December 28, 2018






NA SALEH ALLY
Mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Simba wamegaragazwa kwa kuchapwa mabao 3-1 yasiyo na ubishi dhidi ya timu ya daraja la tatu.

Timu iliyowang’oa inaitwa Mashujaa kutoka mkoani Kigoma. Mashujaa iliilazimisha Simba kusawazisha lakini mwisho ikashindwa kwa bao safi lisilokuwa na ubishi hata chembe.

Hakuna Mwanasimba aliyemlaumu mwamuzi kwa kushindwa kuchezesha haki bin haki kwa kuwa hakukuwa na malalamiko.

Baada ya Simba kutolewa kumekuwa na gumzo la kila aina mitandaoni. Zaidi ni kuhusiana na kipa namba mbili wa Simba, Deogratius Munishi “Dida”.

Mashabiki wa Yanga ndio wamenichekesha zaidi baada ya kumfananisha Dida na kipa wao Klaus Kindoki. Wamekuwa wakisambaza ujumbe unaosema kwamba hata Simba wana Kindoki wao lakini wamekuwa wakimficha!

Hayo ni mambo ya watani ambayo tunaweza kuwaachia. Lakini uhalisia ni kwamba Simba ni timu inayoundwa na wachezaji wanaojisahau mapema sana.

Kama unakumbuka, Kocha Joseph Omog alipoteza kibarua chake ikionekana kama vile alifanya mzaha timu yake kuvuliwa ubingwa wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Green Warriors. Hao ni mashujaa wengine waliowang’oa Simba kwa mikwaju ya penalti Chamazi Complex.

Safari hii Simba wameng’oka katika hali inayofanana tena ikiwa ni siku chache kufanya jambo kubwa kabisa, si kwa Simba pekee bali taifa zima la Tanzania na hasa kwa wapenda mpira.

Unajiuliza, vipi Simba wamefeli katika hatua hiyo dhidi ya timu iliyosafiri kwa basi hadi Dar es Salaam? Timu ambayo haina uzoefu na michuano yoyote ya kitaifa.

Timu ambayo haijawahi kucheza Uwanja wa Taifa na haina hata mchezaji mmoja wa kulipwa. Hili ni jambo la kujivunia kwa Mashujaa lakini Simba wajiulize tena huku wakimkumbuka Omog kwamba uzembe wa wachezaji ndio ulimfukuzisha kazi Mcameroon yule.

Leo, ungeweza kusema ni uzembe wa Patrick Aussems. Nimeona mitandaoni baadhi ya mashabiki wakimlalamikia kocha huyo kwamba alitoa mapumziko ya muda mrefu kwa wachezaji wake.

Hiki ni kichekesho kingine, hivi wachezaji wanapaswa kuchungwa kama wanyama kwa kazi yao wenyewe? Jambo kama hili limepitwa na wakati na kikubwa cha kuangalia kwa sasa ni weledi na si kuchungana kama mbuzi.

Ukiachana na hivyo, kwa pamoja tunapaswa kumpongeza kocha huyo Mbelgiji kwa kuwa amejitahidi kutoa nafasi kwa wachezaji wengine nao waweze kucheza mechi na kuonyesha kiwango chao.

Anajua ana kikosi kipana na kwa kocha mjuzi, angependa kutumia wachezaji tofauti katika mechi kama hiyo kuwapa nafasi ya kucheza nao waonyeshe walichonacho na inakuwa ni kwa faida ya wachezaji wenyewe na faida ya timu na hasa yeye kocha kujua silaha alizonazo nje zina nguvu kiasi gani na azitumie wakati gani anapokuwa ana uhitaji.

Sasa waliopewa nafasi ndio wamemuangusha na bahati mbaya bado anapokea lawama. Kama angekuwa anataka uhakika, angeendelea kutumia kikosi kilekile kilichoing’oa Nkana FC ya Zambia na uhakika angesonga mbele.

Wengine ambao wangebaki benchi, wangeishia kulalama tu kutokana na jambo hilo. Leo wamepewa nafasi wao ndio wamemwingiza Aussems katika hali ambayo hajaitarajia.

Kuna kila sababu ya wachezaji ambao mnapata nafasi kujiuliza na kuangalia mara mbili. Makosa yapo lakini vizuri kujali weledi sana.

Kocha ni kama dereva, kufanya kwake vizuri anahitaji uhakika wa gari lake ili safari iwe sahihi. Jifunzeni kuacha kudharau na kuingia uwanjani na matokeo.

Ukubwa wa Simba na mechi iliyopita kwa kuwa walimng’oa Nkana FC, basi wachezaji wakaingia kama wameshinda hata kabla ya kucheza.

Utaona, mwishoni baada ya kugundua Mashujaa FC hawatanii. Ndio wanajaribu kurejea katika mchezo na mwisho unaona kosa la wachezaji haohao limewamaliza.



3 COMMENTS:

  1. Acha uongo mashujaa wapo daraja la kwanza sio la tatu kabla hujaandika uwe unapitia kwanza taarifa zako

    ReplyDelete
  2. kuna wachezaji hawaonekani kubadilika hapo, wamejisahau kabsaa bila kujua kuwa hyo ni private sector any time unaachwa na anaingia mwngne, wamejiachiaaaaa,naamin watabadilika mechi vs Singida

    ReplyDelete
  3. Mashujaa waliifunga Simba Sc mabao 3-2 na sio 3-1

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic