January 7, 2019




Na Saleh Ally
NIMEJIFUNZA namna ambavyo ukimya unaweza kuwa na nguvu zaidi ya maneno au sauti za watu elfu kumi.


Wakati mwingine unapaswa kuwa kimya ili kujibu vizuri hoja za wengi hasa zile ambazo unaziona hazina msingi.


Wiki iliyopita, watu wasiojitambua wakiambatana na wale wanaoendesha mitandao ya kijamii ya Yanga waliamua kulisakama Gazeti la Championi kwa madai kwamba eti linawasakama na kutaka kuwaangusha wakati wakiwa wameungana katika kipindi hiki kigumu. Wanaolala, wengi hata kilichoandikwa hawakusoma.


Baada ya hapo, wengi ambao binafsi niliona kuwajibu ni kufanana nao waliendelea kusambaza kwamba eti watu wasisome Championi kwa kuwa linaiandama Yanga!


Ukimya wa siku mbili ulikuwa majibu tosha kwao kwamba kuna aina ya watu unaweza kuzungumza nao na wengine ukawanyamazia kuwapa majibu sahihi. Kuishi ni kujifunza, huenda hii ikawa ni silaha kuu ya baadaye.


Stori waliyokuwa wanaipinga ni kuhusiana na baadhi ya wachezaji waliohojiwa na Championi kutokubaliana na hali ya nahodha wao, Kelvin Yondani kuvuliwa unahodha. Wachezaji hao wanaonyesha nia yao nzuri kwa timu na wamesema ukweli huku wakiomba kocha ampe nafasi Yondani kujieleza kuliko kuchukua uamuzi.


Yanga waliokuwa wanakanusha, kipi sasa? Wanakanusha kwa niaba ya wachezaji? Wanachokanusha ni mawazo na hisia za wachezaji ambacho wanakiona ni bora na kinaweza kusaidia mwenendo wa timu yao kwenda vizuri.


Sasa viongozi wao ni wachezaji na Yanga unajua haina mwenyekiti wala makamu wake. Hao wanaokanusha ni akina nani? Wana chuki kwa kuwa mara kadhaa tumehoji kuhusiana na mwenendo wa kifedha kwamba ndani ya Yanga bado fedha zinapatikana na kuna wale ambao wanaweza kuwa wanafaidika na ule msemo wa “Yanga ina Njaa” na fedha zinapatikana na wakati mwingine hazifanyiwi kinachotakiwa.


Najua hawawezi kutuzuia kuhoji, hawana ujanja wa kuwazuia watu wasikipende wanachotaka na ninajua wengine hawajui kwamba wanatumiwa na wale wanaofaidika na kamwe hatuwezi kuwahofia hata kidogo.

Tutafanya kazi yetu kwa weledi bila ya woga na tuwaahidi ushirikiano kama ambavyo wamekuwa wakiomba tuwasaidie ili watu wajitokeze kuchangia zaidi na tukafanya.


Ila, unapofikia wakati wa kuhoji, basi tutahoji sana bila ya woga hata kidogo. Utakapofikia wakati wa kukosoa, hilo nalo litafanyika kwa weledi wa juu bila ya kuhofia chochote kile. Kazi yetu si muziki, kwamba tunataka kuwafurahisha watu kuanzia mwanzo hadi mwisho wa shoo.


Mwisho, niweke msisitizo katika hili na ndilo limenisukuma kuandika makala haya, la sivyo ningekuwa kimya tu kuendelea kuwajibu kwa ukimya hasa wale ambao badala ya hoja wanatukana, binafsi nawaona ni watu wasiofaa kujibiwa kwa hofu ya kufanana nao.


Kilichonisukuma kuandika makala ni kuwakumbusha Yanga kwamba Kocha Mwinyi Zahera ni mwanadamu. Ana uwezo wa kufanya mazuri na tumekuwa tukiona, jambo ambalo tumekuwa tukimpongeza na kumpa ushirikiano mkubwa hata mwenyewe analifahamu hilo.


Pamoja na hivyo, mkumbuke upande wake wa pili kwamba Zahera ni mwanadamu, anaweza kukosea na kama vile anavyosifiwa akipatiwa, basi akosolewe anapokosea.


Acheni uoga wa kizandiki, acheni maneno “choshi” yasiyo na hoja eti mnasambaratishwa pale tu Zahera anapokosolewa. Msiwe dhaifu hivyo kwa kuwa inapofikia kocha amekosewa, anaweza kurudishwa njiani kwa kuelezwa ukweli.


Kwamba Zahera akikosea, basi mtaendelea kunyamaza kwa hofu ipi, hatatoa fedha tena? Makosa yake na hasa za anachokosea huenda yakawa na gharama kubwa zaidi baadaye.


Kuweni wanadamu mnaojiamini, shida isiwashushe na kuwafanya dhaifu msiojiweza. Pia nawakumbusha, anachofanya Zahera kwa kipindi hiki ni utatuzi wa muda mfupi ambao hautamaliza matatizo ya Yanga.


Matatizo ya Yanga yatamalizwa na mipango ya muda mrefu ambayo inapaswa ianze kufanywa sasa badala ya Yanga hii isiyokuwa na uongozi mkuu. 


Najua, mngependa Yanga iendelee kubaki hivi mkitumia kigezo cha timu kushinda kama ngao ya kuficha yale mnayoendeleza chinichini na kuitafuna klabu kimyakimya. Lakini mjue, Yanga ni ya Watanzania, mwisho wake mtaangukia pabaya.


Hivyo, kuweni imara kuisaidia Yanga leo, kesho na baadaye. Msaada wa Zahera pekee, hautaikomboa Yanga. Michango ya majukwaani pekee haitaikomboa Yanga. Acheni kujidanganya na kuwadanganya mashabiki kwa kuwa mnaendelea kutengeneza tatizo kubwa la baadaye.


Wekeni wazi fedha za wadhamini zinatumikaje, nini kifanyike. Bajeti yenu kiasi gani na mnapungukiwa kiasi gani badala ya michango ya kila siku isiyo na mahesabu ambayo mwisho kabisa, itawageukia.

Zahera aendelee kuwa msaada sasa, lakini anapaswa kusaidiwa na kupongezwa lakini msisitizo tena, akikosea, aelezwe na huo ndiyo ubinadamu.





8 COMMENTS:

  1. Ndio maana blog hii
    imepoteza weledi kwa sababu ya mikwara ya Yanga!!
    Mnajaribu sana kuwaridhisha kwa kuwapamba sana.Sasa wanadai hamna haki ya kuwakosoa kwa sababu mliwazoeza.
    Huu ni mwanzo mzuri wa kusema ukweli bila kuegemea popote.Pesa za ufadhili kutoka Sports Pesa na Azam zimetumiwaje?
    Hakuna anayeweza kuhoji ingekuwa ni Simba yangeandikwa makala 100 kuulizia.

    ReplyDelete
  2. Alichokifanya Papaa Zahera hata mimi sikiafiki, lakini Sareh mbona unateseka kuna nn?

    ReplyDelete
  3. Huyu Salehjembe atakuwa ni mke wa mtu sio bure

    ReplyDelete
    Replies
    1. Sio lugha nzuri kaka hata kama humpendi Saleh

      Delete
  4. Afadhali we we kichwa cha habari kinaendana na yaliyomo ndani..wandishi wako wa Tania mbaya ambayo wanairudia tena na tena kuandika vichwa vya habari ambavyo ndani yanayoandikwa ni tofauti nje kabisa.pia hawajitambulishi

    ReplyDelete
  5. Hawa ndiyo wachambuzi wa soka la Bongo weneye kutaka kuuza magazeti kwa vichwa vya habari!

    ReplyDelete
  6. Mimi najikita kwenye hoja.poul pokba alivishwa na kisha akavuliwa unahodha na kocha jose.h apa nyumbani jonas mkude alivuliwa unahodha akapewa kijana mdogo beki is.haka.tena hili lilikua kubwa kwa kupima,kiwango cha mafanikio yao ktk timu.salehe hili hukuwahi kuandika,kuwahoji,wachezaji wengine.kama sivyo tupe kumbukumbu.ktk soka maamuzi ya kiongozi wa wachezaji ni ya kocha.na hakuna maamuzi ya kiumbe yoyote yanayokosa upinzani.kuna watu wajuta kuzaliwa huo si upinzani kwa mungu?kuandika mawazo yako na kutumia matusi yenye nguo ni moja ya magonjwa wanayoumwa waandishi wetu.ktk kizazi hiki.tunaandaa michuano ya vijana imeandikwa vya kutosha?kuna mapinduzi cup nayo vipi?jina yanga ni kubwa na linaweza kukupa wasomaji wengi,aidha wapenzi wa yanga au maadui zake.waandishi mmekua na hasira,mapenzi ya wazi,chuki banafsi,na uvivu wa kufikiri.

    ReplyDelete
  7. Mimi ushauru wangu kwa mwandishi kabla ya kuchapisha habari aliyoikusudia inabidi aipitie upya kuisoma kama kuna makosa ayarekebishe kabla ya kuichapisha, habri inayosomwa na watu wengi nini maana ya neno (Mkataba) katika kichwa cha habari hii jitahidi kuwa mwangalifu sana juu ya uwandishi wako/maandishi yako.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic