January 27, 2019







NA SALEH ALLY
MICHAEL Richard Wambura ni mbishi sana! Lazima unatambua hii si kauli yangu na huenda ni ya wapenda mpira wengi wamekuwa wakiizungumza.


Hii ndio imekuwa sifa ya Wambura, mdau wa michezo ambaye nilianza kufahamiana naye wakati akiwa katika lile kundi la marafiki wa Simba, maarufu kama Friends of Simba.


Kumekuwa na historia yake kwamba aliwahi kuongeza michezo mingine kadhaa, lakini sikuwahi kufahamiana naye kabla. Nimebahatika kufanya naye kazi kama wadau nikiwa mwanahabari naye akiwa kiongozi, kuanzia akiwa Friends of Simba, Fat na baadaye TFF.


Kwangu siwezi kuwa na tatizo na Wambura, lakini siwezi kutetea kila alichofanya kwa kuwa vitu vingine sijui ni sahihi au la, ndiyo maana vimekuwa vikiamuliwa na kamati ambazo zinahusika.


Bahati mbaya moja tu, katika muda wa takriban miaka 15 hivi tokea nimemfahamu Wambura katika tasnia ya michezo na hasa soka, amekuwa akipambana tu.


Nakumbuka mara ya kwanza aliingia Fat kwa kumshinda Ismail Aden Rage akiwashangaza watu wengi, bosi wake akawa Muhidini Ndolanga, mmoja wa vigogo wa Fat wakati huo na walikuwa hawakamatiki hata kidogo.


Baadaye, tukiwa Mwanza katika michuano ya Chalenji, Wambura aliingia kwenye shida ya kusahau kutuma majina ya timu zitakazoshiriki michuano ya Klabu Bingwa na Kombe la Washindi. Ikawa kashfa kubwa na ikamhangaisha sana.
Mwisho aliishia kupambana. Baadaye aliamua kurejea Simba ambako pia aliishia kupambana na unaona baada ya ukimya wa muda mrefu, Wambura akarejea TFF, safari hii akiwa makamu wa rais.





Ingawa hakuwa amepewa nafasi ya kushinda, lakini alirejea na kupata ule ushindi wake wa kushitukiza kama ilivyokuwa wakati wa Fat. Pamoja na hivyo, baada ya muda mfupi wa uongozi, ameendelea kupambana.


Mara nyingi Wambura hakai muda mrefu madarakani au ikiwezekana huwa hamalizi muda wake, huishia kupambana. Huenda hili ndilo lile jina la "Wambura Mpambanaji", linanipa maswali sana, mwisho wake wa kupambana hasa ni upi?


Kwani mwisho wa Wambura kupambana utakuwa ni upi? Najiuliza kwamba kwani bila ya kuongoza mpira, Wambura hawezi kufanya mambo yake mengine? Lakini kama kweli anapenda kuwa kiongozi, vipi kila siku yeye tu hawezi kumaliza muda wake bila ya kuingia katika matatizo yanayomlazimisha kupambana?


Hapohapo, bado najiuliza, hivi kweli watu wote huwa hawampendi Wambura, aliwakosea nini maskini? Maana tokea Fat, Simba na sasa TFF, kuna nini hasa? Tatizo ni wale watu au yeye mwenyewe? Na kama ni hao watu, mbona ni watu tofautitofauti na nyakati tofauti?


Ulisikia TFF walivyomfungia Wambura kupitia Kamati ya Maadili iliyokuwa ikiongozwa na marehemu, Hamidu Mbwezeleni lakini Wambura "mbishi" akaifuata haki mahakamani na kufanikiwa kurudishwa madarakani kwa ile hukumu iliyotoka Novemba 30, mwaka jana katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kupitia Jaji Benhaji Masoud.


Kabla hata Wambura hajaanza kazi, hukumu kutoka Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), imetangaza kumfungia kujihusisha na masuala ya michezo maisha! 




Wakati watu wakitafakari, nimeambiwa Wambura hajaacha ubishi, ameamua kuwapandia Fifa na mwanasheria wake, Emmanuel Muga ambaye kitaaluma pia ni mwanahabari, amesema kulikuwa na upotoshaji kutoka TFF na wanachofanya ni kuwasiliana na Fifa kwa ajili ya kutoa ufafanuzi.


Kamwe sipingi kabisa Wambura kugombea haki zake za kimsingi, lakini maswali yaleyale najiuliza, asipokuwa kiongozi wa soka, hataishi maisha mazuri?


Unajua haiwezekani Wambura akawa hana tatizo halafu akawa na matatizo na karibu kila anaokuwa nao karibu kiuongozi. Mara nyingi nimepinga sana masuala ya makundi na hasa baada ya uchaguzi.


Wakati wa Fat na baadaye TFF, suala la makundi limekuwa kubwa sana na watu hawakubali hili. Tunajua Wambura ni kambi ambayo haiendani na ile iliyo madarakani na huenda hawaelewani iwe tatizo ni yeye au wao.


Pamoja na hivyo, hatukuwahi kuambiwa tuhuma za ubadhilifu anazotuhumiwa si sahihi baada ya kuelezwa. Tuliamini TFF inamuonea, lakini leo na Fifa pia imempa adhabu kubwa kabisa. Pamoja na wakili wake kusema wamepotoshwa, najiuliza Fifa hadi wanafikia kumfungia mtu maisha, wanaweza kukurupuka tu kweli?


Wambura naye ni mwanadamu, ingawa anaupenda mpira angeweza kujifunza kwa kujiuliza vipi watu wote wamchukie kama ni kweli? Au wapingane naye kila mara hali inayomlazimu kupambana kila kukicha kubaki katika nafasi!
Unaona hata alipokuwa kiongozi anakuwa hana muda wa kuonyesha uwezo wake kikazi maana lazima atakuwa anapigania abaki madarakani tu, jambo ambalo si zuri hata kidogo.


Nawakumbusha ule msemo “Gari linalovutwa, hali overtake”. Kuna kila sababu ya Wambura kuangalia muda wake, maana umri nao ndio unakwenda. Badala ya kubaki na ubishi wa kutaka madaraka, basi anaweza kuendelea kuwa mbishi kusaka maendeleo mengine. Maana hawezi kusema kuwa madarakani ndio maendeleo.


Kama anataka kuendelea kubaki kuwa mbishi wa kuhakikisha anakuwa madarakani kwa "kuipata haki yake", basi bado ana nafasi ya kujitafakari pia, kwa kuwa haitawezekana ikawa watu wote wanasigana naye kwa uzawa tofauti na ikabaki watu tu ndiyo wana matatizo dhidi yake.



1 COMMENTS:

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic