November 19, 2018



NA SALEH ALLY
SAFU ya uongozi wa Simba utakaoongoza kwa mfumo mpya wa mabadiliko imekamilika na kwa hali ilivyo, utaona hakuna mjadala kwamba ni watu wasio na uwezo wa kuifikisha Simba inapotaka kwenda.


Upande wa mwekezaji na ule wa klabu utaunganisha nguvu kuwa moja kama kauli mbiu ya Simba ya “Nguvu Moja” inavyosema, baada ya hapo litafuatia suala kupambana kwa ajili ya maendeleo.


Watu nane kutoka upande wa klabu na tisa kutoka upande wa klabu, unafanya wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi kuwa 17 tayari kuitetea Simba.


Ukiangalia watu walio ndani ya bodi hiyo, wengi wameishakuwa ndani ya Simba na kupata sifa kubwa ya mafanikio kwa maana ya Simba kufanya vizuri.




Lakini kuna wale watu ambao hawakuwa viongozi wa Simba kwa maana ya kuchaguliwa lakini mara nyingi wakawa msaada mkubwa.

Watu mfano wa Musleh Al Rawahi, huyu amekuwa mwanachama na shabiki wa Simba aliyejitolea mara lukuki akiwa nje ya uongozi wa Simba.



Imekuwa ni vigumu hata kujua kama amejitolea hadi ulipofanyika uchunguzi mkubwa kujua nini kimefanyika.

Mfano mzuri wakati ule alipojitolea gari kumpa kiungo wa Simba, Ramadhani Singano ‘Messi’. Lengo lake likiwa ni kuzidi kumhamasisha kwa kuwa alimzawadia gari la kufanya biashara ya kubeba mizigo ili awe anaingiza kipato zaidi.

Musleh amekuwa akiendelea kufanya hivyo kimyakimya, akionyesha wazi ana nia ya kuona Simba inakwenda bila ya kutaka hata kujulikana. Watu kama hao wana nafasi kubwa sana ya kuwa msaada kwa klabu hii kwa kipindi hiki ambacho ni kigumu.

Nasema kigumu tofauti na wengi wanavyoamini ni kipindi rahisi, la hasha. Simba itaendeshwa kwa mfumo tofauti, mfumo mgeni ambao unahitaji ufundi, ubunifu, usikivu na masikilizano ya hali ya juu.

Kama hakutakuwa na hali hiyo, badala ya kujenga Simba wanaweza kujikuta wanaharibu. Maana yake nini? Walio ndani ya uongozi lazima wakubali kujifunza na kuingia ndani ya mfumo mpya kwa ajili ya kuleta mabadiliko na baadaye mafanikio.

Wako wengi ndani ya Simba ambao wamefanya vema, mfano tunajua mafanikio ya Kassim Dewji akiwa Katibu Mwenezi na baadaye Katibu Mkuu wa Simba. Zacharia Hans Poppe, kati ya wale waliojitolea sana na kufanya mambo kwa kuipigania Simba na kadhalika.

Mwenyekiti kijana wa Simba, Swedy Mkwabi ambaye pia atalazimika kukubali kujifunza na wakubwa au wakongwe nao watalazimika kumsikiliza ili mambo kwenda kwa usahihi.


Angalia kuna Asha Baraka, anajua maana ya uongozi na kuongoza watu, Profesa Mohamed Janabi na wengine ambao wapo na watalaamu wa masoko na kadhalika. Kwa uhakika watu hawa wamekamilika lakini suala la utekelezaji ndilo linalobaki mbele yao na lazima walitambue suala la dhamana.


Hawa wanaingia katika pande hizi mbili za bodi bila ya kujali wanatokea wapi. Mwisho ni kuangalia mafanikio ya Simba na njia sahihi ya kupita.


Kupishana hoja au mawazo ni jambo sahihi kwa wanaojielewa, lakini kuna kila sababu ya wahusika wote 17 kujua yale ambayo nimeyasema na suala la kuvumiliana hapa linachukua nafasi kubwa.

Simba sasa iko mikononi mwa watu hawa 17 ambao watatakiwa kuwa makini sana wakijua dhamana waliyokabidhiwa ni kubwa na muhimu.

Kusiwe na hisia za mimi wa huku au yule wa kule, kama wako wajumbe wakiamini hivyo, basi safari ya Simba itakuwa ya mwendo wa kobe na hata ule wa kinyonga wa kudunda mbele na nyuma.

Lazima Simba isonge mbele kwenda kwenye mafanikio na lazima wahusika waliopewa dhamana wajue wanaaminika na wahakikishe maslahi yanakuwa ya Simba na si Simba Klabu au Simba Mwekezaji. 

Kama Simba itafanya vema, itakuwa chachu ya klabu nyingine kuamini kilichofanyika ni sahihi na huenda ikachangia mabadiliko ya baadaye. 


UPANDE WA KLABU:
1. Swedy Mkwabi
2. Salim Abdallah
3. Hassan Kipusi
4. Hussein Milinga
5. Zawadi Kadunda
6. Asha Baraka
7. Mwina Kaduguda
8. Seleman Said


UPANDE WA MWEKEZAJI:
1. Mohamed Dewji (Mwenyekiti wa Bodi)
2. Zacharia Hans Poppe
3. Octavian Mshiu
4. Musleh Al Rawahi
5. Prof Mohamed Janabi
6. Barbara Gonzalez
7.  Mulamu Nghambi
8. Kassim Dewji
9. Mohamed Nassor


1 COMMENTS:

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic