Mbinu anazozitumia Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems kuwamaliza wapinzani wake katika kipindi cha pili, zimevuja.
Mbinu hizo zimevuja ikiwa ni baada ya Simba kuifunga Ruvu Shooting mabao 5-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar, Jumapili iliyopita.
Mara kadhaa, Simba imekuwa ikicheza vizuri sana kipindi cha pili na hiyo ni baada ya Aussems kuzisoma mbinu za wapinzani wao na kuzifanyia kazi wakati wa mapumziko.
Katika mchezo dhidi ya Ruvu, kipindi cha kwanza kilimalizika kwa Simba kuwa mbele kwa mabao 2-0, hali ya hewa ilibadilika zaidi kipindi cha pili na timu hiyo kufunga mabao mengine matatu kuhitimisha idadi hiyo ya mabao matano, hata hivyo uongozi wa Simba ulifanya kosa baada ya kuzisahau mbinu za kocha huyo vyumbani.
Aussems raia wa Ubelgiji, wakati wa mapumziko aliamua kuwachorea vijana wake namna ya wapinzani wao walivyojipanga na wanavyocheza, kisha akawapa mbinu za kuwazuia wasiweze kuleta madhara golini kwao.
Aussems aligundua mapema kuwa, washambuliaji wa Ruvu Shooting, Said Dilunga na Fully Maganga ndiyo wanategemewa zaidi, pamoja na viungo wao Willium Patrick, Zuberi Dabi na Shaban Usala.
Katika mchoro huo ambao gazeti la Championi iliukuta kwenye chumba cha kubadilishia nguo cha Simba, unaonyesha kuwa, Said Dilunga, alitakiwa kukabwa na mabeki wawili ambao ni Juuko Murshid na Pascal Wawa.
Fully Maganga, hakutakiwa kukabwa na mtu, bali Mzungu huyo aliwaambia vijana wake wamuache acheze kati ya viungo na mabeki ili iwe ngumu kwake kupata mipira na kweli hakuwa akipata mipira mingi kama ilivyokuwa kipindi cha kwanza.
Kwa upande wa Willium Patrick, Zuberi Dabi na Shaban Usala, waliwekewa watu makini kama Claytous Chama, Shiza Kichuya, Jonas Mkude na wakati mwingine Emmanuel Okwi alikuwa anakuja kuwasaidia, huku John Bocco na Meddie Kagere wakiachwa mbele.
Shomary Kapombe aliyekuwa akicheza beki wa kulia na beki wa kushoto akiwa Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, walibaki wakiwa huru kufanya wanavyotaka ndiyo maana muda mwingi walikuwa wakishambulia sana.
Baada ya nyota hao kuzuiliwa vilivyo, baadaye Kocha wa Ruvu Shooting, Abdulmutik Haji, aliamua kumtoa Patrick, Dilunga na Maganga, hata hivyo, nafasi zao zilivyochukuliwa na wengine, hawakuweza kubadili matokeo.
- CHANZO: CHAMPIONI








0 COMMENTS:
Post a Comment