Uongozi wa timu ya Manispaa ya Kinondoni KMC umeachana rasmi na mchezaji wake Abdulahim Humud kwa kile walichoeleza kuwa ni makosa ya utomvu wa nidhamu kwa kuwashawishi wake wa wachezaji wenzake ili awe nao kwenye mahusiano.
Humud aliongeza mkataba na KMC kwa muda wa mwaka mmoja baada ya kuisaidia kupanda Lugi Kuu baada ya kufunga bao la ushindi kwenye Ligi Daraja la Kwanza dhidi ya JKT Mlale na ameitumikia timu kwa muda wa usiozidi miezi minne.
Kaimu Katibu Mkuu wa KMC, Walter Harson amesema kuwa wamefikia hatua hiyo baada ya mchezaji huyo kuwa na vitendo visivyo vya kinidhamu kwa kutaka kuanzisha mahusiano na wapenzi wa wachezaji, kusahau vifaa vya michezo Dar es Salaam walipokwenda Tanga kucheza na Coastal Union.
"Wachezaji wakiwa kambini amekuwa akichukua namba za simu za wapenzi wao na kuanza kuwasiliana nao kwa kuwashawishi wavunje uhusiano nao, pia amekuwa akimshawishi mke wa mchezaji mwingine ambaye hakuwa kambini kwa kumtaka kuwa naye kimahusiano, ushahidi uliletwa na tukakaa kumuonya akaomba msamaha.
"Uongozi ulikaa na kamati ya nidhamu, tukamuuliza mwalimu kama ana mhitaji akasema bado ana takiwa ndani ya kikosi, kabla hatujampa barua kumrudisha kambini aliandika barua ya kuacha kazi mwenyewe hivyo tumempa ruhusa, tutakaa na wanasheria ili tuangalie namna ya yeye kuweza kulipa gharama zetu kwa kuwa hajamaliza mkataba wetu," alisema
Kwa upande wa Humud alisema kuwa anasikitishwa na taarifa hizo zinazotolewa kwakwe na kuutaka uongozi kueleza ukweli na sio kupindisha kwani anajua mambo mengi kutokana na muda aliokaa na timu tangu kuipandisha daraja.
"Uongozi unabidi uongee ukweli kwa sababu niliomba kuachana na timu muda mrefu baada ya kuona napokea mshahara bila kufanya kazi, kuhusu madai ya kuwataka wake za watu hilo halina ukweli kwa kuwa nina mke mzuri kuliko wachezaji wote.
"Kuna mambo mengi ambayo yanatokea kwetu ila niliamua kutumia busara kukaa kimya sikuongea na kama watataka niongee nitafanya hivyo, mpira kwangu ni ajira hivyo siwezi kukubali kupoteza uwezo wangu kwa kukaa mahali ambapo sipewi nafasi.
Nilikuwa Afrika kusini nimerudi, hivyo kama wanahitaji niwarudishie gharama zao nipo tayari ila nao inabidi wawe tayari kusema ukweli," alisema.
0 COMMENTS:
Post a Comment