December 11, 2018





Mwandishi mkongwe wa michezo nchini, Saleh Ally “Salehjembe” ameishauri La Liga kuwapa mafunzo waandishi wa michezo nchini ili wawe msaada mkubwa kwao kusambaza na kueleza ubora wa ligi hiyo ya Hispania.


Salehjembe amesema leo pale walipokutana waandishi wa michezo hasa soka na mwakilishi wa La Liga, Luis Cardenas ambaye yuko nchini.


Katika mazungumzo hayo ikiwa ni sehemu ya kuzungumzia mnasuala kadhaa ya mchezo wa soka na kushauriana, Salehjembe alisema kuna kila sababu ya La Liga kutoa mafunzo kadha.


“Mafunzo hayo yatolewe hasa kwa waandishi wanaochipukia, ianzie hapa Tanzania na ikiwezekana waende Hispania na kujionea zaidi kuhusiana na ubora wa ligi hiyo.

“Nimekuwa Hispania mara nne tofauti, nimeangalia mechi tofauti za La Liga, hakika ni ubora wa juu kuanzia kuingia uwanjani, wakati wa mechi na baada ya hapo.

“Mimi ninakuwa nina uelewa tofauti na wengine ambao hawajabahatika kufika huko. Wapeni nafasi waandishi wanaochipukia kwenda kujionea. Lakini kabla kunaweza kukawa na mafunzo kadhaa hapa nyumbani.

“Unapokwenda vitani wasaidie askari wako mafunzo ya kutosha. Sasa kama unataka wadau wajue zaidi kuhusiana na La Liga, basi wanaofikisha hizo habari wanatakiwa kuwa wamejitosheleza na waliojitosheleza hawazidi watatu kama nilivyo mimi,” alisema Salehjembe.


Cardenas alisema amepokea mawazo hayo ya mkongwe Salehjembe na kusisitiza lengo lao ni kuchukua maoni na kuyafanyia kazi kwa ufasaha zaidi.


“Tunalichukua hilo, tena kwa uzito kwa kuwa sisi ni watu tunaojifunza na tumelenga kuhakikisha watu wanajua mengi kuhusiana na La Liga ambayo ni zaidi ya soka,” alisema.

Kabla, Cardenas alizungumza kadhaa huku akieleza ubora na burudani ya La Liga namna ilivyo na kusisitiza ubora wake ni zaidi ya soka tu badala yake burudani na mengi ya kujifunza.


“Suala la burudani kupitia La Liga ni namba moja lakini La Liga ni zaidi ya mpira pekee kwa kuwa kuna mengi.



“Suala la kuburudika, kuwa pamoja, kujumuika na kujifunza mambo mbalimbali kuhusiana na utamaduni, maisha na kadhalika unaweza kuyapata,” alisema na kuongeza.

“Ukizungumzia suala la ubora kwa takwimu zilizopo sasa, La Liga ndio zaidi duniani. Angalia ubora wa Ulaya na hili halina mjadala.


“Sisi La Liga, tumekuwa tukiendelea kuboresha kila namna ya mambo kama ubora wa viwanja, uhakika wa usalama na kadhalika. Lakini lengo kuu ni kutengeneza kitu kilicho sahihi na kinachowezekana kuwa bora zaidi na zaidi.”

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic