjenge, si kukosoa muonekane mnajua sana. Kuwavunja nguvu askari wako ni kujiangamiza kwa mikono yako mwenyewe.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic