November 19, 2018




NA SALEH ALLY
MAUMIVU ni makubwa sana, hakika ni  jambo ambalo linaumiza moyo kwa kiwango cha juu, lakini sitaki kuingia katika kundi la wale wanaoamini kulaumu ndio mafanikio.

Kipigo cha bao 1-0 walichokipata Taifa Stars kutoka kwa Lesotho tena kwa bao “mlendamlenda” hakika inaumiza hata kufikiria.

Jambo hili linaumiza hasa kama ulitaka kuona Taifa Stars inafuzu na kucheza Afcon kwa mara ya pili katika historia ya nchi yetu.

Asilimia 80 ya wanaopenda soka hawakuwahi kuiona Tanzania ikicheza Afcon, nafasi yetu ilikuwa jana kwa kuwa timu tulikuwa tukicheza nayo tunaimudu kabisa.

Kwa wale walioishuhudia Taifa Stars ikicheza dhidi ya Lesotho watakubaliana nami kwamba mpira ulikuwa kwetu na kazi ilikuwa ni kumaliza tu.

Hali ilivyokuwa, tungeweza kufanya tunachotaka lakini mwisho mambo yamekwenda katika mwendo ambao haukutarajiwa.

Washambuliaji waliopewa nafasi wamejitahidi lakini lazima tutakubali kwamba walikuwa na papara zisizokuwa na sababu.

Kipindi cha kwanza, utaona Lesotho walimiki mpira vizuri zaidi yetu na mashambulizi machache lakini makali. Sisi pia tulifanya mashambulizi kadhaa ambayo kama tungekuwa makini tungeweza kufanya vizuri.

Utaona Kocha Emmanuel Amunike alipanga wachezaji wengi zaidi wa ulinzi kama vile kumchezesha Mudathir Yahaya katika kiungo cha ushambulizi. Ni mfumo wa ugenini kutaka kusaidia ulinzi lakini bado tulihitaji mapema kushambulia zaidi kupata mabao.

Bado naweza kusema Mudathir alijitahidi sana kadiri ya uwezo wake hadi anatoka. Lakini bado Stars ilihitaji ubunifu zaidi na suala la kumficha Saimon Msuva acheze namba 10, kwangu niliona lilikuwa na shida na huenda angetokea pembeni angeweza kuwa na madhara zaidi.

Wako ambao wanasukuma lawama kwa kipa Aishi Manula, kwamba alipangua mpira ambao ulibaki langoni. Kawaida, mpira anapoucheza kipa, unakuwa umerudi mchezoni na kila mmoja anatakiwa kushiriki.

Baada ya Manula kuupandisha mpira ule juu, nani aliruka na mchezaji wa Lesotho aliyepiga kichwa? Waliokuwepo langoni vipi walishindwa kuokoa? Jibu la mwisho hili kosa halitamalizwa kwa kulaumiana kwa kuwa tu tuna nafasi ya kurekebisha kosa.

Taifa Stars ina nafasi ya mwisho kujifunza kupitia mechi ya jana kwamba kufunga kusiwe kama sehemu ya kujaribu na badala yake ni kufanya hasa kinachotakiwa.

Ukipata nafasi funga, ukiwa unaweza kufanya fanya kweli. Waliokosea jana ni wengi na wengine walirekebisha kwa ajili ya wenzao lakini mwisho imekuwa kilichotokea.

Sasa Lesotho ana pointi tano kama Stars, Cape Verde naye ana nne na kila timu kati ya hizi ina nafasi ya kufuzu.

Stars inamalizia nyumbani dhidi ya Uganda na kinachotakiwa ni kushinda tu, sasa dua itakuwa kubwa zaidi kwa Lesotho ifungwe na Cape Verde, jambo ambalo ninaamini Cape Verde hawatawaacha.

Kama itatokea hivyo, tukashinda dhidi ya Uganda, basi inawezekana tukavuka kwa kuwa Cape Verde wakishinda, watakuwa na pointi saba. Kama watapoteza, basi Lesotho watalingana pointi na sisi na tutaanza mahesabu.

Kizuri kabisa kwa Stars ni kushinda dhidi ya Uganda na baada ya hapo kuanza kale kamchezo kabaya ka kuomba watoke sare Lesotho na Cape Verde.

Nafasi bado ipo na kuna uwezo wa kuuvunja ukuta wa miaka 38 sasa bila kucheza Afcon. Kikubwa ni Taifa Stars kujipanga dhidi ya Uganda na wale walioumia hasa wachezaji, ninaamini watakuwa wanajua wanatakiwa kufanya nini.

Tulitakiwa tushinde, ninaamini nao walipania tushinde lakini imeshindikana. Hili ni jambo baya kulishuhudia lakini chondechonde Watanzania, huu si wakati wa kuivunja timu moyo. Tuache wamalize kazi kwanza kwa kuwa wako vitani.

Kama tutaanza kuwashambulia wachezaji kipindi hiki, tutajitoa mchezoni wenyewe hata kabla ya karata ya mwisho. Tunaweza kuendelea kukosoa kwa nia ya kujenga badala ya kushambulia tukisubiri matokeo ya mwisho ambayo kama tutawaunga mkono tena, huenda tukasahau yaliyotokea jana.


3 COMMENTS:

  1. Weengi wamekosoa kwa nia ya kujenga, hususan upangaj wa kikosi, hata mechi vs Capezverde Taifa, ushindi ule ni matokeo ya kukosoa upangaji wa Team away, jana imejirudia tena!

    ReplyDelete
  2. Mwandishi hakuna Mtanzania anayelaumu mchezaji bali watanzania wanalaumu kocha ambaye naona katika makala hii kwangu ni kama umejaribu kumtetea,ukweli utabaki nafasi ya kiungo ilipwaya na tuna wachezaji ambao wangeweza kuifanya kuwa imara(Mkude na FeiToto),pia beki za pembeni kulia na kushoto aliwatoa wapi,waliruhusu mashambulizi most of the time kutokana na uwezo wao mdogo,bado katika hili pia tulikuwa na wachezaji wazuri wa kumudu hizo nafasi.

    ReplyDelete
  3. Lawama anazistahili Kocha kwa upande wangu, na hata watanzania wengi sijapata tafsiri ya mtu yeyote aliyewakosoa wachezaji, ila wengi wamelaumu na upangaji wa kikosi uliofanywa na kocha. Kiujumla kwa matokeo ya jana KOCHA ametufanya tustahili kuyapata vile. Hatukatai kupanga kikosi kama alivyopanga, tunachukulia kwamba wale ndio walianza, lakini alikuwa na uwezo pia wa kufanya SUB mapema baada ya kuona tumepwaya kwenye kiungo na beki za kulia na kushoto. Lakini aliamua kuacha hivyo, mpaka dkk za 82 na 92 ndo anafanya mabadiliko! Unadhani nani alaumiwe kama sio Kocha?

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic