Licha ya mbwembwe zake na uzoefu wake, Kocha wa Mbabane Swallows ya Swaziland, Thabo ‘Koki’ Vilakati akisikia jina la Mohammed Dewji ‘Mo’ na Emmanuel Okwi wa Simba anashtuka paap!
Kocha huyo mzawa anayesifika kwa staili ya uchezaji ya 4-3-2-1 na uwezo mkubwa wa kuhamasisha, timu yake itacheza na Simba Novemba 27 jijini Dar es Salaam katika mechi ya kwanza ya hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mbabane ambayo ni timu ya zamani ya Papy Tshishimbi wa Yanga na Asante Kwasi wa Simba, iliwaondoa Azam kwenye Kombe la Shirikisho msimu uliopita. Kama Simba ikiwaondoa Mbabane itaingia raundi ya kwanza kucheza na mshindi kati ya Nkana ya Zambia na UD Songo ya Msumbiji.
Thabo ambaye amekimbiwa na wachezaji kadhaa nyota waliokwenda kusaka masilahi nje, amezungumza na Championi Jumatano na kusema kwamba anajua mambo kadhaa kuhusiana na Simba lakini tishio kubwa akataja ni ufundi wa Okwi na uwekezaji wa Mo.
Anasema kuwa anaelewa kuna mabadiliko makubwa Simba ambayo yametokana na uwekezaji wa Mo ambaye ana shauku ya mabadiliko na amefuatilia na kugundua anataka kufanya sapraizi msimu huu.
Kocha huyo ambaye yupo klabuni hapo tangu msimu wa 2016, ameweka wazi kwamba mchezaji anayemuumiza sana kichwa ni Okwi ambaye amekuwa kwenye fomu muda mrefu huku akimtaja kama mchezaji asiyekubali kushindwa.
Lakini akadadisi kujua nini kimemtokea au wapi alipo winga machachari ndani ya Simba, Shiza Kichuya kama ilivyokuwa msimu uliopita.
Tunawafahamu. Tunajua nini wanafanya na kila kitu kinachoendelea kwao tumekuwa tukikifahamu.
“Tunafahamu kuwa Simba ni timu kubwa Afrika, na inatupa hofu zaidi sasa kwa kuwa ina mwekezaji bilionea Afrika, Mohammed Dewji, huyu amewekeza fedha nyingi na ni mtu maarufu sana.
“Tunafahamu anataka mafanikio makubwa kwenye timu yake, hivyo watakuja kamili sana, lakini pia Simba wanaye mmoja kati ya wachezaji mahiri Afrika Mashariki, Emmanuel Okwi, huyu kila mtu anaujua uwezo wake, hivyo lazima tuwe makini tunapocheza nao.
“Ila jambo moja ambalo sijaelewa ni kwamba walikuwa na winga wao wa msimu uliopita (Shiza Kichuya) huyu alikuwa hatari sana lakini sasa haonekani, hivi yupo?” alisema kocha huyo mwenye mbwembwe nyingi.
Mpaka sasa kwenye ligi ya ndani, Mbabane wamecheza mechi nane na wako kwenye nafasi ya nne na pointi zao 16. Wameshapoteza mechi mbili, wakati msimu uliopita walitwaa ubingwa bila kupoteza mchezo hata mmoja zaidi ya sare tisa kwenye michezo 26 kwani ligi yao ina timu 14.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Swedy Mkwabi wanachoangalia ni kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa tu na si vinginevyo na tayari wameanza kusaka video za Mbabane.
CHANZO: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment