Na Saleh Ally
WACHEZAJI wengi sana wameamua kuachana na mpira katika kipindi ambacho hawakutarajia au hawakuwa wakitaka kufanya hivyo kutokana na mambo kadhaa.
Kutotaka kuacha mpira kwao, kunaweza kukawa kunatokana na mambo kadhaa lakini zaidi ni kwa kuwa wanaona umri bado unawaruhusu, uwezo wao bado ni mkubwa na kadhalika.
Majeraha huwa yanaamua yanavyotaka, yanaamua bila ya taarifa na mchezaji anajikuta anapangiwa tofauti na namna alivyopanga au alichokuwa anataka kukifanya.
Majeraha yanayotesa mioyo ya wachezaji yanapatikana kwa aina mbili tofauti. Moja ni kutokana na miundombinu na pili ni kutokana na wao wachezaji kutofuata misingi sahihi ya mchezo husika.
Kwa nchi zilizoendelea, suala la majeraha kuhusiana na miundombinu unaweza kusema ni hadi asilimia tano tu. Kwa asilimia kubwa hasa kwa madaraja ya juu, kunakuwa hakuna tatizo hilo.
Zaidi ni kwa nchi zilizo na miundombinu duni kama Tanzania ambayo inasababisha wachezaji wengi kuumia. Mfano mzuri ni kama viwanja hakika ni vibovu wakati wa mechi zenye ushindani zimekuwa zikiwasababishia majeraha.
Mfano, mechi katika viwanja vingi vya mikoani zimekuwa ngumu kwa wachezaji wengi kwa kuwa zinawasababishia majeraha hayo na kuwapa wakati mgumu.
Pili ni weledi. Wachezaji wanajua wanatakiwa kufanya nini na hasa wakati wa kipindi cha mashindano. Mfano ligi inaendelea na kadhalika. Wengi wao wamekuwa wakishindwa kuwa wavumilivu katika mambo kadhaa hasa yale ya starehe.
Mfano, wachezaji wanatakiwa kujiepusha na masuala ya starehe na hasa ngono. Kuna kiwango ambacho mchezaji anaruhusiwa kufanya kulingana na wakati.
Pamoja na hayo, bado kuna suala la kuumia kwa wachezaji wenyewe, inawezekana kugongana au kukanyagana, hili linakuwa ni la kimchezo zaidi.
Pamoja na hivyo, kuna suala la kupumzika ambalo pia limekuwa mtihani kwao kutokana na urafiki wao na starehe hivyo wanasababisha hata majeraha kuwa rafiki kwao.
Majeraha yanawalazimisha wachezaji kadhaa wenye uwezo kukaa nje hata mwezi au zaidi. Hii imekuwa ikitengeneza presha kubwa kwao kwa maana ya suala la nafasi hasa kama timu ina ushindani.
Wanajua wakikaa nje, nafasi inachukuliwa kwa kuwa timu lazima iendelee kucheza. Pia wanajua watakaporejea mambo yanakuwa magumu kwa kuwa wanalazimika kufanya kazi ya ziada tena kupata nafasi hizo.
Hivyo, majeraha ni adui mkubwa wa wachezaji, wakiwa wamejitakia au kusababishiwa.
Papy Tshishimbi (Yanga)
Amekaa nje kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa kutokana na maumivu ya goti. Kiungo huyo raia wa DR Congo amekuwa na wakati mgumu tokea kutua kwa Kocha Mwinyi Zahera kutoka DR Congo ambaye amekuwa akimsisitiza kufuata maelekezo.
Suala la majeraha nalo limeongeza ugumu kwake lakini kuna taarifa kwamba tayari ameanza mazoezi akijiandaa kurejea.
Shomari Kapombe (Simba)
Amelazimika kupata matibabu nchini Afrika Kusini kutokana na maumivu makali ya enka aliyoumia akiwa kambini timu ya taifa.
Pamoja na kiwango chake bora, Kapombe amekuwa akikumbana na majeraha ya mara kwa mara jambo linalomfanya kuwa si mchezaji wa kuaminika sana.
Stamili Mbonde (Mtibwa)
Unapozungumzia mafowadi wa kati wenye miili sahihi, Stamili ni namba moja katika Ligi Kuu Bara. Mtibwa wanamtumia kuwazuia mabeki wawili wa timu pinzani wasiondoke. Sasa naye amekuwa mtazamaji ingawa imeelezwa anarejea.
Frank Domayo (Azam FC)
Goti limekuwa likimpa wakati mgumu Domayo ambaye pia aliwahi kulalamikia kifundo cha mguu. Kila anaporejea, anaonyesha uwezo kwa kiwango cha juu na kuwa msaada mkubwa katika timu yake. Majeraha hayajawahi kumpa nafasi ya kutosha.
Asante Kwasi (Simba)
Raia huyu wa Ghana aliwahi kuchukua nafasi ya Mohamed Hussein Zimbwe maarufu kama Tshabalala, lakini alipoumia na Kwasi akaipata nafasi sasa inaonekana ameishika vizuri na sasa ni presha kwake baada ya kupona na tayari kaanza mazoezi.
Gadiel Michael (Yanga)
Mmoja wa mabeki bora wa pembeni, Gadiel analazimika kubaki nje akiishuhudia Yanga ikipambana kutokana na kuwa majeruhi ya enka. Hata hivyo ndani ya kikosi cha Yanga anaonekana hana upinzani mkubwa sana atakaporejea, tayari ameanza mazoezi.
Jamal Mnyate (Lipuli)
Simba ililazimika kumuachia kwa kuwa alionekana alikosa kujiamini sana. Hali hii ilisababishwa na majeraha aliyoyapata mfululizo. Hivyo kupoteza ile hali yake ya kujiamini, baada ya kutua Lipuli alionekana ni msaada lakini sasa tena anaishuhudia timu akiwa jukwaani.
Salim Mbonde (Simba)
Kifundo cha mguu ndiyo tatizo kubwa na inaonekana aliumia vibaya. Karibu msimu mzima kama utajumlisha na uliopita. Akiwa fiti, vigumu kumuweka benchi kwa kazi yake nzuri.
Juma Mahadhi (Yanga)
Takribani nusu msimu unakwenda akiendelea kusota benchi. Licha ya umri mdogo, Mahadhi ameendelea kusota jukwaani kutokana na majeraha mfululizo.
Kelvin Kiduku (Mtibwa)
Kiduku ni kati ya washambulizi wenye uwezo mkubwa na njaa ya kufunga. Mambo yake yamekuwa magumu kutokana na kuandamwa na majeraha ya nyonga.
0 COMMENTS:
Post a Comment