January 28, 2019


Beki wa kati wa Azam FC, Mghana, Daniel Amoah, amerejesha matumaini kwenye kikosi cha Mholanzi, Hans van Der Pluijm kinachoshiriki Ligi Kuu Bara baada ya kupona majeraha yake ya goti.

Beki huyo alipata majeraha hayo mwishoni mwa msimu uliopita wa ligi kabla ya kusafirishwa kwenda kufanyiwa upasuaji nchini Afrika Kusini. Safu ya ulinzi ya Azam hivi sasa inaongozwa na Aggrey Morris na Daniel Yakubu ambaye naye ni raia wa Ghana.

Kwa mujibu wa Championi Jumatatu, meneja wa timu hiyo, Phillip Alando, alisema beki huyo tayari ameanza mazoezi mepesi ya uwanjani kabla ya kuanza magumu ya pamoja na wenzake.

Alando alisema, beki huyo anaungana na kiungo mkabaji, Frank Domayo na winga machachari, Joseph Kimwaga, wote walikuwa na majeraha ya goti, kwa ajili ya kufanya mazoezi mepesi.

Aliongeza kuwa, kiungo wao mshambuliaji Mzimbabwe, Tafadzwa Kutinyu, anasubiria kufanyiwa kipimo cha MRI kwenye goti lake baada ya kupata majeraha ya goti kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Mapinduzi walipokutana na Simba.

“Ni habari njema kwa mashabiki wa Azam kuwa wachezaji wao muhimu katika timu tayari wameanza kurejea uwanjani kwa kuanza mazoezi mepesi akiwemo Amoah.

“Amoah ameungana na wachezaji wenzake wengine wawili ambao ni Domayo na Kimwaga waliopona majeraha ya goti wote.

“Wameanza na program ya kukimbia mbio fupi na ndefu uwanjani huku wakifanya yale ya viungo kabla ya kuanza kufanya magumu pamoja na wenzao katika kujiandaa na mechi zijazo za ligi,” alisema Alando.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic