January 28, 2019


Hivi karibuni uongozi wa Simba unadaiwa kuajiri shushushu kimyakimya bila ya wachezaji wa timu hiyo na benchi la ufundi kujua baada kupata taarifa za mara kwa mara za wachezaji wa timu hiyo kutoroka kambini na kwenda kufanya starehe.

Wiki hii shushushu huyo aliwachoma baadhi ya wachezaji waliochomoka kambini hapo kabla ya mechi dhidi ya Bandari na kufanya viongozi kuvamia kambi hiyo kufanya rokoo.

Habari za kuaminika kutoka ndani ya Simba ambazo Spoti Xtra limezipata zimedai kuwa baada ya viongozi hao kufanya rokoo hiyo waliondoka zao na baadaye walizungumza na kocha mkuu, Patrick Aussems na kumwambia jambo hilo.

“Kocha alishtushwa na hilo ndipo na yeye akafanya uchunguzi wake ili kubaini kama ni kweli wachezaji hao walitoroka kambini. Baadaye aligundua kuwepo kwa mtu katika kambi hiyo ambaye alijitambulisha kuwa ni mlinzi na ameletwa hapo na viongozi kwa ajili ya kusaidiana na mlinzi wa siku zote wa kambi hiyo,”kilidokeza chanzo chetu.

Alipoulizwa kuhusiana na hilo, Aussems hakuwa tayari kufafanua lakini mlinzi wa timu hiyo Ngande Ngalambe alisema kuwa: “Kilichotokea ni kwamba, baada ya kumalizika kwa mechi yetu na FC Leopards ya Kenya Jumatano iliyopita wachezaji kama watano hivi walimuomba ruhusa kocha kuwa wana matatizo ya kifamilia hivyo wanataka wakayatatue mara moja kisha watarudi kambini siku hiyohiyo.”

“Kocha aliwaruhusu ila walichelewa kurudi, wakati viongozi hao wanafika hawakuwakuta wachezaji hao lakini wakati wanajiandaa kuondoka baadhi walikuwa tayari wameisharudi kwa hiyo si kweli kabisa kuwa walitoroka ndiyo maana hata kocha alishituka.”

Wachezaji wanaodaiwa kutoroka kambini ni Haruna Niyonzima, Jonas Mkude, Mzamiru Yassin, Pascal Wawa, Hassan Dilunga, Shiza Kichuya na Mohammed Ibrahim, huku mastaa wengine akiwemo Emmanuel Okwi wakikutwa kambini.

CHANZO: SPOTI XTRA

1 COMMENTS:

  1. Ndiyo maana timu zinafungwa tu ovyo, kumbe hata nidhamu ni shida. Halafu kama mwandishi ameandika vizuri, hapa kuna vitu vinazungushwa ili tulioko nje ya mfumo tusijue. Mimi ni shabiki wa Yanga lakini naisapoti sana Simba kwenye mashindano ya kimataifa kwani nyie ndiyo wawakilishi pekee kwa hiyo mnabeba bendera ya Taifa, ila mkiendekeza mambo haya, tutaambulia patupu. Ningeomba wachezwaji waonywe kwa vile wamegundulika mara ya kwanza ila kama itajirudia ni kuchapa adhabu tu.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic